Mahakama yagoma kumfutia kesi Chavda, mwenyewe kukata rufaa

Mfanyabiashara maarufu nchini, Pravinchandra Chavda (75) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusikiliza kesi yake ya kutoa taarifa za uongo Kituo cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Picha na Hadija Jumane
Muktasari:
- Chadva anakabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kutoa taarifa za uongo Polisi, kwa lengo la kupewa ripoti ya upotevu wa hati tano za viwanja.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imegoma kumfutia kesi ya kutoa taarifa za uongo kituo cha Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, mfanyabiashara maarufu nchini, Pravinchandra Chavda (73) na badala yake imeelekeza kesi hiyo kuanza kusikilizwa Agosti 19, mwaka huu.
Mahakama hiyo imefikia hatua hiyo, baada ya kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na mshtakiwa huyo, akiomba kesi yake hiyo ifutwe kwa madai kuwa ni kesi ya madai na sio jinai, na kwamba chombo chenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ni Mahakama Kuu.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo kupitia wakili wake Majura Magafu, ameieleza Mahakama hiyo kuwa hajaridhika na uamuzi huo na kwamba anakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Chavda, raia wa India na mkazi wa Upanga, anakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kutoa taarifa za uongo Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kwa lengo la kujipatia ripoti ya upotevu wa hati za viwanja vitano na kisha kujipatia viwanja hivyo kwa njia ya udanganyifu.
Uamuzi huo umetolewa jana Julai 19, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, anayesikiliza kesi hiyo.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Lyamuya amesema kuwa anatupilia mbali pingamizi lililowekwa na mshtakiwa, kwa sababu mahakama haioni kama kuna kesi ya madai hasa ikizingatiwa kuwa kuna masuala ya ulaghai na kujipatia kiwanja kwa njia ya udanganyifu.
“Mahakama imepitia hoja zilizowasilishwa na pande zote, haioni kama kuna asili ya kesi ya madai katika hati hii ya mashtaka, badala yake inaona ni kesi ya jinai kwa sababu ndani yake kuna masuala ya ulaghai ambayo yameingia katika shtaka la kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo polisi. Haya ni makosa ambayo yapo katika kanuni ya adhabu” alisema hakimu Lyamuya
Hakimu Lyamuya baada ya kutupilia mbali pingamizi hilo, alielekeza kesi hiyo ianze kusikizwa Agosti 19, 2024, huku akitaka upande wa mashtaka kuja na mashahidi siku hiyo.
Muda mfupi baada ya kutolewa uamuzi huo, Wakili Magafu alidai kuwa mteja wake hajaridhika na uamuzi huo na kwamba anakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Magafu aliiomba mahakama hiyo impatie nakala ya uamuzi huo pamoja na mwenendo wa kesi hiyo.
Magafu baada ya kueleza hayo, hakimu Lyamuya alisema kuwa atapatiwa nakala ya uamuzi pamoja na mwenendo wa shauri hilo kama alivyoomba.
Awali, kabla ya kutoa uamuzi huo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisaidiana na Frank Michael, wamedai kuwa shauri hilo limeitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutolewa uamuzi na wapo tayari kusikiliza.
Mwanga baada ya kueleza hayo, wakili Magafu naye alidai yupo tayari kusikiliza uamuzi huo.
Pingamizi la Chavda
Chavda kupitia wakili wake, aliwasilisha pingamizi akidai hati ya mashtaka iliyopo mahakamani hapo asili yake ni kesi ya madai na sio kesi ya jinai.
Hivyo, aliomba mahakama hiyo, ifute hati ya mashtaka na kumwachia kwa sababu katika mashtaka yake, kuna mchanganyiko wa vitu ambavyo vinaonekana kuwa ni madai na sio jinai.
Mshtakiwa huyo alijikita katika shtaka la kwanza ambalo ni kujipatia mali (kiwanja) kwa njia ya udanganyifu, alidai mwenye mamlaka ya kutoa uamuzi juu ya mmiliki wa kiwanja hicho ni Mahakama ya Ardhi kwa kuwa shtaka lake asili yake ni kesi ya madai na sio jinai.
Vilevile, Magafu amedai hata shtaka la pili la mteja wake ambalo ni kutoa taarifa za uongo polisi kuhusiana na kupotea kwa hati ya kiwanja ni la madai na sio jinai.
