Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Epuka haya unapohidfadhivyakula katika jokofu lako

Muktasari:

Watu wengi, hususan maeneo ya mjini hutumia majokofu kuhifadhi vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Vyakula vibichi na vilivyopikwa vinafaa kuwekwa katika jokofu, lakini jambo la kuzingatia ni muda na upangiliaji wa chakula.

Watu wengi, hususan maeneo ya mjini hutumia majokofu kuhifadhi vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Vyakula vibichi na vilivyopikwa vinafaa kuwekwa katika jokofu, lakini jambo la kuzingatia ni muda na upangiliaji wa chakula.

Je, unafahamu namna bora ya kuhifadhi chakula chako katika jokofu, ili kiendelee kuwa na virutubisho? Mwananchi imefanya mahojiano na Mtaaalamu na Ofisa Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Kaunara Aziz ambaye anasema kabla ya kuhifadhi chakula unapaswa kuangalia mfumo wa umeme katika jokofu kama upo vizuri.

“Kwa kawaida majokofu yenye sehemu mbili kwa maana ya mlango wa juu na chini, yanatakiwa kusetiwa nyuzijoto kuanzia sifuri hadi jotoridi 7°C, ili chakula ama kinywaji kiweze kuhifadhiwa kwa muda mrefu,” anasema.

Anasema chakula kikihifadhiwa katika nyuzi inayotakiwa hukaa muda mrefu bila kuharibika, kwani hupunguza uzalishaji au ukuaji wa wadudu, hususani bakteria wanaoharibu chakula.

Mtafiti huyo wa masuala ya lishe anashauri chakula kilichopikwa kihifadhiwe kwa muda usiozidi siku tatu, huku chakula kibichi kama mboga mboga na matunda navyo havitakiwi kuhifadhiwa kwa muda mrefu, kwani vitapoteza ubora na virutubishi vyake.

Anasema nyama, samaki na kuku inapaswa kukaa kwenye jokofu kwa siku mbili hadi tano, wakati mbogamboga na matunda zinapaswa kukaa siku tatu hadi siku tano, huku saladi zinapaswa kukaa siku tatu hadi nne.

Maelezo hayo yanaungwa mkono na Ofisa Mtafiti Mwandamizi wa sayansi ya chakula kutoka TFNC, Francis Modaha, anayesema nyama na samaki zinapaswa kuwekwa mapema katika jokofu pindi zinapotolewa buchani au kuvuliwa (kwa samaki).

Modaha anasema nyama inaponunuliwa inapaswa kwanza kuoshwa ndipo ikatwekatwe, ili isipoteze virutubishi na madini yaliyopo.

“Pia tunashauri mtu akinunua nyama, mfano kilo tano anatakiwa kuiosha na kuikatakata vipande vidogo, kisha kuweka katika vyombo maalumu vya plastiki vinavyotumika kuhifadhia chakula.

“Ni muhimu kuigawa katika posheni, ili iwe rahisi wakati wa upikaji, badala ya kuchukua nyama yote na kuyeyusha. Hii itasaidia nyama inayobaki kuwa na ubora ule ule,” anasema Modaha.

Pia katika uhifadhi wa matunda kama ndizi, anasema inapaswa kuhifadhiwa katika baridi ndogo, ili kuepuka kuungua na kubadilika rangi kutoka njano hadi nyeusi.


Madhara ya kuhifadhi vyakula muda mrefu

Aziz anasema vyakula vilivyokaa muda mrefu kwenye jokofu hupoteza au hupungua ubora pamoja virutubishi.

“Uhifadhi wa vyakula kwenye jokofu kwa muda mrefu unaweza kusababisha bakteria kuzaliana na kusababisha kupata madhara ya kiafya kama kuhara na magonjwa mengine.

“Chakula pia hupoteza virutubishi na husababisha mazalia ya bakteria, hasa tunapohifadhi katika eneo ambalo sio safi,” anasema.


Namna bora ya kuhifadhi vyakula

Mtaalamu huyo wa lishe anashauri vyakula vihifadhiwe kwa kutenganishwa kulingana na uasili wake.

“Mfano vyakula kama mbogamboga vinapaswa vitenganishwe na vyakula vya jamii ya nyama, huku vyakula vilivyopikwa viwekwe ngazi ya juu ya jokofu, huku vibichi vihifadhiwe ngazi za chini za jokofu, sehemu yenye barafu ili visiharibike haraka.

“Pia ni vema vyakula vinavyohifadhiwa kwenye jokofu vifunikwe au viwekwe kwenye chombo chenye mfuniko, ili kuepuka kuzaliana kwa bakteria,” anafafanua.

Je, vyombo gani ni sahihi kuhifadhi vyakula kwenye jokofu? Mtaalamu huyo anasema si sahihi kuhifadhi chakula kilichopo kwenye sufuria kwenye jokofu.

“Hii sio njia sahihi ya kuhifadhi chakula, mara nyingi sufuria haziwi katika hali ya usafi, kwani huwa na mabaki ya chakula pembeni au nje ya sufuria.

“Tafiti zinaonyesha chakula kinachohifadhiwa kwenye sufuria za chuma kwenye jokofu huharibika haraka kuliko kile kinachohifadhiwa kwenye vyombo vingine,” anasema.

Hivyo, anasema kwa ajili ya afya bora, ni vizuri vyakula vihifadhiwe kwenye vyombo vya aina ya plastiki.

“Vyombo hivi pia vinapaswa viwe safi na pia viwe na mfuniko, ili kuepusha vyakula kumwagika au kuchuruzika kwenye jokofu. Pia chombo kioshwe kila unapoweka chakula kingine,” anasema.


Usafi wa jokofu

Mtafiti huyo anasema watu wengi hawana utaratibu wa kuosha majokofu yao mara kwa mara, hali inayoweza kusababisha mazalia ya vijidudu vya magonjwa.

Wataalamu hao wanashauri jokofu lioshwe kila wiki kwa maji safi na sabuni na lifutwe vizuri kwa kitambaa safi kabla ya kuendelea kutumika.

“Kabla hujaweka vyakula na vingine kama matunda na baadhi ya mbogamboga vinapaswa kuoshwa kwa maji safi na kukaushwa vizuri ndipo vihifadhiwe kwenye jokofu,” anasema Modaha.