Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dereva wa bajaji, kondakta wake wauawa wakituhumiwa kumuibia abiria wao

Baadhi ya madereva bajaji wakiendelea na zoezi la ukaguzi wa bajaji zinazokiuka utaratibu na kuwa na kondakta katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Amina Mbwambo

Muktasari:

  • Watu hao ambao ni dereva wa bajaji na kondakta wake, wameuawa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kufanya jaribio la kumuibia mteja wao katika eneo la Viwandani, Kata ya Nyihogo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kahama. Watu wawili akiwemo dereva wa bajaji Rajabu Hussein (mwenye umri kati ya miaka 27 na 30), pamoja na mtu mwingine anayedaiwa kuwa kondakta wake ambaye bado hajafahamika, wanadaiwa kuuawa na wananchi wenye hasira usiku wa kuamkia Machi 30, 2025, katika mtaa wa Nyihogo, Kata ya Nyihogo, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga huku Jeshi la Polisi likikemea tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Tukio hili linadaiwa kutokea baada ya watu hao wawili kushukiwa kuhusika katika tukio la ujambazi au unyanyasaji, ambalo lilikusanya hasira za wananchi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyihogo, Idi Mitimingi, amesema alipigiwa simu na wananchi wake akiwa msikitini na alipoenda eneo la tukio, alikuta tayari polisi walikuwa wamefika na kuondoka na watuhumiwa.

Akiwa katika mahojiano na waandishi wa habari, Mitimingi amesema kuwa maelezo aliyopewa na wananchi ni kwamba, dereva na kondakta wa bajaji walijaribu kumkaba abiria wao, ambaye alilipiga kelele, na hivyo kusababisha wananchi kuungana na kufika eneo hilo.

Mitimingi amesema kuwa changamoto kubwa ni kuwa baadhi ya bajaji sasa zimekuwa na kondakta na wengi wao si waaminifu, jambo ambalo linaongeza hatari ya uhalifu.

"Madereva wa bajaji wanapaswa kuzingatia na kuchunguza watu wanaowapa bajaji kuendesha, hasa nyakati za usiku, maana inaonekana baadhi yao wanahusika na vitendo vya uhalifu. Sasa nashangaa bajaji zenye kondakta, huyu kondakta anafanya kazi gani hasa kwenye bajaji? Hii ni changamoto kubwa kwa usalama wa wananchi," alisisitiza Mitimingi.

Mwenyekiti huyo aliitaka jamii kuwa makini na hali hii, akisisitiza kuwa ni muhimu kuwa na ushirikiano wa karibu kati ya madereva, wananchi na vyombo vya usalama ili kupambana na vitendo vya uhalifu vinavyoathiri maeneo yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bajaji Mkoa wa Shinyanga (Chamwapita), Idsam Mapande amekiri kulifahamu tukio la kuuawa kwa watu wawili katika Mtaa wa Nyihogo na kusema kwamba chama hicho kimeshaweka marufuku bajaji kuwa na kondakta, ili kupunguza vitendo vya uhalifu vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya waendesha bajaji wanaokuwa wawili kwenye bajaji moja.

Mapande amesema chama hicho kimeanzisha msako wa kukagua madereva wanaokuwa wawili kwenye bajaji na kwamba madereva wanaobainika wanachukuliwa hatua za kisheria kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, hasa Kitengo cha Usalama Barabarani.

"Kwa sasa, tumepiga marufuku bajaji kuwa na kondakta, na tunahakikisha tunatekeleza hili kwa kuwaonya madereva. Hatufanyi biashara na watu wanaovunja sheria, na tumekuwa tukishirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wote wanaovunja sheria," amesema Mapande.

Aidha, Mapande alikemea kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi na madereva kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanaposhuhudia vitendo vya uhalifu.

Amesema kuwa chama hicho kinaendelea kutoa elimu kwa madereva ili waweze kuepuka kuwa na kondakta au wapiga debe katika bajaji zao, kwani mara nyingi wao hutumika kufanya uhalifu kwa abiria.

"Tumekuwa na utaratibu wa kutoa elimu endelevu kwa madereva wetu kwa kushirikiana na shule za mafunzo ya udereva na Jeshi la Polisi. Hatuwezi kuruhusu bajaji kuwa na kondakta, hiyo ni kinyume na utaratibu wetu," amesisitiza Mapande.

Pia, aliongeza kwamba kundi la waendesha bajaji linaendelea kukua na kuwa muhimu kwa vijana, kwani linatoa ajira kwa watu wengi, hususan wale waliokosa ajira rasmi.

"Sasa tumekuwa na utaratibu wa kutambuana na kuhakikisha madereva wanajulikana kwa majina na utambulisho wao," alisema.

Dereva bajaji kutoka Manispaa ya Kahama, Juma Yassin, amesema kuwa biashara ya bajaji ni kazi kama kazi nyingine yoyote, lakini alikiri kwamba baadhi ya madereva wamekuwa wakiharibu sifa nzuri ya kazi hiyo kwa kutokuwa waaminifu.

Yassin amewataka wanawake katika Manispaa ya Kahama ambao wamekuwa wakiathirika na vitendo vya udhalilishaji na uhalifu wa kijinsia, kutoa taarifa kwa polisi au uongozi wa bajaji ili hatua zichukuliwe dhidi ya madereva hao.

"Nawaomba wanawake ambao wamekumbana na hali ya udhalilishaji au wameshikiliwa maungo yao wanapokuwa kwenye bajaji, kutoa taarifa kwa polisi au kwa uongozi wa bajaji. Hii itatusaidia kuchukua hatua na kulinda usalama wa kila mmoja," alisisitiza Yassin.

Dereva mwingine, Kennedy Samweli, ametoa wito kwa madereva wenzake kuwa waangalifu na kuithamini kazi ya bajaji.

Samweli amekumbusha kwamba kazi hiyo imetoa ajira kwa vijana wengi na kuwa ni muhimu kuacha tabia ya kuendesha bajaji wawili wawili, hasa nyakati za usiku.

"Tunapaswa kuepuka kutembea madereva wawili kwenye bajaji, hasa usiku, kwa sababu hii inachochea hofu miongoni mwa abiria. Wakati mwingine, abiria wanapowaona madereva wawili na kuona hali hiyo kama ni ya hatari, wanaweza kuamua kuchukua hatua ambazo si sahihi," alisema Samweli.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema kuwa analifuatilia na kwamba atatoa taarifa zaidi baadaye. Hata hivyo, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa wakati taarifa hii inatolewa.