Akijibu pingamizi hilo, wakili Mwanga alidai kuwa upande wa mashtaka shida yao sio kujua ua kuhakiki mmiliki wa ardhi ni nani, bali mchakato wa kupata viwanja hivyo kuna ulaghai umefanyika ndani yake kitu ambacho ni jinai.
"Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka tunasisitiza kuwa kesi hii iliyopo mbele yako ni ya jinai na sio madai kama ambavyo mshtakiwa anadai" amedai Mwanga
Kuhusu shtaka la kutoa taarifa za uongo pilisi, wakili Mwanga amedai shtaka hilo ni jinai na limewekwa katika kanuni ya adhabu na Mahakama hiyo ina mamlaka ya kuweza kusikiliza na kutolea uamuzi.
“Na pia hii ni mapema sana kwa Mahakama kujua shauri hilo ni la madai au jinai kwa kuwa ina mamlaka ya kusikiliza mashahidi na kujua kesi hii ni ya madai au jinai, hivyo kwa hicho lilichowasilishwa na upande wa utetezi ni ngumu kwa mahakama kujua kama ni jinai au madai ”amedai Mwanga na kuongeza:
“Kwa sababu upande wa mashtaka tunao ushahidi na kwa kuwa upande wa utetezi hawana ushahidi wetu, basi wasubirie kesi isikilizwe na kutokana na majibu yetu, tunaomba Mahakama itupilie mbali pingamizi lililowasilishwa na mshtakiwa” amedai Mwanga.
Kesi ya msingi
Mshtakiwa anadaiwa Januari 10, 2022 jijini Dar es Salaam, alijipatia kiwanja namba1814 kilichopo eneo la Msasani Peninsula kwa njia ya udanganyifu baada ya kuwasilisha kwa msajili wa hati, nyaraka ya uhamisho wa kiwanja hicho akijifanya kuwa yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sole, kampuni ya uwekezaji ambayo ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua sio kweli.
Oktoba 7, 2019 katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Chavda alitoa taarifa za uongo kuhusiana na upotevu wa hati tano za viwanja kwa lengo la kujipatia hati za upotevu wa mali hizo wakati akijua sio kweli.
Iliendelea kudaiwa kuwa mshtakiwa akiwa jijini Dar es Salaam, huku akijua na kwa lengo la kudanganya alighushi nyaraka inayoitwa maazimio ya bodi, akijaribu kuonesha kwamba nyaraka hiyo ni halisi na imetolewa na Mkurugenzi wa Point Investment Limited, ambayo ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua si kweli.
Pia anadaiwa Januari 10, 2022 katika jiji la Dar es salaam , aliwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi kwa msajili wa hati akionesha kwamba kiwaja namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula aliuziwa.
Ilielezwa kutokana na mazingira hayo mshtakiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha Polisi kuhojiwa na baada ya hapo alifikishwa Mahakamani na kufunguliwa kesi hiyo.
Hata hivyo, tangu upelelezi wa kesi hiyo ukamilike na mshtakiwa kusomewa hoja za awali( PH) Desemba 2023, na kupangiwa kuanza kusikilizwa Januari 10, 2024, kesi hiyo haikuweza kuendelea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mshtakiwa kuwa nje ya nchini kwa ajili ya matibabu.
Sababu nyingine ya kesi hiyo kutoendelea na usikilizwaji ni kutokana na mshtakiwa kuwasilisha malalamiko yake kwa DPP, ambayo yalisababisha jalada la kesi hiyo kupitiwa upya na Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa wa Dar es Salaam( RPO).
Jalada hilo lilipelekwa kwa RPO, Aprili 2024 kutokana na mshtakiwa huyo kuwasilisha malalamiko mbalimbali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), yakiweo ya kuomba kesi hiyo ifutwe.
Kutokana na malalamiko hayo, DPP alimuelekeza RPO kupitia upya jalada hilo, kabla ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Jalada hilo lilirudishwa mahakamani hapo Aprili 16, 2024 baada kupitiwa upya na RPO na Mahakama ilipanga Mei 14, 2024 kuanza kusiliza ushahidi.
Hata hivyo Juni 2024 mshtakiwa aliwasilisha pingamizi akiomba mahakama imfutie kesi hiyo kwa madai kuwa ina asili ya kesi ya madai.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Oktoba 23, 2023 na kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Chavda yupo nje kwa dhamana.