Diaspora wafungua kesi ya uraia pacha nchini

Muktasari:
Kesi hiyo ya Kikatiba namba 18 ya mwaka 2022 imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu na Shaban Fundi, Patrick Nyelesa Nhigula, Restuta Kalemera, Nkole Muya, Emmanuel Emmanuel na Bashir Kassam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Dar es Salaam. Suala la kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja maarufu kama ‘uraia pacha’ nchini sasa limechukua sura mpya baada ya Watanzania sita wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi kufungua kesi ya kikatiba kupinga sheria inayozuia uraia pacha.
Kesi hiyo ya Kikatiba namba 18 ya mwaka 2022 imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu na Shaban Fundi, Patrick Nyelesa Nhigula, Restuta Kalemera, Nkole Muya, Emmanuel Emmanuel na Bashir Kassam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kwa mujibu wa viapo vyao, hawa ni Watanzania kwa kuzaliwa walioondoka nchini na kwenda ughaibuni kwa nyakati tofauti tofauti hususani katika nchi za Marekani, Uingereza na Canada wanakoishi na kufanya kazi ambako pia walishapata uraia.
Wakili wa wadai hao, Peter Kibatala jana alisema kuwa kesi hiyo tayari imepangiwa jopo la majaji watatu watakaoisikiliza wakiongozwa na Jaji Mustafa Ismail akishirikiana na Jaji Hamidu Mwanga na Jaji Obadia Bwegoge, imepangwa kuanza kutajwa Februari 20, 2023
Katika kesi hiyo wanaiomba mahakama itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Uraia vinavyozuia uraia pacha ni batili wakidai kuwa vinakiuka haki zao za Kikatiba kwa kuwa vinawanyanya haki ya asili isiyonyang’anyika yaani uraia wa kuzaliwa.
Vifungu hivyo wanavyopinga ni pamoja na kifungu cha 7(1) na (2) (c), (4)(a) (6) vya Sheria ya Uraia ambavyo wanadai kuwa vinakiuka haki zao nyingine za Kikatiba.
Katika viapo vyao wanaeleza kuwa wameathirika sana kitendo cha kunyimwa haki mbalimbali katika nchi yao waliyozaliwa kwa kuzingatia kwamba walipata uraia wa nchi hizo kwa sababu za kiuchumi na ustawi wa kijamii.
Wanadai kuwa wao ni Watanzania kwa damu na kwamba wanatamani kuendelea kuwa Watanzania, lakini kwa vifungu hivyo vya Sheria ya Uraia wananyimwa haki hiyo.
Wanadai kuwa wenzao wanaotoka katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kama vile Kenya, Rwanda na Uganda, wanaoishi nje ya nchi wanaruhusiwa kuwa hati za kusafiria za Afrika Mashariki kwa kuwa nchi zao zinaruhusu uraia pacha lakini wao hawawezi kupata hati hizo.
Miongoni mwa haki wanazozikosa nchini walikozaliwa ni pamoja na kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi na kwamba wanapotembelea nchini wanaishia kuishi katika nyumba za ndugu zao au hotelini.
Wanataja haki nyingine wanazozikosa kuwa ni pamoja na kutokuchagua viongozi wala kushiriki kugombea nafasi ya umma katika uchaguzi nchini.
Akizungumzia msingi wa kufungua kesi hiyo, Wakili Kibatala alisema kuwa hoja ya hoja zinazotolewa kupinga uraia pacha ni madai kuwa ni hatari kwa usalama wa Taifa.
Hata hivyo, alisema kuwa hoja hizo ni hoja mgando ambazo hazina mashiko huku akitolea mfano wa mtoto wa Rais wa Liberia ambaye anachezea Timu ya Taifa ya Marekani kwa kuwa ana uraia wa nchi mbili na hakuna tatizo.
Alisema kuwa kama kesi hiyo itafika hatua ya kusikilizwa hoja za msingi baada ya kuvuka hatua ya mapingamizi ya Serikali kama yataibuliwa, anaamini kuwa wana hoja za kuishawishi mahakama.