Dk Mpango amtabiria mtoto kukalia kiti cha Makamu wa Rais

Muktasari:
- Mtoto huyo ni wa kwanza kuzaliwa tangu kuanza huduma za afya katika kituo cha Kitumbeine na dakika chache tangu kuzinduliwa na makamu wa Rais Dk Philip Mpango
Longido. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amemtabiria mtoto wa kwanza kuzaliwa katika kituo cha afya Ketumbeine kuja kuwa Makamu wa Rais miaka ijayo.
Dk Mpango ametoa utabiri huo leo Februari 10, 2024 kwa mtoto aliyezaliwa na kupewa jina la Philipo baada ya msichana, Nengai Nairowa (17) kutembelewa na makamu huyo wa Rais katika wodi ya wajawazito wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya Kitumbaine kilichoko wilaya ya Longido mkoani Arusha.
“Mtoto huyu ni bahati yangu na amepewa jina langu kwa sababu amezaliwa baada tu ya kumtembelea wodini na sasa Mtanzania huyu mpya aliyekuja na kilo 2.8 atakuja kuwa Makamu wa Rais wa nchi hii, yaani mrithi wangu nimempata mapema,” amesema Dk Mpango.
“Na nitaenda kumtembelea kumsalimia ili kumjua mrithi wangu baada ya hotuba hapa,” amesema.
Mpango ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa za kuzaliwa mtoto huyo, akiwa jukwaani akihutubia wananchi wa Longido baada ya uzinduzi wa kituo hicho cha afya Kitumbaine.
Katika hatua nyingine, Dk Mpango amewapongeza wananchi wa Longido kwa kutoa mifugo yao kuchangia zaidi ya Sh300 milioni katika kituo hicho kilichogharimu zaidi ya Sh1.32 bilioni, huku Serikali kuu ikitoka Sh800 milioni na Shirika la World Vision wakichangia Sh215 milioni.
“Nimeona kituo kimeanza kazi lakini hakuna chumba cha kuhifadhi maiti wala gari la wagonjwa, nikuagize Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel uhakikishe kinajengwa haraka maana tunaishi na tunakufa,” amesema.
Amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya Sh150 milioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba ambapo amemuagiza Naibu Waziri na Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi anayeshughulikia afya, kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa vema kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.
Pia, amewataka viongozi na wananchi wote kuchukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na magonjwa ya tumbo.
Awali, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Arusha imetengewa zaidi ya Sh40 bilioni kwenye sekta ya afya.
Akizungumzia kituo hicho, diwani wa viti maalumu kata ya Kitumbaine, Elizabeth Timothy amesema ujenzi wa kituo hicho kilichoanza kufanya kazi mwaka huu utaokoa maisha ya watu wengi waliokuwa wanatembea zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma za afya wilaya ya Monduli au Longido mjini.
“Wanawake kwenye kujifungua ndio ilikuwa changamoto kubwa na tulifikisha kilio chetu kwa Rais na leo ametekeleza, kiukweli ameokoa maisha ya wengi,” amesema.
Awali, Dk Mpango alizindua mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu iliyohitimisha upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote 49 vya wilaya ya Longido.
Akizungumzia mradi huo, Dk Mpango amesema kuwa umeme ni nyenzo muhimu kwa uchumi, hivyo amewataka wataalamu kuhakikisha unawaka muda wote ili ulete tija kwa wahusika.
“Umeme ni uchumi hivyo niwatake na wananchi wa Longido ukawe na manufaa kwenu, kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi,” amesema.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Hassan Saidy amesema jumla ya Sh15 bilioni zimefanikisha kusambaza umeme wilaya nzima ya Longido katika vijiji 29.
“Katika awamu hii ya tatu ya kukamilisha vijiji vyote 49, tumekamilisha ambapo wa Kitumbaine umegharimu jumla ya Sh1.7 bilioni.
Amesema nchi ina vijiji 12,318 ambapo vijiji 11,720 sawa na asilimia 95 vimeshapata umeme huku vijiji 598 vilivyobaki wakandarasi wako hatua mbalimbali za kukamilisha, ambapo hadi Juni vijiji vyote nchini vitakuwa na umeme.