Chalamila awaita vijana wasio na mitaji ofisini kwake

Muktasari:
- Lengo ka kuwaita vijana hao ni kuwakutanisha na wafanyabiashara wakubwa waweze kuwakopesha bidhaa.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema vijana wanaotaka kufanya biashara eneo la Kariakoo wafike ofisini kwake ili kukopeshwa bidhaa za kuanzia kama mtaji.
Chalamila ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 27, 2025 katika sherehe za kilele cha uzinduzi wa ufanyaji biashara saa 24,uliofanyika jijini humo.
Shughuli za ufanyaji biashara saa 24 zilianza rasmi Februari 25,2025 ambapo kulikuwa na matukio mbalimbali yaliyokuwa yakifanyika.
Chalamila amesema pamoja na mambo mengine Kariakoo imeanza kufanya kazi saa 24 anaona ni wakati pia wa kuwawezesha vijana kwa kuwakutanisha na wafanyabiashara wakubwa ili waweze kuwakopesha bidhaa za kuanzia biashara.
"Naomba vijana waache kukaa huko kulalamika hawana kazi,waje wakopeshwe bidhaa nao waingie kwenye biashara na Serikali tutakuwa wadhamini wao,"amesema Chalamila.
Akilizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti Jumuiya ya wafanyabiashara soko la Kariakoo, Mfaume Mfaume amesema mitaji sio shida kwa wafanyabiasha katika eneo hilo la Kariakoo,shida ipo kwenye elimu ya ujasiri na ujasiriamali kwa vijana.
Mfaume amesema unaweza kumpa mtaji wa bidhaa kijana lakini akawa hana nia ya kuifanya biashara husika lakini pia akawa sio mwaminifu.
"Wafanyabiashara wakubwa wanataka watu waaminifu na unavyotuona wafanyabiashara wengi hapa Kariakoo tunafanya biashara kwa mali kauli hakuna mwenye fedha mfukoni,"amesema Makamu huyo.
Kijana aliyejitambulisha kwa jina la Joram Munuo mkazi wa Kinondoni, amesema wazo la Chalamila ni zuri lakini lisiwe ni kisiasa kwani ni kweli vijana wengi wanahitaji kufanya biashara lakini hawana mitaji.
"Pia hii itatusaidia vijana kutokuwa mawinga hapa Kariakoo ambapo unategemea uongeze bei ya bidhaa ya mwenye duka ili uweze kupata hela kidogo ya kuendesha maisha, ambapo kwa sasa tumekuwa wengi kutokana na uhaba wa ajira "amesema Munuo.
Ataka watu wasikate tamaa ufanyaji biashara saa 24
Katika hatua nyingind Chalamila amewataka wananchi na wafanyabiashara kupuuza maneno ya mtaani kuwa haiwezekani kufanya biashara saa 24.
Mkuu huyo wa mkoa alitolea mfano wa mabasi ya mkoani kusafiri usiku nalo pia lilipata upinzani wakati linaanza, lakini leo imewekana na kutaka watu wasikatishwe tamaa.
Kuhusu soko la Kariakoo ,amesema linatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ndio anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.