CCM yatoa msimamo mikopo kwa wanafunzi elimu ya juu

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla.

Muktasari:

  •  Mbunge wa CCM, jimbo la Bunda Vijijini, Mwita Getere akichangia mjadala bungeni alipendekeza kufutwa kwa fedha za kujikimu za wanafunzi (Boom).

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema maoni ya baadhi ya watu juu ya kuondolewa kwa fedha za kujikimu (boom) kwa wanafunzi wa elimu ya juu hayatazingatiwa, kwani hakuna haja ya kumpangia matumizi ya fedha mtu mzima.

Kauli ya CCM imetolewa leo Mei 9, 2024 ikiwa ni siku mbili baada ya mbunge wa chama hicho jimbo la Bunda Vijijini, Mwita Getere kutaka fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo ziondolewe kwa sababu hawasomi na wanaitumia isivyo, ikiwamo kwa ulevi.

Alisema fedha hizo ni vyema zikatumika kuwalipia ada wanafunzi wote wenye sifa.

Alitoa kauli hiyo jijini Dodoma akichangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyowasilishwa bungeni juzi.

Getere alisema, “Hii kitu kinaitwa Boom ni matatizo, wanafunzi wote wanaosoma na kupata boom hawasomi, wanalewa, wana nidhamu mbaya, nitakachokifanya ni kuwalipia wenye sifa ya kupata mikopo ada, tukimaliza tunapunguza matumizi,” amesema.

Mbunge huyo amesema watoto wengi wanahangaika kupata mikopo kwa ajili ya kulipa ada, hivyo itakuwa ni vyema njia hiyo kutumika, akipendekeza fedha za kujikimu zitolewe kidogo kwa wanafunzi ili wazazi wao washiriki.

Kauli hiyo iliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.

CCM katika taarifa imesema, “Maoni ya baadhi ya watu juu ya kuondolewa kwa fedha za kujikimu hayatazingatiwa kwani hakuna haja ya kumpangia matumizi ya fedha mtu mzima, bali CCM itaendelea kupokea maoni ya namna bora ya kuboresha na kuimarisha mikopo hii.”

Imeeleza Serikali haina mpango wa kufuta au kuondoa mikopo hiyo kwani ina tija kubwa, kwa kutoa nafasi hasa kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia zisizoweza kugharimia elimu ya juu, kusoma vyuo vikuu nchini.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla inaeleza katika kutimiza azma hiyo, Serikali iliongeza fedha ya kujikimu, kutoka Sh8,500 kwenda Sh10,000 kwa siku.

“Kama ambavyo tumeahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi (2020-2025) katika ukurasa wa 131, tutaendelea kuhakikisha wanafunzi wengi wenye uhitaji na sifa wanapata fursa ya kujiunga na elimu na kupata mikopo kama inavyostahili,” imesema CCM.

Makalla amewahakikishia wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vikuu kuwa chama hicho kitaendelea kubeba matarajio na masilahi yao kwa namna ya kipekee.

“Tunauhakikishia umma wa Watanzania kuwa CCM itaendelea kuisimamia Serikali kutenga na kutoa pesa hizi za kujikimu na gharama nyingine kwa wanufaika wengi zaidi wenye sifa stahiki,” imeelezwa.