Boni Yai akwama mahakamani kulinda ‘password’ za simu zake

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob akiwa kizimbani. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Boni Yai kupitia wakili wake Hekima Mwasipu alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu, chini ya hati ya dharura, akiiomba iitishe kumbukumbu za mwenendo wa Mahakama ya Kisutu, ijiridhishe na usahihi na uhalali wake, hatimaye itengue amri hiyo
Dar es Salaam. Meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob amekwaa kisiki baada ya Mahakama Kuu kumkatalia maombi yake kupinga amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, kulipa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni nywila (password) za simu zake.
Jacob, maarufu Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Kisutu.
Katika kesi hiyo namba 26918/2024, anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RCO), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) David Msangi aliwasilisha maombi akiiomba Mahakama imuamuru mshtakiwa kutoa nywila za simu zake mbili za mkononi kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma hizo.
Maombi hayo namba 29695/2024 yaliamuriwa upande mmoja, Mahakama hiyo ilimuamuru Boni Yai kufika ofisi ya RCO na kutoa nywila kufungua simu zake mbili za mkononi aina ya Samsung Galaxy S20 Ultra SG na Samsung Galaxy S23 Ultra.
Boni Yai kupitia wakili wake Hekima Mwasipu alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu, chini ya hati ya dharura, akiiomba iitishe kumbukumbu za mwenendo wa Mahakama ya Kisutu, ijiridhishe na usahihi na uhalali wake, hatimaye itengue amri hiyo.
Alidai amri hiyo ilitolewa bila kumpa kwanza Boni Yai haki ya kusikilizwa.
Hata hivyo, Serikali iliibua pingamizi la awali likipinga shauri hilo lisisikilizwe kwa kuwa ni batili kisheria huku ikitoa sababu mbili.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Anold Kirekiano Novemba 28, 2024, imeikataa sababu moja ya pingamizi la Serikali na kukubaliana na sababu moja ambayo imetosha kutupilia mbali shauri hilo.
Serikali ilidai shauri hilo halina ustahilifu na ni batili kwa kukiuka kifungu cha 43(2) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu (MCA), sura ya 11 marejeo ya mwaka 2019
Jaji Kirekiano baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria na kesi rejea zilizorejewa na mawakili wa pande zote, amesema Mahakama Kuu inaweza kuitisha na kuchunguza kumbukumbu za mwenendo wa Mahakama za chini.
Hata hivyo, amesema pale uamuzi au amri iliyotolewa na Mahakama ya chini inapokuwa haina athari ya hitimisho, chini ya kifungu cha 372 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Mahakama hiyo inawekewa ukomo wa mamlaka ya kuifanya mapitio.
Hivyo, amesema hakubaliani na hoja za Wakili Mwasipu kuwa mtu asiyeridhika na uamuzi usiohitimisha haki za wadaawa, ambao umezuiwa chini ya kifungu cha 372 (2) cha CPA anaweza kuomba mapitio chini ya kifungu cha 372(1) CPA.
Amesema kwa kuzingatia maombi na nafuu zilizoombwa katika hati ya maombi, kwamba yapo katika uamuzi uliotolewa ambao umewekewa ukomo chini ya kifungu cha 372 (2) CPA na kifungu cha 43 (2) MCA.
"Kwa kuzingatia hayo, sababu ya kwanza ya pingamizi ina mashiko na inakubaliwa. Shauri lililoko mbele yangu halina ustahilifu. Amri sahihi ni kulitupilia mbali (striking out na siyo dismissal). Kwa kusema hayo yote, shauri hili linatupiliwa Mbali," amesema Jaji Kirekiano.
Awali, wakati wa usikilizaji wa pingamizi hilo, Boni Yai aliwakilishwa na mawakili Hekima Mwasipu na Michael Lugina na Serikali iliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Wandamizi, Clemence Kato na Nura Manja na Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi.
Katika sababu hiyo iliyokubaliwa na Mahakama, Wakili Kato alidai amri (ya Mahakama ya Kisutu) katika shauri la maombi namba 29695 /2024, iliyomuamuru Boni Yai kutoa nywila za simu zake haikuamua hatima ya shtaka linalomkabili katika Mahakama hiyo ya chini.
"Hivyo shauri hili huangukia katika mawanda ya kifungu cha 43 (2) cha MCA, hii ndio kusema kuwa, ni amri isiyohitimisha shauri ambalo haliwezi kufanyiwa mapitio," amesema Wakili Kato.
Kusisitiza hoja hiyo, aliirejesha Mahakama katika msimamo wa Mahakama ya Rufani kwenye rufaa za kesi mbalimbali ilizokwisha kuziamua kuhusiana na hoja hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Mwasipu amesema amri hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu haiko zile zisizofanyiwa mapitio kwa kuwa haki ya mwombaji (Boni Yai) kusikilizwa iliamuriwa na kumalizika kwani shauri la maombi namba 29695/ 2024 lililoomba amri hiyo lilishaamuirwa na kumalizika.
Wakili Mwasipu alidai kuwa, kama amri hiyo (iliyokuwa inapingwa), ya kutoa nywila za simu Boni Yai ingetolewa katika kesi ya msingi, ingekuwa ni aina y amri zinazozuiliwa kufanyiwa mapitio.
Hivyo, aliiomba Mahakama kuzingatia msimamo wa Mahakama ya Rufani kama ilivyoelezwa katika moja ya rufaa ilizowaho kuziamua.
Amesema katika kesi hiyo Mahakama hiyo ilisema kuwa licha ya msimamo wa kifungu cha 43 (2) cha MCA, haikuwa dhamira ya Bunge kuzuia mamlaka ya Mahakama Kuu kuitsha na kukagua mwenendo wa mashauri ya Mahakama za chini kujiridhisha na uhalali na usahihi wake.
Aliirejesha Mahakama katika uamuzi wa Mahakama ya Rufani kwenye rufaa ya jinai baina ya Wakili Peter Madeleka dhidi ya Jamhuri.
Kuhusu kesi hiyo alisema Mahakama hiyo ilisema hata kama amri itaoneakana kuwa ni aina ya amri zinazozuiwa kufanyiwa mapitio, bado Mahakama hiyo inaweza kutumia mamlaka yake ya kimapitio kujiridhisha na usahihi wa mwenendo wa mashauri ya mahakama za chini.
Wakili Kato alipinga hoja hizo za Wakili Mwasipu akidai kuwa haki ya wadaawa itaamuriwa katika uamuzi wa kesi ya msingi inayosubiri kusikilizwa.