Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DCEA yateketeza kilo 614 za dawa za kulevya

Muktasari:

  • Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza kilo 614 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine na heroini.

Dar es Salaam. “Hakuna atakayebaki salama katika biashara ya dawa za kulevya na tunaendelea kuhakikisha Tanzania haiwi tena lango la kupitishia dawa hizi.”

Ni kauli ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo aliyoitoa leo Desemba 18, 2024 wakati wa uteketezaji wa kilo 614.12 za dawa za kulevya, ambazo zilikuwa zinashikiliwa kama vielelezo na kuamiriwa ziteketezwe na mahakama.

Hiki ni kiwango kikubwa zaidi cha dawa za kulevya kilichoteketezwa ndani ya mwaka 2024 jijini Dar es Salaam.

Dawa hizo, kilo 601.87 ni methamphetamine na heroini huku kilo 12.25 zikiwa vielelezo vilivyokamatwa kutokana na kesi tatu za makosa ya dawa za kulevya, zilizokuwa zikiendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani (Kibaha) na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kwa mujibu wa Lyimo, dawa hizo zinateketezwa wakati kesi zikiwa bado zinaendelea mahakamani kutokana na uwezekano wa kuharibika na kubadilika umbo lake.

“Uteketezaji wa dawa za kulevya hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kanuni zake. Sheria hii inaelekeza kwamba, uteketezaji wa dawa za kulevya unaweza kufanywa kabla shauri halijaanza kusikilizwa, wakati linaendelea kusikilizwa au baada ya shauri husika kumalizika mahakamani.

“Uteketezaji hufanyika kwa namna ambayo hulinda afya na kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira. Zoezi hili hushuhudiwa na wadau mbalimbali walioainishwa kisheria,” amesema.


Pamoja na uteketezaji uliofanyika, mamlaka hiyo mwezi huu (Desemba 20240 imeteketeza ekari 12 za mashamba ya bangi katika Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, kilo 398.105 za aina mbalimbali za dawa za kulevya mkoani Mtwara na inatarajia kuteketeza kilo 126.21 za mirungi mkoani Arusha.

Lyimo amesema kutokana na kuboreshwa mifumo ya udhibiti na ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na vyombo vingine, hakuna namna wafanyabiashara wa dawa za kulevya watakwepa mkono wa dola.

Amesema nguvu kubwa kwa sasa imewekwa kwa wafanyabiashara wakubwa na wasafirishaji wa dawa hizo ili kuzuia Tanzania kuwa lango la kupitishia dawa za kulevya.

“Tumewakamata wengi na wengine taarifa zao tunazo tunaendelea kuwafuatilia, niwaambie tu wale wanaofikiri wanaweza kufanya biashara hii ndani ya Tanzania na wakabaki salama siku zao zinahesabika.

“Tumeongeza juhudi na mbinu mbalimbali katika ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya, hivyo hakuna atakayesalimika, lengo ni kuhakikisha tunalinda afya za Watanzania na tunakuwa na nguvu kazi ya uhakika isiyoathiriwa na dawa hizi haramu,” amesema.

Lymo amesema tathmini inaonyesha kadri Serikali inavyoongeza juhudi kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya, ndivyo mafanikio hutokea.

Amesema: “Hili tunalipima, hata takwimu mwaka 2023 tulikamata kilo milioni 1.9 za dawa za kulevya, mwaka huu tumeshakamata zaidi ya kilo milioni mbili na operesheni zinaendelea, kuna watu tunawafuatilia na tuna uhakika tutawakamata kabla mwezi huu kuisha.”