Familia yataka haki kijana aliyedai kuvunjwa mguu na polisi

Muktasari:
- Mjomba wake, Ezekiel Mollel amesema licha ya kutoa taarifa polisi, hakuna hatua zilizochukuliwa kwa zaidi ya siku 100 sasa.
Arusha. Familia ya kijana aliyedai kupigwa hadi kuvunjwa mguu na askari polisi ndani ya chumba cha mahojiano, wamelitaka Jeshi la Polisi kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Kijana huyo, Peter Charles (21), mkazi wa kata ya Daraja Mbili jijini Arusha, alidai kupigwa hadi kuvunjwa mguu na askari polisi, akimlazimisha kukiri kosa la kujihusisha na kucheza kamari.
Mei 29, 2024 saa moja usiku, wakiwa watatu nyumbani kwa mmoja wa rafiki yao wakitazama runinga, askari waligonga mlango na kuingia, wakajitambulisha kuwa wao ni askari, wakawabeba kuwaingiza kwenye gari walilokuja nalo.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao, leo Septemba 18, 2024, walezi wa kijana huyo, wamesema tangu kutokea kwa tukio hilo, hakuna hatua zilizochukuliwa kwa mtuhumiwa, ikiwemo kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kijana Peter Charles (21) akiwa nyumbani kwao
Mjomba wa kijana huyo, Ezekiel Mollel amesema tangu kijana wao afanyiwe ukatili huo Juni 6, 2024 hadi sasa, hakuna hatua iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi dhidi ya mtuhumiwa, ili kutenda haki kwa usawa unaostahili kwa mujibu wa sheria.
“Tangu kijana wangu avunjwe mguu na huyo askari wa polisi, ni zaidi ya siku 100 zimepita, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa, kwani bado yuko kazini na hajafikishwa mahakamani, yeye pia haoni kama amefanya kosa, aombe radhi,” amesema Mollel.
Amesema baada ya kupata kadhia hiyo, walikwenda kutoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ambapo waliitwa kutoa maelezo, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea wala majibu ya maelezo hayo.
“Tumepitia mengi katika kumuuguza kijana wetu, lakini haiwezi kuishia hivi kwa sababu naye ni binadamu. Licha ya kuwa ametoka familia ya kimaskini, lakini anahitaji haki ya damu yake iliyomwagwa ndani ya kituo cha polisi, hivyo tunaomba Serikali na Jeshi la Polisi litende haki kwa kijana wangu.
“Kikubwa tunataka tuone hatua za kisheria zikichukuliwa, kwani kunyamazia hivi inazidisha vitendo vya vitisho vya maisha yetu, pia imani na jeshi hilo inapungua na zaidi ushirikiano utatoweka kwa jeshi hilo,” amesema Mollel.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema bado suala hilo linashughulikiwa katika hatua za awali na likikamilika hatua za kimahakama zitafuata.
“Tunashughulikia, bado liko ngazi za chini na likikamilika litafikishwa ngazi ya kimahakama, hivyo subirini tu,” amesema Kamanda Masejo.
Bibi wa kijana huyo, Getrude Mollel (61) ameiomba Serikali kuchukua hatua za kisheria, ili mjukuu wake apate haki na pia iwe fundisho kwa wengine.
“Huyu kijana niliachiwa na mwanangu tangu akiwa na mwaka na miezi sita, nimemlea na kumsomesha huku akipigania ndoto zake za kuwa mwanajeshi, leo amekamatwa bila kosa na kuvunjwa mguu. Hata kama angekuwa mhalifu, ndiyo astahili adhabu hii? Naomba Serikali iseme jambo,” amesema bibi huyo.
Akizungumzia hali yake, Peter amesema anaendelea vizuri, ingawa bado anapitia maumivu makali ya mguu na nyonga kukaza hasa nyakati za usiku.
“Maumivu niliyopitia ni makubwa, ingawa sasa hivi kwa jitihada za madaktari wa Seliani na ndugu zangu kunifuatilia kwa upande wa matibabu, hali inaendelea kuimarika na maumivu yanapungua, ingawa bado usiku nateseka kulala,” amesema.