Dk Mpango aagiza mishahara mipya ianze Januari mwakani

Muktasari:

Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango amewataka waajiri wa sekta binafsi kuanza kulipa mishahara mipya kama ilivyoagizwa na Serikali kuanzia Januari mwakani.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango amewataka waajiri wa sekta binafsi kuanza kulipa mishahara mipya kama ilivyoagizwa na Serikali kuanzia Januari mwakani.

Kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 697 la Novemba 25, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza kima cha chini cha mishahara katika maeneo tofauti ya uzalishaji ya sekta binafsi ambayo Dk Mpango ametia msisitizo utekelezaji wake.

Dk Mpango alitoa agizo hilo kwenye sherehe za utoaji tuzo ya mwajiri bora wa mwaka 2022 zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika juzi usiku jijini hapa.

“Nataka waajiri kufuata sheria zilizopo kuhusu ajira kwa wageni, wengine wanaajiri wageni ambao utaalamu wao unapatikana nchini, hizo ni nafasi za wazawa. Nakuagiza waziri wa nchi na timu yako mfuatilie na kuchukua hatua kisheria,” alisema Dk Mpango.

Vilevile, aliwataka waajiri kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kufuata na kuzingatia miongozo iliyowekwa na kutolewa na Serikali, likiwamo agizo la kima cha chini cha mishahara.

“Pia angalieni namna mtakavyoboresha maslahi ya wafanyakazi, nawaomba angalieni njia mbalimbali kwa kuwapa motisha na posho ili waweze kujikimu kimaisha. Wanaofanya vizuri wapewe tuzo na motisha, wapandisheni vyeo na walipeni stahiki zao,” alisema.

Dk Mpango pia alizungumzia suala la mikataba ya kazi, akiwataka waajiri kuzingatia sheria kwa kuitoa, si kuwafanyisha kazi kama vibarua ilhali wangeweza kupata ajira kwa kuwa huo ni wajibu na haki ya mwajiri na mwajiriwa.

Pia aliwaagiza waajiri kuhakikisha wanawajengea uwezo wafanyakazi na kuwapa vitendea kazi na kuwaruhusu kujinoa kitaaluma ili wafanye kazi kwa ufanisi unaotegemewa na kuhitajika kazini.

Katika hatua nyingine, Dk Mpango alikemea tabia ya baadhi ya waajiri kuwaonea wafanyakazi, kutumia vibaya madaraka yao, udhalilishaji na ngono za lazima kwamba ni mambo yanayoathiri utendaji kazi.

“Hatutaki malalamiko ya wafanyakazi yafike juu kabisa, tungependa waajiri mtoe haki na stahiki za wafanyakazi wenu kwa mujibu wa taratibu za kazi, ofisi yangu inasikiliza kesi nyingi sana. Haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki ilionyimwa, tutende haki kwa kufuata sheria za kazi. Uonevu, matumizi mabaya ya madaraka, wafanyakazi kudhalilishwa inaathiri utendaji kazi, lazima tuhakikishe vitendo hivi vinakoma sababu vinapoteza utu. Juzi nimepokea kesi mbili ofisini kwangu za aina hii, bado kuna uonevu, ngono za lazima na upendeleo, haya mambo tusiyafumbie macho,” alisema Makamu wa Rais.

Akitoa salamu zake, Profesa Ndalichako alisema waajiri wanapaswa kutambua wafanyakazi ndiyo nguzo muhimu ya ufanisi wa shughuli wanazozifanya, hivyo hawana budi kuwathamini na kutambua mchango wa kazi zao.

“Niwatangazie sekta binafsi, Serikali imekamilisha upandishaji wa kima cha chini cha mishahara, ninaagiza suala hili litekelezwe bila changamoto ya aina yoyote ifikapo Januari mosi 2023. Upangaji wa kima cha chini umefanyika baada ya bodi yetu kufanya utafiti kuangalia hali ya biashara na gharama za maisha. Ilikuwa ni shirikishi na ATE na mashirikisho yote ya vyama vya wafanyakazi yameshiriki,” alisema.

Profesa Ndalichako alisisitiza kuwa mara ya mwisho mshahara wa kima cha chini ulipandishwa mwaka 2013, yaani miaka tisa iliyopita.

“Nawasihi tutekeleze bila kuwa na changamoto yoyote. Sitarajii nishushiwe barua na Makamu wa Rais kwamba kuna kampuni hazitaki kutekeleza amri hiyo. Naomba kila mmoja atekeleze wajibu wake,” alisema Profesa Ndalichako.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisisitiza kuwa kampuni nyingi za kigeni hugawa fursa kwa wazawa kwa asilimia kubwa, huku akisisitiza utekelezaji wa agizo la kulipa kima cha chini cha mishahara kilichotangazwa.

“Sisi Tucta tulishirikishwa kuhusu mishahara mipya, wafanyakazi tumeridhika kwa kuwa tulishiriki katika upangaji huo ninaamini waajiri mtakwenda kuanza kulipa mishahara mipya kuanzia Januari mosi,” alisema Nyamhokya.