Prime
Dosari kisheria zamtoa jela maisha baba wa kambo

Muktasari:
- Mrufani (mshtakiwa) alidai ugomvi baina yake na shahidi wa kwanza ni yeye kuoa mwanamke aliyekuwa mke wake wa zamani.
Arusha. Dosari za kisheria zimesababisha Hamisi John kuepa adhabu ya kifungo cha maisha jela alichohukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kambo wa miaka saba.
Miongoni mwa dosari hizo ni ukiukwaji wa sheria ya ushahidi uliotolewa na mwathirika wa tukio hilo.
Desemba 23, 2021 Mahakama ya Wilaya Pangani ilimtia hatiani Hamisi kwa kosa la ubakaji kinyume cha kifungu cha 130 (1), (2) (e) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hukumu iliyomwachia huru Hamisi imetolewa Mei 30, 2025 na jopo la majaji Shabani Lila, Panterine Kente na Agnes Mgeyekwa, ambayo pia imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jopo hilo halikuridhishwa na ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili katika kesi ya msingi, pia ushahidi wa mwathirika ulipokewa kinyume cha sheria.
Msingi wa kesi
Kumbukumbu za Mahakama zinaeleza kati ya Septemba na Novemba, 2021 mwathiriwa alikwenda kwa shangazi yake Agness Emily (shahidi wa pili) aliyekuwa akiishi Kijiji cha Mkalamo wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Agness alidai Novemba Mosi, 2021 mwathiriwa alikwenda kumtembelea akamwambia hatarudi nyumbani kwao (alipokuwa akiishi na mrufani) hadi atakaponunuliwa sare mpya za shule.
Alidai hataki kurudi nyumbani kwani baba yake wa kambo alikuwa akimbaka wakati wowote ambao mama yake na ndugu zake hawapo nyumbani.
Shahidi alidai alipomuuliza iwapo alimweleza mama yake taarifa hizo, alijibu alimweleza ila mama yake alipuuzia jambo hilo.
Alidai baba yake wa kambo alipomaliza kumbaka alimweleza atoke nje akacheze na alimtisha kuwa angemchinja endapo angemweleza mtu.
Shahidi alidai alimweleza dada yake kuhusu unyanyasaji na mateso ya binti huyo, kisha wakamjulisha baba yake mzazi (shahidi wa kwanza) aliyekwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Pangani.
Kutokana na taarifa hiyo, mrufani alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi, huku mwathirika akipewa rufaa ya kwenda hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu ambao ulithibitisha alibakwa.
Shahidi wa nne, Dk Yusufu Mrero amliyemchunguza mtoto huyo alithibitisha kuwa alibakwa.
Utetezi wa mshtakiwa
Mrufani (mshtakiwa) alidai hakumbuki tarehe ila Novemba, 2021 alimpelekea mwathirika sare za shule.
Alidai shahidi wa kwanza alimpeleka mtoto hospitali ikaelezwa anasumbuliwa na malaria.
Shahidi alidai siku iliyofuata alisafiri kwenda Dar es Salaam na siku mbili baadaye aliambiwa kuna tatizo kubwa linalohitaji uwepo wake.
Alipochunguza alidai alijulishwa shahidi wa kwanza alimtuhumu kuwa amembaka binti yake wa kambo.
Alidai alirejea mkoani Tanga siku iliyofuata akamuuliza mwathirika wa tukio hilo ambaye alikataa kubakwa na kudai kuwa shangazi yake (shahidi wa pili) na shahidi wa kwanza ndio walimwambia aseme tuhuma hizo za uongo.
Mrufani alidai katika kusuluhisha suala hilo kwa amani, ndipo alipokwenda nyumbani kwa shahidi wa kwanza ambako kulizuka ugomvi kati yao akajeruhiwa.
Baada ya Mahakama kusikiliza pande zote mbili, ilimtia hatiani mrufani (mshtakiwa) kwa kosa la ubakaji na kumhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Kuhusu rufaa
Awali, alikata rufaa Mahakama Kuu ambayo iliitupilia mbali ikieleza kulikuwa na ushahidi wa kutosha uliothibitisha shtaka la kubaka.
Katika rufaa ya pili, aliwasilisha sababu nne akidai kosa halikuthibitishwa kwa viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, umri wa mrufani haukuthibitishwa na ushahidi wake ulipokewa na kukubalika kinyume cha sheria, pia utetezi wake (mrufani) haukuzingatiwa.
Alidai ugomvi baina yake na shahidi wa kwanza ni baada ya yeye (mrufani) kuoa mwanamke aliyekuwa mke wake wa zamani (shahidi wa kwanza).
Mrufani hakuwa na wakili alijiwakilisha mwenyewe, huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Matiku Nyangero aliyeunga mkono hukumu iliyotolewa na mahakama ya mwanzo ya rufaa.
Uamuzi majaji
Majaji katika huku wamezingatia misingi ya kukata rufaa na hoja zinazotolewa na kila upande kwa maandishi na mdomo.
Kuhusu hoja ya shtaka kutothibitishwa bila kuacha shaka, wamesema Mahakama za chini zilipaswa kuzingatia utetezi wa mrufani.
Majaji katika hoja ya ushahidi wa mwathirika kutozingatia sheria, wamesema baada ya kupitia mwenendo wa mashauri wamebaini ushahidi wake aliutoa kinyume cha sheria.
“Kuhusu shahidi wa kwanza na wa pili hatujaridhishwa nao, kwa mfano tumebaki tukijiuliza kwa nini shahidi wa pili aliamua kumweka pembeni mama wa mwathiriwa ambaye ni dada yake na kukimbilia kuripoti kosa kwa shahidi wa kwanza ambao waliripoti haraka polisi bila kutaka kuhakiki walichoambiwa na mwathiriwa au kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa. Hakuna sababu iliyotolewa kwa mashahidi hao wawili kuharakisha kuweka sheria katika hoja dhidi ya mrufani,” wamesema majaji.
Wamesema hali kama hiyo haiwezi kusemwa kwa kiwango chochote cha uhakika kwamba mwathirika hawakumfundisha au kumshawishi kumhusisha mrufani kwa uongo.
“Kutokana na sababu hizo tunaruhusu rufaa hii, kufuta hukumu ya mrufani na kutengua kifungo cha maisha alichopewa. Tunaamuru aachiwe mara moja,” imesema hukumu.