Huduma za kibingwa zatua hospitali 184 za halmashauri

Madaktari watakaotoa huduma za kibingwa kwenye hospitali za halmashauri nchini wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu,  wakati wa uzinduzi wa mpango huo mkoani Iringa leo. Picha na Tumaini Msowoya.

Muktasari:

Serikali imezindua huduma za madaktari bingwa walioweka kambi katika hospitali 184 za halmashauri nchi nzima, ili kuwapunguzia gharama wagonjwa waliokuwa wanatakiwa kufuata matibabu hayo kwenye hospitali za rufaa.

Iringa. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amezindua mpango wa makambi ya madaktari bingwa waliosambaa nchi nzima kutoa za matibabu kwenye hospitali zote 184 za halmashauri.

Madaktari bingwa watano wa upasuaji; afya ya uzazi, watoto na watoto wachanga, magonjwa ya ndani pamoja na wale wa ganzi na usingizi watakuwa wakitoa huduma za kibingwa kwenye hospitali moja ya halmashauri kwa muda wa siku tano.

Akizindua huduma hiyo iitwayo  Madaktari Bingwa wa Mama Samia, Waziri Ummy amesema watatoa huduma kwa bei waliyoikuta kwenye hospitali husika tofauti na wakati madaktari hao wanapofuatwa kwenye hospitali za rufaa ambazo huwa wanahudumia.

Amesema jumla ya madaktari bingwa 95 wameanza kutoa matibabu hayo leo, Mei 6, 2024 katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma, lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama wagonjwa wanaopaswa kwenda kupata matibabu kwenye hospitali za rufaa za mikoa, kanda na Taifa.

Kwa kawaida, kambi za huduma za madaktari bingwa, zimekuwa zikifanyika katika hospitali za rufaa za kanda au mikoa huku, magonjwa ya aina moja yakiwa ndiyo yanayopata matibabu.

“Kwa kila hospitali moja ya halmashauri, madaktari bingwa wa magonjwa matano wanaweka kambi kwa siku tano ili kuwahudumia wagonjwa kwa bei ileile waliyoikuta. Kitu hiki ni kikubwa na niwapongeze madaktari hawa wazalendo ambao wameamua kuwafikia wananchi,” amesema Waziri Ummy.

Amesema ni kweli Serikali chini ya Rais Samia imefanya kazi kubwa ya kujenga majengo na kuhakikisha uwepo wa vifaa tiba lakini bila matibabu kwa wagonjwa, haitakuwa imefikia azma yake ya kutoa huduma.

“Kazi ya Rais  haitakuwa na maana kama tutabaki kushabikia majengo na vifaa tiba isipokuwa huduma bora zenye staha kwa wananchi,” amesema Waziri Ummy.

Amesema Serikali ina mpango wa kushusha huduma za kibingwa kwenye hospitali za wilaya na kwa kuanzia, amezitaka halmashauri kushusha huduma hizo kwenye zahanati na vituo vya afya.

Amesema mbali na kumpunguzia mwananchi mzigo, lengo jingine la huduma hiyo ni kuwasogezea uzoefu madaktari wa ngazi za halmashauri katika kutoa huduma za kibingwa ili waweze kuwa kutatua baadhi ya changamoto, wakati wanapokutana nazo.

Vilevile, amesema huduma hizo za kibingwa zitaambatana na ufunguzi wa wodi maalumu za watoto wachanga ili kuokoa uhai wao na kupunguza vifo.

Kuhusu bima ya afya kwa wote,  Waziri Ummy, amesema watasimama kwenye mstari kuhakikisha sheria inafuatwa.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Herry James amesema huduma hizo zitawasaidia wananchi kupata matibabu huku akiiomba Serikali isaidie kusambaza mashirika ya lishe kwenye mikoa yenye changamoto ya utapiamlo.

James, amemuomba Waziri Ummy gari kwa ajili ya wataalamu wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa ili iwasaidie katika kutoa huduma za afya.