Dk Shoo: Vijana msikubali kurubuniwa kisiasa

Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo
Muktasari:
- Amesema kupatikana kwa viongozi waadilifu, wacha Mungu na wenye upendo na uzalendo kwa Taifa kutaondoa malalamiko ya uwepo wa viongozi wabaya.
Hai. Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo amewataka vijana nchini kuepuka kutumiwa vibaya kisiasa na kurubuniwa, kisha kuwachagua viongozi wasiofaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.
Pia amewataka pia vijana wenye sifa na vipawa vya uongozi, kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali, ili kupata fursa ya kuingia katika vyombo vya maamuzi kuanzia ngazi za mitaa hadi bungeni.
Dk Shoo ametoa rai hiyo leo Jumapili Juni 23, 2024 alipofunga kongamano la vijana na askofu lililofanyika kwa siku tano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Machame ambalo liliwakutanisha vijana 411 kutoka majimbo matano ya Dayosisi ya Kaskazini.
Amesema vijana ni kundi muhimu katika Taifa, hivyo wanatakiwa kutumia vizuri haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuhakikisha wanapatikana viongozi wazuri, wenye hofu ya Mungu na kamwe wasikubali kurubuniwa na wanaotaka madaraka kwa manufaa yao binafsi.
“Mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini mwaka ujao ni uchaguzi mkuu, nilete wito kwenu, kwa kila kijana kushiriki kuchagua viongozi kwa umakini wa hali ya juu, msikubali kurubuniwa ukajikuta umepoteza haki yako ya msingi ya kupiga kura,” amesema Dk Shoo.
Hata hivyo, amesema ili kiongozi bora apatikane, ni wajibu wa kila kijana aliyefikia umri wa kupiga kura aende kujiandikisha na apige kura siku ikifika.
“huu ni wito wangu, wewe kama kijana Mkristo moja ya vitu vya kujua ni kutumia haki yako ya kikatiba inavyopasa, usiseme hayakuhusu maana upende usipende, hatimaye yatakuhusu,” amesema kiongozi huyo wa dini.
Kijana na kazi
Dk Shoo ametumia nafasi hiyo kuwaonya vijana kujiingiza kwenye uraibu wa michezo ya kamari na kubeti na badala yake wafanye kazi zitakazowaingizia kipato.
“Kijana uwe na bidii katika kufanya kazi, utajiri wa kijana utapatikana kwa kufanya kazi, naomba niwaonye, wapo vijana wanapoteza fedha na muda wao kwa kubeti, tambueni huwezi kupata maendeleo wala utajiri kama unaogopa kufanya kazi, eti utajiri utakuja tu hivi kirahisi kwa kubeti au kucheza kamari, mnadanganywa,” amesema.
Amesema anatambua kuwa nchi ina changamoto ya ajira rasmi, hivyo ni vema wakajifunza ufundi wa aina mbalimbali, ikiwa ni sambamba na kujiingiza kwenye kilimo na ufugaji wa kisasa, ili wajiajri.
“Ufundi kila wakati utakuwa na soko, lakini pia jiingizeni kwenye ufugaji wa kisasa na kilimo cha kisasa hata cha mbogamboga, kwani miji yetu inakua kwa kasi na ongezeko la watu linazidi kukua. Mkifanya hivyo mtajijengea uhakika wa ajira na kipato,” amesema.
Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Katibu wa idara ya vijana na wanafunzi, Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Mathayo Mtui amesema vijana wakifanya kazi kwa bidii wataweza kupiga vita adui umaskini na kujikwamua kuchumi.
“Kongamano hili la vijana na askofu limefanyika kwa baraka, vijana wamepata mafunzo ya kuwaimarisha kiroho na kiuchumi, na ninaamini wakizingatia waliyofundishwa na kujituma katika kazi, wataweza kupambana na adui umaskini kikamilifu,” amesema.