DC Moshi atangaza kiama watakaoshindwa kupeleka watoto sekondari

Mkuu wa wilaya ya Moshi (DC), Abas Kayanda akikata utepe ikiwa ni ishara ya kupokea vyumba 82 vya madarasa vilivyojengwa shule mbalimbali Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Picha na Fina Lyimo
Muktasari:
Mkuu wa Wilaya ya Moshi (DC), Abas Kayanda amesema atawachukulia hatua kali wazazi ambao watashindwa kuwapeleka wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2022.
Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Moshi (DC), Abas Kayanda amesema atawachukulia hatua kali wazazi ambao watashindwa kuwapeleka wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2022.
Akizungumza leo Desemba 29, 2021 wakati akikabidhiwa madarasa 82 ya Halmashauri ya Moshi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro yaliyojengwa kutokana na fedha za Uviko 19 zilizotolewa na Serikali.
Amesema mzazi yoyote atakayeshindwa kumpeleka mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza atachukuliwa hatua za kisheria.
"Madarasa tayari yamekamilika kwa ajili ya kupokea wanafunzi ambao wamechaguliwa kwa kuanza kidato cha kwanza bila msongamano hivyo, watoto wote waliochaguliwa wapelekwe shule bila kikwazo." Amesema Kayanda
Amesema zipo taarifa kuwa Halmashauri ya Moshi kitaaluma hawafanyi vizuri, na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hio na wadau wa elimu kujadili changamoto zilizopo ili kuweze kuzimaliza.
Amesema Halmashauri ya Moshi yenye majimbo mawili ya uchaguzi ilipokea Sh1.7 bilioni kwa ajili ya kujenga vyumba 82, pamoja na madawati 1400 na kwamba ujenzi umekamilika kwa wakati
Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dk Charles Kimei amesema fedha hizo zimeleta mabadiliko makubwa kwa muda mfupi hivyo wananchi waunge jitihada za miradi hiyo pamoja na inayoanzishwa na Serikali.
"Serikali imekuwa ikianzisha miradi ambayo imekuwa ikigusa wananchi wa hali ya chini ikiwamo maji, barabara na afya hiyo wananchi hawana budi kuunga mkono na kuachana na propaganda zinzotolewa na baadhi wanasiasa wasio iwazia mema nchi dhidi ya miradi hiyo" amesema Dk Kimei.