Bosi UWT achangia ujenzi kituo cha watoto Dodoma

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Mary Chatanda

Muktasari:

Siku chache baada ya Mary Chatanda kuchaguliwa kushika nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, ameenda kushukuru Mungu kwa kuchaguliwa kupata nafasi hiyo na kuchangia ujenzi wa kituo cha watoto.

Dodoma. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Mary Chatanda amechangia Sh1 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la watoto wadogo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Bethel uliopo Chadulu, jijini Dodoma.

  

Chatanda ametoa mchango huo leo Jumapili Desemba 04, 2022 wakati alipokwenda kumshukuru Mungu kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.


Katika uchaguzi wa UWT uliofanyika Novemba 28, 2022, Chatanda aliibuka mshindi kwa kupata kura 527 huku aliyekuwa mwenyekiti akitetea nafasi hiyo, Gaudentia Kabaka akipata kura 219.


Wengine waliokuwa wakiwania kiti hicho cha UWT, ni Dk Wemael Chamshama, Mariam Lulida wao waliambulia kura moja moja kati ya kura 756 halali zilizopigwa.


Amesema alikwenda katika kanisa hilo kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa mambo makuu aliyomtendea kwa kupata uenyekiti wa UWT Taifa.


Chatanda amesema pamoja na hilo katika kanisa hilo kulikuwa na shughuli za kijamii kwa harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la kufundishia watoto wadogo.


“Kwa hiyo walikuwa na harambee, nikaahidi kuchangia Sh1 milioni na mifuko 100 ya saruji ambayo nimetoa kwa niaba ya Rais (Samia Suluhu Hassan),” amesema.