Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Changamoto tatu mwiba kwa wazee nchini

Muktasari:

Kuelekea siku ya wazee duniani ambayo huadhimishwa kila wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetaja changamoto kubwa tatu zinazowakabili wazee ikiwemo huduma duni za afya, uhakika wa kipato na ukatili.


S:

Herieth Makwetta, Mwananchi

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetaja changamoto kubwa tatu zinazowakabili wazee ikiwemo huduma duni za afya, ukatili na uhakika wa kipato.

WHO imesema wakati wazee wakikabiliwa na changamoto hizo, asilimia 93 ya wenye zaidi ya umri wa miaka 60 hawamo katika mfumo wa hifadhi ya jamii.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 27, 2022 jijini hapa, Mkurugenzi Mkazi Shirika la kimataifa la kusaidia wazee (Help Age International), Smart Daniel amesema Siku ya Wazee duniani ambayo itaadhimishwa Oktoba 3, 2022 jijini Dodoma itatumika kutafakari changamoto zinazowakabili wazee na kuona nini kifanyike ili kuwaboreshea maisha.

Amesema suala la huduma za afya ni changamoto kubwa kwa kundi hilo na kwamba wazee wengi wanakosa haki hiyo, “Mzee yeyote atakachokutajia nini anahitaji ni suala la afya ambalo ni hitaji muhimu kwao.”

Almesema kipato ni changamoto nyingine ambapo asilimia 93 ya wazee nchini hawapo katika mfumo wa hifadhi ya jamii hali inayosababisha ugumu wa maisha kwao.

“Ni asilimia 7 pekee ndiyo wapo kwenye hifadhi ya jamii na ukiangalia nchi zinazoendelea nyingi asilimia 20 ya wazee wapo kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii, Tanzania bado tupo nyuma sana,” amesema.

Smart ametaja ukatili kuwa unaliumiza zaidi kundi la wazee na kwamba takwimu zinaonyesha mpaka sasa zaidi ya wazee 40 wanauawa kila mwaka kutokana na imani za kishirikina.

“Angalau idadi inazidi kupungua miaka sita nyuma tulishuhudia wazee mpaka 600 wakiuawa kwa mwaka tumetoa elimu angalau imesaidia.”

Kwa upande wake mwakilishi wa WHO nchini Tanzania (WHO), Dk Zabulon Yoti amesema pamoja na kuwepo kwa sera, changamoto za wazee bado zipo nyingi ikiwemo masuala ya afya, upatikanaji wa kipato pamoja na ukatili wanaofanyiwa wazee.

''Oktoba Mosi kila mwaka huadhimishwa kama siku ya Umoja wa Mataifa ya wazee. Mwaka huu jijini Dodoma na kupitia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Desemba 14, 2022.

“Juhudi hizi zinaunganisha Serikali, mashirika ya kiraia, mashirika ya kimataifa, wataalamu, wasomi, vyombo vya habari na sekta binafsi ili kuboresha maisha ya wazee, familia zao na jumuiya zao,'' amesema

Amesema ni vema kuendeleza mazingira rafiki kwa wazee, kupambana na ubaguzi wa umri, utunzaji jumuishi kwa wazee na matunzo ya muda mrefu.

“Janga la Uviko19 limesababisha hofu na mateso makubwa kwa wazee kote duniani, mpango wa kitaifa wa kukabiliana na Uviko 19 unathamini ukweli kwamba wazee wako katika hatari kubwa  kuliko makundi mengine,'' amesema.

Dk Yoti amesema wazee ambao hawajachanjwa na watu walio na magonjwa sugu wako katika hatari kubwa ya athari ya Uviko19  na wana uwezekano mkubwa wa kulazwa hospitalini au hata kufariki ikiwa watapata ugonjwa huo.

Amesema mkakati wa kimataifa wa chanjo wa WHO unalenga chanjo ya asilimia 100  kwa wazee wote na wafanyakazi wa afya hivyo WHO nchini  Tanzania kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine imekuwa ikisaidia chanjo ya Uviko19 kama sehemu ya mwitikio wa Kitaifa.

Ofisa Programu wa dawa na vifaa tiba WHO, Rose Shija amesema tayari shirika lao limeweza kununua vifaa saidizi kwa wazee ambapo programu hiyo inatarajia kuanzia mkoani Morogoro vifaa hivyo vitapelekwa katika vituo vya huduma za afya.

Miongoni mwa vifaa hivyo saidizi ni pamoja na fimbo za kuweza kutembelea pamoja na wheerchair, vifaa hivyo vitapitia Bohari ya Dawa (MSD).