Familia yalia ndugu yao ‘kutekwa’

John Lukonge, mkazi wa Mkurunga mkoani Pwani anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Mkuranga/ Dar. Jinamizi la watu kupotea au kutekwa huenda limeanza kurejea baada ya John Lukonge (40), mkazi wa Mkurunga mkoani Pwani kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana siku 14 zilizopita na mpaka sasa haijulikani alipo.
Familia ya Lukonge imepaza sauti kwa mamlaka mbalimbali kuomba isaidiwe kupatikana kwa ndugu yao akiwa hai kutoka kwa watekaji hao waliomchukua usiku wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser.
Mazingira ya kuchukuliwa kwa Lukonge yanataka kufanana na jinsi alivyotekwa ama kupotea aliyekuwa mwandishi wa gazeti hili wilayani Kibiti, Azory Gwanda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo mkoani Kigoma, Simon Kanguye takriban miaka sita iliyopita ambao mpaka sasa haijulikanani kama bado wapo hai ama wameshafariki dunia.
Azory alitekwa na watu wasiojulikana Novemba 21 mwaka 2017. Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni, asubuhi ya siku hiyo watu wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walifika katikati ya Mji wa Kibiti sehemu ambayo mumewe alikuwa akipatikana mara kwa mara na kumchukua kwamba kuna kazi wanaenda kuifanya na angerejea itakapokamilika.
Baada ya kumchukua, watekaji hao walienda shambani alikokuwa analima, ulikuwa muda wa saa nne asubuhi na walipofika, (Azory, aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma) alimwita (Anna) na kumuuliza alikokuwa ameuficha ufunguo wa nyumba yao.
Anna alisema alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumwelekeza alipouweka ufunguo huku Azory akimwambia amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo (Novemba 21) basi angerudi siku inayofuata, yaani Novemba 22.
Hata hivyo, hadi sasa, Azory hajulikani alipo na juhudi za kuendelea kumtafuta zinaendelea kwa matarajio kwamba siku moja ataonekana ili aungane na familia yake na kuonana na mwanaye ambaye hajawahi kumwona kwani aliondoka wakati wa ujauzito wake.
Tukio la Azory, halitofautiani na la Lukonge ambalo ndugu zake wamelieleza gazeti hili kuwa siku anatekwa watu kadhaa ambao hawakufahamika walikuja nyumbani kwake na kuegesha kwenye gari aina ya Land Cruiser, nje ya nyumba aliyokuwa anaishi siku zote.
Mmoja wa ndugu wa Lukonge, alisema “Maliki alipotoka nje walimkamata na wakamsukumia ndani ya gari na kuondoka naye. Tulipomfuatilia tulipata namba za gari” ambazo kwa sasa gazeti hili imezihifadhi.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ali alipotafutwa kulizungumzia tukio hilo alisema taarifa hizo hazijui.
“Hapana sina hiyo taarifa, wasiliana na OCD (mkuu wa polisi wa wilaya) labda anaweza kuwa na taarifa,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa ujumbe mfupi wa maneno alioliandikia gazeti hili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rufiji, Protus Mutayoba kwa upande wake alisema “ndugu mwandishi wa habari, nakuomba uje ofisini kwangu kesho (leo) nitalizungumzia tukio hilo, karibu sana.”
Jinsi Lukonge alivyotekwa
Ndugu mwingine wa Lukonge ambaye ameomba kuhifadhiwa jina lake alisema ndugu yao aliyekuwa akiishi eneo la Koragwa, Dundani umbali wa kilomita tatu kutoka Mkuranga Mjini alipoishi kwa miaka 20 sasa, hajaonekana tena na familia yake haijui alipo.
Alisema wakati Maliki akitekwa, watu hao walisimama mahali hapo kwa dakika 20 kisha wakaliondoa gari na kuelekea Mkuranga Mjini. Baada ya gari hilo kuondoka, alisema na ndugu walianza kulifuatilia na lilipofika Kisemvule lilisimama kwa muda kumshusha mtu waliyekuwa naye ndani.
“Aliyeshuka kwenye gari alikuwa mrefu, mwembamba na alivaa t-shirt, pensi na kapero. Sisi tuliamua kutangulia mbele hadi eneo la viwanda vya Bakharesa hadi kilipo kituo cha polisi tukawapa taarifa lakini waliiacha gari hiyo ipite bila kuisimamisha,” alisimulia ndugu huyo.
Baada ya kuliacha gari hiyo lipite bila kulisimamisha, alisema polisi waliwataka ndugu hao walioambatana na vijana wengine wawe na subira kwamba ndani ya saa 24 wangepewa taarifa lakini haikuwa kama walivyoambiwa .
“Siku ya pili (Alhamisi) ndugu tuliamkia Kituo cha Polisi Maturubai, Chang’ombe pamoja na Stakishari, kote hakukuwa na taarifa zake jambo linaloendelea kutuacha njiapanda,” alisema.
Hata hivyo, alisema amekuwa akiwasiliana na kamanda wa Kanda Maalumu ya Rufiji pamoja na kamanda wa Wilaya ya Mkuranga lakini hawajapata msaada wowote mpaka sasa hali inayowatia wasiwasi wa kinachoendelea kwa ndugu yao.
Mbali na kutekwa kwa Lukonge na Azory ambayo ni mwendelezo ya watu kupotea mkoani Pwani na Dar es Salaam.
Miongoni mwa waliopotea ni aliyekuwa msaidizi wa Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Ben Saanane.
Desemba 26 ya mwaka 2021, vijana watano wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ambao ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe wanadaiwa kutekwa wakiwa maeneo ya Kariakoo na mpaka sasa hivi hawajulikani walipo, licha ya juhudi kadhaa za kuwatafuta zilizofanywa na ndugu zao.