DPP amfutia kesi Mkurugenzi Jatu

Muktasari:
- Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umasikini (JATU PLC), Peter Gasaya, aliyekuwa anakabiliwa na kosa la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, amefutiwa kesi baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuonyesha nia ya kutoendelea na kesi hiyo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umasikini (JATU PLC), Peter Gasaya, aliyekuwa anakabiliwa na kosa la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuieleza Mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Gasaya alikuwa akikabiliwa na shtaka moja la kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya JATU kwa madai kuwa fedha hizo anazipanda ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Amefutiwa kesi hiyo leo, April 11, 2023 na hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Mary Mrio, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Mshtakiwa huyo hao amefutiwa shtaka lake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Akimfutia kesi hiyo, Hakimu Mrio amesema kutokana na hati hiyo iliyowasilisha chini ya kifungu hicho, Mahakama ina inamwachia huru mshtakiwa kwa sababu upande wa mashtaka hawana nia ya kuendelea na kesi dhidi washtakia.
Muda mfupi baada ya kufutiwa kesi na kuachiwa huru na Mahakama hiyo, Gasaya alichukuliwa na askari polisi na kuwekwa chini ya uangalizi katika Mahakama hiyo.
Awali, kabla ya kufutia kesi hiyo, Wakili Mwanga ameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH) lakini DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo mahakamani hapo.
Wakili Mwanga baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alionekana kutabasamu.
Hata hivyo, mshtakiwa anatetewa na mawakili Nafikile Mwambona akisaidiana na Kung'e Wabeya.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa Mahakamani hapo Desemba 29, 2023 kujibu shtaka linalomkabili.
Kwa kipindi chote hicho mshtakiwa walikuwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo alitakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh 2.6bilioni au mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 2.6bilioni.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai namba 207/2022.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Gasaya alidaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.