Boni Yai akabidhi ofisi ya Chadema Ubungo, wajipanga kushinda mitaa 47

Mwonekano wa Ofisi mpya ya jimbo la Ubungo la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zilizopo Kata ya Msewe baada ya ujenzi wake kukamilika
Muktasari:
- Ujenzi wa ofisi ya Jimbo la Ubungo uliokuwa ukisusua kwa miaka kadhaa umekamilika na kukabidhiwa kwa viongozi, baada ya aliyekuwa meya wa Kinondoni, kumalizia ujenzi huo.
Dar es Salaam. Meya wa zamani Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, Boniface Jacob amesema Chama cha Demokrasia (Chadema) Wilaya ya Ubungo imejipanga kuibuka kidedea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 2024 kutokana na maandalizi wanayoendelea kuyafanya.
Miongoni mwa maandalizi hayo ni kukamilika kwa ofisi ya Jimbo ya Ubungo huku Kibamba mchakato ukiendelea. Ofisi hizo zitatumika katika kuratibu shughuli za uchaguzi huo kwa nyakati tofauti.
Jacob aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, amesema hayo leo Jumapili, Juni 23, 2024 wakati akikabidhi ofisi ya Jimbo la Ubungo, baada ya kumalizia ujenzi wake ulioanzia Mei 12, 2024.
"Nguvu ya Chadema kushinda mitaa 47 ya Ubungo ipo kutokana na kuwa na timu nzuri ya wilaya na kata itakayowezesha ushindi wa mitaa. Tuna wanachama wa Chadema walio tayari kupambania ushindi wa Chadema," amesema Jacob.
Jacob maarufu Boni Yai amesema haoni sababu ya Chadema kushindwa kuinyakua mitaa 47 ya wilaya hiyo, kutokana na uwepo wa vitendo kazi ikiwemo ofisi mpya ya kisasa ya maandalizi ya mchakato huo.
"Mimi na wanachama wenzangu tulichokifanya ni kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kisasa ili iwe ngome ya ushindi kuanzia Serikali za mitaa. Sasa tunachowaidai viongozi wetu ni matokeo ya Serikali za mitaa, nataka ofisi itumike hadi kwa ajili ya mikutano.
"Tuna deni kubwa la kukomboa mitaa yetu 47 ya Jimbo la Ubungo iliyokwenda chama tawala cha CCM," amesema.
Kuhusu ujenzi wa ofisi hiyo Jacob amesema:"Nilichokifanya nimemalizia sehemu ya ujenzi wa ofisi maana kwa muda mrefu ilikuwa kama boma, viongozi wa jimbo walinifuata na kuniomba nishiriki mchakato.
"Natambua nguvu na jitihada za wanachama wa Chadema mbalimbali waliofanikia suala kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013.
"Kilichobaki sasa ni samani za ndani najua mtajiuliza inakuaje mbona ametukabidhi ofisi tu, nawaahidi ninakwenda kuwatafutia ili mfanye shughuli zenu katika mazingira bora," amesema Jacob.
Mbali na hilo, Jacob amesema atashiriki mchakato wa ofisi bora za kisasa za majimbo mbalimbali yakiwamo ya Kibamba na Temeke ili kuhakikisha viongozi wanakuwa katika mazingira mazuri kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Katibu wa Jimbo la Ubungo, Moses Odinga, amesema:"Ni siku ya furaha kwetu kukamilka kwa ofisi ya jimbo la Ubungo, hii ni zawadi kwetu kukabidhiwa ofisi yetu.
"Mara mwisho Mei 12 tulikutana hapa baada ya kuleta vifaa, haikuwa kazi rahisi alipotuahidi kukamilisha ujenzi wa ofisi hii. Hii ni ofisi ya chama kila mmoja ajisikie yupo huru," amesema Odinga.