Chavda aomba nakala ya uamuzi ili akate rufaa Mahakama Kuu

Mfanyabiashara maarufu nchini, Pravinchandra Chavda (75) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusikiliza kesi yake ya kutoa taarifa za uongo Kituo cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Picha na Hadija Jumane
Muktasari:
- Mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kutoa taarifa za uongo Polisi kwa lengo la kupewa ripoti ya upotevu wa hati za tano za viwanja.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Pravinchandra Chavda (75) anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa taarifa za uongo kituo cha Polisi, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, impatie nakala ya uamuzi pamoja na mwenendo wa kesi yake, ili aweze kukata rufaa Mahakama Kuu.
Chavda ambaye ni mkazi wa Upanga, anakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kutoa taarifa za uongo Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central) kwa lengo la kujipatia ripoti ya upotevu wa hati za viwanja vitano na kisha kujipatia viwanja hivyo kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa huyo ametoa ombi hilo leo kupitia wakili wake Majura Magafu wakati kesi hiyo ya jinai namba 189/ 2024 ilipoitwa kwa ajili kuanza kusikilizwa.
Kesi hiyo inasikilizwa na hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Wakili Majura amedai kuwa mteja wake ameshindwa kukata rufaa Mahakama Kuu kutokana na kukosa nakala ya uamuzi uliotolewa Julai 18, 2024 na Mahakama hiyo pamoja na mwenendo wa shauri hilo tangu lilipofunguliwa.
"Mheshimiwa hakimu, kutokana na hali hii, tunaomba tupatiwe nakala ya uamuzi pamoja na mwenendo wa kesi kwa ujumla ili tuweze kukata rufaa Mahakama Kuu kutoka na uamuzi na Mahakama hii mwezi uliopita" alidai wakili Majura.
Wakili Majura aliwasilisha ombi hilo muda mfupi, baada ya wakili wa Serikali Frank Rimoy kuieleza Mahakama hiyo kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama mshtakiwa amekata rufaa au la.
"Mheshimiwa hakimu, kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama mshtakiwa amekata rufaa au la na kama hajakata rufaa tunaomba tuanze usikilizwaji wa ushahidi kwa kuwa tunaye shahidi mmoja ambaye yupo hapa mbele ya Mahakama" alidai Wakili Rimoy.
Rimoy, baada ya kutoa maelezo hayo, ndipo wakili Magafu alipoieleza mahakama kuwa wanaomba wapatiwe nakala hizo ili wachukue hatua ya ziada.
"Hatujakata rufaa kwa sababu tunasubiria tupatiwe nakala ya uamuzi ili tuchukue hatua ya ziada, ambayo ni kukata rufaa" alidai.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maeneo ya pande zote, alielekeza mshtakiwa huyo kupatiwa nakala hizo.
Baada ya kueleza alihirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2024 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji iwapo mshtakiwa atakuwa haja kamata rufaa lakini akikata rufaa shauri hilo litaitwa kwa ajili ya kutajwa.
Sababu ya mshtakiwa kukata rufaa:
Julai 18, 2024 Mahakama hiyo ilimgomea Chavda kufuta kesi hiyo na badala yake ilielekeza shauri hilo kuanza kusikilizwa Agosti 19, 2024 mahakamani hapo.
Mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo, baada ya kutupilia mbali pingamizi lililowasilisha na mashtaka huyo, akiomba kesi yake hiyo ifutwe kwa madai kuwa ni kesi ina asili ya madai na sio jinai na kwamba mwenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ni Mahakama Kuu.
Mshtakiwa huyo aliomba mahakama hiyo, ifute hati ya mashtaka na kumwachia kwa sababu katika mashtaka yake kuna mchanganyiko wa vitu ambavyo vinaonekana kuwa ni madai na sio jinai.
Baada ya uamuzi huo mshtakiwa huyo aliieleza Mahakama hiyo kuwa hajaridhika na uamuzi huo na kwamba anakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Katika uamuzi huo, uliotolewa na Hakimu Lyamuya alisema kuwa anatupilia mbali pingamizi lililowekwa na mshtakiwa kwa sababu mahakama haioni kama kuna kesi ya madai hasa ikizingatiwa kuwa kuna masuala ya ulaghai na kujipatia kiwanja kwa njia ya udanganyifu.
“Mahakama imepitia hoja zilizowasilishwa na pande zote, haioni kama kuna asili ya kesi ya madai katika hati hii ya mashtaka, badala yake inaona ni kesi ya jinai kwa sababu ndani yake kuna masuala ya ulaghai ambayo yameingia katika shtaka la kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo polisi, haya ni makosa ambayo yapo katika kanuni ya adhabu,” alisema hakimu Lyamuya.
Kesi ya msingi:
Mshtakiwa anadaiwa Januari 10, 2022 jijini Dar es Salaam, alijipatia kiwanja namba1814 kilichopo eneo la Msasani Peninsula kwa njia ya udanganyifu baada ya kuwasilisha kwa Msajili wa hati, nyaraka ya uhamisho wa kiwanja hicho akijifanya kuwa yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sole, kampuni ya uwekezaji ambayo ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua sio kweli.
Oktoba 7, 2019 katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Chavda alitoa taarifa za uongo kuhusiana na upotevu wa hati tano za viwanja kwa lengo la kujipatia hati za upotevu wa mali hizo wakati akijua sio kweli.
Iliendelea kudaiwa kuwa mshtakiwa akiwa jijini Dar es Salaam, huku akijua na kwa lengo la kudanganya alighushi nyaraka inayoitwa Maazimio ya Bodi akijaribu kuonyesha kwamba nyaraka hiyo ni halisi na imetolewa na Mkurugenzi wa Point Investment Limited, ambayo ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua si kweli.
Pia anadaiwa Januari 10, 2022 katika Jiji la Dar es Salaam, aliwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi kwa Msajili wa hati akionesha kwamba kiwaja namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula aliuziwa.
Ilielezwa kutokana na mazingira hayo mshtakiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi kuhojiwa na baada ya hapo alifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi hiyo.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Oktoba 23, 2023 na kusomewa mashtaka yanayomkabili na yupo nje kwa dhamana.