Bweni la shule laungua moto Simanjiro

Muktasari:
Bweni hilo la shule ya sekondari Ewong'oni wilayani Simanjiro mkoani Manyara, limeungua moto mchana wakati wanafunzi hao wakifanya mtihani wa majaribio
Simanjiro. Bweni la wanafunzi wavulana wa shule ya sekondari Ewong'oni wilayani Simanjiro mkoani Manyara limeungua moto na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwemo ndani.
Diwani wa kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Taiko Laizer amesema tukio hilo limetokea leo Jumatano, Mei 19, mwaka huu.
Taiko amesema bweni hilo limeungua moto wakati wanafunzi hao wakiwa darasani wanafanya mtihani wa majaribio.
Amesema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana ila kila kilichokuwa huko ndani ya bweni kimeteketea kwa moto.
Amesema hakuna mwanafunzi yeyote aliyedhurika Ila vitu vyote vilivyokuwemo ndani ikiwemo nguo za wanafunzi na magodoro vimeteketea.
"Tunamshukuru Mungu hakuna mtoto aliyedhurika ila kila kilichokuwa ndani ya bweni kimeteketea kwa moto," amesema Laizer.