Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi atoa maagizo kupunguza tatizo la ajira Tanzania

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi

Muktasari:

  • Wajumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi wameanza ziara katika mikoa mitano ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/25,  kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Manyoni. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amezitaka halmashauri zote nchini kuwatambua vijana wasomi kwenye maeneo yao na kuwashirikisha kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbali na kuwatambua, wawaunganishe kwenye vikundi kutokana na taaluma zao kisha  wawapatie mikopo wanayoitoa ya asilimia 10 kwa ajili  ya wanawake, wenye ulemavu na vijana ili wazitumie kwenye mitaji.

Lengo la mkakati huo ni kupunguza idadi ya vijana wanaohitimu fani mbalimbali vyuoni kubaki mitaani pasi na kupata ajira, licha ya kusomeshwa kupitia mikopo inayotolewa na Serikali.

Dk Nchimbi ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Mei 29, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manyoni Mjini, Mkoa wa Singida, katika siku ya kwanza ya ziara yake kwenye mikoa mitano.

Mtendaji mkuu huyo wa chama tawala ametoa maagizo akiitikia ushauri uliotolewa na mmoja wa wananchi kwenye mkutano huo ambaye amesema ili kumaliza tatizo la ajira, vijana kwenye halmashauri watambuliwe, wapewe mikopo na wasimamiwe kutekeleza miradi kama ya ujenzi kutokana na fani zao.

Dk Nchimbi amesema chama hicho kinapokea ushauri huo ambao ni mzuri unaoweza kupunguza tatizo la vijana wasomi wanapohitimu wanakaa mitaani pasi na kuwa na kazi za kufanya licha ya gharama kubwa kutumika kuwasomesha.

"Nitoe maagizo kwa mamlaka za Serikali za mitaa zote nchini kutambua makundi ya vijana wenye uwezo na wasomi ili kuwaunganisha kwenye vikundi na kuwapatia mikopo  kwa masilahi ya nchi yetu," amesema Dk Nchimbi.

Ametolea mfano, iwapo vijana wasomi wa sekta ya kilimo wa  Manyoni, "kama tungewatambua,

wangetumika vizuri Manyoni si ajabu tungeweza kupata uzalishaji mkubwa wa alizeti."

Dk Nchimbi amesema mikopo hiyo ambayo sasa itaanza kutolewa Julai Mosi, 2024, iangalie eneo hilo kwa kila halmashauri nchini.


Kero ya umeme, maji

Katika mkutano huo, wananchi wameibua kero ya umeme kukatika mara kwa mara ambapo hata wakati wa mkutano huo ulikatika pia,  pamoja na upatikanaji wa maji na kumwomba alifanyie kazi.

Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Singida, Martha Malata amesema pamoja na mambo mengine yaliyofanyika lakini suala la umeme wa uhakika unahitajika.

Amesema kukosekana kwa umeme wa uhakika na eneo la Manyoni linakuwa kutokana na shughuli za kiuchumi, linaathiri upatikanaji wa maji.

"Tunataka umeme saa 24, umeme wa mgao unaathiri sana upatikanaji wa maji. Nikuombe Katibu Mkuu ulitolee maelekezo suala hili ili tupate umeme wa uhakika kwa kuwa na 'sub station' yetu," amesema Malata.

Mkazi wa Manyoni, Thomas Chacha akitoa kero yake amesema kuna tatizo la maji, "lakini leo nimeshangaa sana kuanzia asubuhi hadi sasa (saa 9 mchana) maji yametoka, sasa haya maji yametoka wapi? Waulize viongozi haya maji  yametoka wapi au kwa sababu umekuja?"

Pia, suala hilo la umeme, limezungumzwa na Mbunge wa Shingida Mashariki, Miraj Mtaturu akimwambia Katibu mkuu huyo kuwa kuna  wananchi wa jimbo lake hawajaunganishiwa umeme.

Akijibu kero hizo, Dk Nchimbi amesema atamtafuta Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kujua miradi inayotekelezwa imekwama wapi.

