Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dosari za kisheria zafuta hukumu miaka 30 jela, kesi kuandikwa upya

Muktasari:

  • Uamuzi huo unatokana  na Mahakama kubaini kulikuwa na kasoro za kisheria katika namna hukumu ilivyotolewa ambapo Mahakama ya Wilaya ilishindwa kubainisha wazi hatia kwa kila shtaka.

Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Simiyu, imebatilisha hukumu ya kifungo cha miaka 30 aliyokuwa amehukumiwa Majingwa Ndushi baada ya kubaini kasoro za kisheria katika namna hukumu ilivyotolewa na mahakama ya chini. Mahakama imefuta hukumu yote na kuamuru kesi irejeshwe Mahakama ya Wilaya ya Meatu kwa ajili ya kutoa hukumu upya kwa mujibu wa sheria.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 17, 2026, na Jaji Hussein Mtembwa, aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyokatwa na Majingwa akipinga hukumu. Jaji alibaini kuwa hukumu ya awali haikuonyesha wazi hatia kwa kila shtaka, kwani haikueleza kama ilihusu shtaka la kwanza, la pili, au yote mawili, jambo linalokinzana na taratibu za kisheria. Aliongeza kuwa Mahakama ilipaswa kumtia hatiani mshtakiwa kwa kila shtaka tofauti na kubainisha adhabu husika.

Awali, Majingwa alishtakiwa Mahakama ya Wilaya ya Meatu kwa makosa mawili ya kumiliki dawa za kulevya aina ya bangi kinyume cha Kifungu cha 16(1) na (2)(c) cha Sheria ya Kudhibiti na Utekelezaji wa Dawa za Kulevya. Agosti 21, 2025, alipatikana na misokoto 38 ya bangi (gramu 110.4) pamoja na majani makavu ya bangi (kilo 2) katika eneo la Mwashilingi Mtoni, wilayani Meatu. Ushahidi ulionyesha kuwa alipatikana na mali hizo na kuongoza polisi hadi mahali alipokuwa amezihifadhi, huku akikanusha mashtaka yote.

Mahakama ya Wilaya ilimtia hatiani Majingwa kwa makosa yote mawili na kumuhukumu kifungo cha miaka 30, ikisema ilikuwa adhabu ya chini kwa kuzingatia kuwa alikuwa mkosaji wa kwanza. Mshtakiwa hakuridhika na hukumu hiyo na akakata rufaa Mahakama Kuu akipinga akiegemea kwenye kasoro za kisheria, ikiwemo kushindwa kuzingatia utetezi wake na tatizo la utaratibu wa kutoa hukumu kwa kila shtaka.

Wakili wa Serikali alikiri kuwepo kwa mapungufu na aliomba kesi irejeshwe mahakama ya mwanzo ili marekebisho yafanyike. Baada ya kupitia hoja zote, Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja hiyo, ikibatilisha hukumu ya awali na kuamuru kesi iandikwe upya kwa kufuata taratibu sahihi za kisheria.