Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

COP28 yaonyesha mwelekeo wa dunia mabadiliko ya tabianchi

Rais wa COP28, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Abu Dhabi, Sultan Ahmed al-Jaber akiwa katika moja ya mijadala. Picha File

Dar es Salaam. Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC-COP28) uliokuwa ukifanyika Dubai – Umoja wa falme za kiarabu (UAE) umemalizika.

Mkutano huo umemalizika ukitoa makubaliano mengi likiwamo lile lenye ishara ya ‘mwanzo wa mwisho wa enzi za matumizi ya nishati kisukuku’ (nishati chafu – makaa ya mawe, mafuta na gesi) kwa kuweka msingi wa namna ya kuacha matumizi hayo kwa kuzingatia haki na usawa.

Akizungumza wakati wa ufungaji wa mkutano huo jana, Rais wa COP28, Dk Sultan Al Jaber alisema makubaliano hayo yanaunga mkono juhudi za dunia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na malengo ya kuweka juhudi za haraka kudhibiti ongezeko la joto kufikia nyuzi joto 1.5°C mwaka 2030.

Tafiti zinasema matumizi ya nishati chafu yamechangia ongezeko la joto kwa zaidi ya asilimia 80 jambo linalosababisha mabadiliko ya tabianchi duniani.

"Ulimwengu ulihitaji kutafuta njia mpya, tumeipata njia hiyo,” alisema Rais wa COP28, Dk Al Jaber ambaye pia alikuwa mjumbe maalumu wa UAE kwenye mkutano huo.

"Tumejitahidi kuandaa maisha bora kwetu na vizazi vijavyo pamoja na dunia yetu. Tunapaswa kujivunia mafanikio yetu ya kihistoria."

Dk Al Jaber alisema wamefanikiwa kuweka maazimio kwenye kilimo, chakula, afya na matumizi ya nishati lakini kubwa ni kuja na Rasimu ya Kwanza ya Maandishi (GST) inayotoa malengo na mwelekeo wa dunia kwenye kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNCC), Simon Stiell alisema, “sasa nchi na biashara zote zinahitaji kugeuza ahadi hizi kuwa matokeo ya uchumi halisi, bila kuchelewa."

GST inachukuliwa kama matokeo makubwa zaidi ya COP28 kwa kuwa ina vipengele vilivyojadiliwa na vinavyotoa miongozo kwa nchi kuandaa mipango thabiti ya utekelezaji wa kukabili mabadiliko ya tabianchi hadi mwaka 2025.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na UNFCCC, GST imeamuliwa kwa kutambua sayansi inayoonyesha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani unaohitaji kupunguzwa kwa asilimi 43 ifikapo 2030, ikilinganishwa na viwango vya 2019, ili kudhibiti joto hadi 1.5°C, lakini imeonyesha nchi bado hazijafikia lengo hilo.

Nchi zimetakiwa kuwasilisha mipango yao ya hiari ya kupunguza Matumizi ya Nishati Chafu (NDC) huku Stiell wa UNCC akikumbusha wanatakiwa kufanya hivyo mapema mwaka 2024.

Mambo mengine yaliyokubaliwa ni mfuko wa madhara na hasara ambao kwa mara ya kwanza ulipata Dola 800 milioni za Marekani (Sh2 trilioni) zilizoahidiwa.

Nchi pia zilikubaliana juu ya Lengo la Kimataifa la Kukabiliana Mabadiliko ya Tabianchi (GGA), la namna ulimwengu unavyotakiwa kufanya kustahimili athari.


Habari hii imewezeshwa na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.