"Nawahakikishia nimelichukua hili, namtafuta Waziri na kumtaka kasi iongezeke. Nimeulizwa haya maji yametoka wapi? Yametoka kwa sababu mgeni amekuja," amesema Dk Nchimbi huku wananchi wakishangilia.

Kuhusu umeme, Dk Nchimbi amesema, "nimeongea na Waziri wa Nishati (Dk Doto Biteko). Nimemweleza wanahitaji sub station na yeye amenihakikishia linafanyiwa kazi na umeme utakuwa mzuri bila usumbufu."

"Nitambana Dk Biteko, nitataka kupata taarifa za kila mara utekelezaji umefikia wapi. Yaani nitampigia simu mara kwa mara hadi umeme upatikane," amesema.


Tukemee kugawanywa

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amewasihi wananchi kukemea watu wanaoeneza migawanyo ya kikabila na ukanda.

"Safari moja huanzisha nyingine, leo watatugawa kwa ukabila, U-bara na U-Zanzibar, tukimaliza, safari moja huanza nyingine, Manyara watawakataa Singida. Kisha Mwanza watawakataa Shinyanga, itakuja Mbeya wagawanywe na Songwe."

"Tukemee sana kugawanywa, tudumishe umoja wetu, mshikamano wetu na wote wanaotaka kutugawa, tuwaonyeshe kwa vitendo kuchukizwa na kauli zao hizo," amesema Dk Nchimbi pasi na kufafanua zaidi kina nani wanatoa lugha za kuwagawa Watanzania.



Alichokisema Makalla

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla amesema hii ni awamu ya pili ya ziara ya Dk Nchimbi  katika mikoa mitano ikitanguliwa na waliyoifanya kwenye mikoa sita ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Baada ya kutoka Singida ataendelea na ziara hiyo mkoani Manyara, Arusha, Kilimanjaro na kumalizia Tanga.

"Tunawaambia ndugu zetu, tutaizunguka nchi nzima. Wajiandae vizuri katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, tutashinda kwa kishindo na mwakani tutashinda kwa kishindo pia," amesema.

Makalla amesema huu ni wakati wa wanachama kuendelea kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Mwenezi huyo amesema katika awamu ya sita ndio pekee ambayo imepeleka fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo. Sasa kwa maendeleo haya atakuja mtu hapa atasema hakuna kilichofanyika, hebu muulizeni hizi barabara, huduma za afya, maji au umeme amefanya nani?"


Halima: Mambo mengi yamefanyika

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Singida (RC), Halima Dendego akitoa taarifa ya mkoa amesema shughuli mbalimbali zinaendelea licha ya uwepo wa changamoto ndogondogo ambazo yeye pamoja na watendaji wengine serikalini wanazitafutia ufumbuzi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia mkoa huo umepokea Sh1.7 trilioni za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Halima amesema mipango hiyo wanaifanya kwa kufuata takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambayo mkoa huo una zaidi ya wananchi milioni mbili, "hii inatusaidia sana kujua mahitaji ya wananchi na sisi tunaitumia vyema."

Mkuu huyo wa mkoa amesema shughuli za afya, elimu, maji, kilimo ikiwemo upatikanaji wa mbolea yenye ruzuku, mitandao ya simu, barabara, kutangaza vivutio vilivyopo Singida zinaendelea kufanyika.

"Katibu Mkuu changamoto zipo na tumekueleza. Ukifika kwa mwenyekiti wetu mpelekee salamu zetu na mweleze sisi huku chini tunaendelea kuchapa kazi na malengo yote tunataka kumaliza kabla ya Juni 2025," amesema Halima.

Halima ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari wa Kudumu la Wapiga Kura, kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kuchagua na kugombea nafasi mbalimbali.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Rehema Sombi amesema kipindi hiki Jumuiya ya vijana imepata mafanikio, "Wewe katibu mkuu unatokana na jumuiya hii uliyoihudumu kwa awamu mbili (nafasi ya uenyekiti)."

Rehema amesema vijana wako tayari kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.