Chongolo aonya viongozi waleta migogoro Malinyi

Muktasari:

  • Chongolo amewaambia wenyeviti wa vijiji wa wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wenye tabia ya kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kuruhusu mifugo kuingia mashambani wakae sawa, kwani hawatavumiliwa.

Morogoro. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewataka wenyeviti wa Wilaya ya Malinyi wenye tabia ya vitendo vya rushwa inayosababisha migogoro ya wakulima na wafugaji kukaa mguu sawa, akisema Serikali haitawavumilia.

Chongolo ameeleza hayo leo Jumatano Februari Mosi, 2023 wakati akizungumza na wanaCCM na wananchi wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro katika mwendelezo ya ziara yake ya siku tisa mkoani hapa.

"Niwaambie kwa huyu Mkuu Wilaya (mpya- Sebastian Waryuba), mkae sawa sawa kama mwenyekiti wa kijiji alitengeneza laini kuruhusu mifugo mashambani na kuathiri wakulima aanze kukaa mguu sawa.

"Kama kuna mtu anaitwa mtendaji wa kata au kijiji alijitengenezea laini kwenye mifugo na kusababisha migogoro, akae mguu sawa sawa hilo halitawezekana tena, mtakuja kuniambia nikirudi tena hapa," amesema Chongolo.

Chongolo amesema baadhi ya wenyeviti wa vijiji wa Malinyi wamekuwa na tabia ya vitendo vya rushwa vinavyochochoea mgogoro kati ya wakulima na wafugaji, akimtaka mkuu wa wilaya kuwachukulia hatua haraka pindi watakaobainika

Amemtaka Waryuba akigundua wenyeviti wa vijiji 30 au 50 wana shida awakatame wote kuwaweka ndani kisha kuwafikisha mahakamani, akisema wakifanya hivi utatuzi wa migogoro hiyo utakwenda vizuri.

"Tukianzia hapa tutakwenda vizuri, afadhali ulalamilikiwe kwa kuchukua hatua, utaheshimika kuliko kulalamikiwa kwa kutochukua hatua.

“Usipochukua hatua madhara yake ni vifo, uharibifu kwa upande mmoja unaolalamika, lazima tuchukue hatua.

"Hili la wafugaji na wakulima linahitaji kuchukuliwa hatua kali nzito na kali ni afadhali ulalamikiwe kwa kuchukua hatua," amesema.

Baadhi ya wakazi wa Itete waliozungumza na Mwananchi, wamedau kuwa wenyeviti vijiji vya Malinyi ndio wamekuwa chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuchukua rushwa na kuruhusu mifugo kuingia shambani.

"Wenyeviti hapa ni shida wapo radhi wachukue fedha za wafugaji ili mashamba yako yatetekezwa na mifugo, ukimpelekea kesi hii kwake anakuona kama kinyago wala hana habari na wewe," amesema Peter Makoi.

Naye, Elimida Pascal alimuomba Chongolo kuangalia kwa jicho la tatu suala la wenyeviti wa vijiji akisema wamekuwa katika wakati mgumu akisema wafugaji wamekuwa wakipewa kipaumbele pindi mashamba yao yanapovamiwa na mifugo.