Chongolo awahakikishia Morogoro ujenzi wa barabara

Muktasari:

  • CCM imewaambia wananchi wa Morogoro vijijini kwamba ujenzi wa barabara hiyo hadi Bwawa la Julius Nyerere umeshaanza, kikisema hakutakuwa na maneno bali ni utekelezaji.

Morogoro. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewaambia wananchi wa Morogoro Vijijini kwamba hakutakuwa na maneno mengi kuhusu ujenzi wa barabara urefu wa kilomita 78 inayotoka mjini hadi Bwawa la Julius Nyerere, bali ni utekelezaji tu.

Chongolo ameeleza hayo leo Ijumaa  Februari 3, 2023 akizungumza na wananchi wa Kiroka katika halmashauri ya Morogoro Vijijini mkoani hapa, katika mwendelezo wa ziara ya siku tisa ya kikagua uhai wa chama na kusikiliza kero za wananchi na kuoa majibu.

"Nimezungumza na Rais Samia Suluhu Hassan amesema niwaambie kwamba maneno maneno hakuna, sasa ni hivi kazi ya utekelezaji.

“Akaniambia ameshamwagiza Waziri (Profesa Makame Mbarawa) amwagize meneja wa Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) azunguke na mimi ili kutoa majibu,” amesema.

Kabla ya kueleza kwa kina kuhusu barabara hiyo, Chongolo alimwita Meneja wa Tanroads, mkoa wa Morogoro, Alinanuswe Kyamba kueleza mwenendo wa ujenzi wa barabara hiyo.

Kyamba amesema barabara hiyo inayoanzia mjini kupita Kiroka, Kisaki hadi Bwawa la Julius Nyerere imeshafanyiwa usanifu wa kina na kutangazwa zabuni kwa kipande cha kutoka Bigwa hadi Mvua.

"Zabuni ya barabara hii itatangazwa Machi mwaka huu, tunatarajia ikifika Juni mwaka huu mkandarasi atapatikana na kuanza kazi," amesema Kyamba.

Baada ya maelezo hayo, Chongolo aliwambia wananchi kwamba kazi kubwa inakua katika kutangaza zabuni sasa shughuli hiyo imeshafika na fedha zipo za ujenzi wa barabara hiyo.

"Barabara hii ikikamilika Tanroads wekeni taa hasa maeneo ya vijijini.Sio mnapitisha barabara nzuri lakinj hakuna taa, wekani taa hata kipande cha mita au kilomita moja mbili," amesema Chongolo.

Kuhusu changamoto ya umeme, Chongolo amesema vijiji vya halmashauri ya Morogoro Vijjini vimeshawekwa nishati, kinachofuata ni kuhamia katika vitongoji, huku akiwataka kuwa watulivu, akisema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wamejipanga katika kufanikisha hilo.

Mbunge wa Morogoro Vijijini Hamis Taletale ' Babu Tale' amesema suala barabara hiyo ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili jimbo, hata hivyo ameishukuru Serikali kwa kuanza mchakato wa ujenzi huo.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema, amewataka wanachama wa chama hicho mkoa wa Morogoro kuendelea kueleza mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Rais Samia.