Bilioni 20 kukarabati vyanzo vya umeme Kidatu, Mtera na Kihansi

Eneo la Bwawa la kuzalishia umeme la Kihansi
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali imetoa Sh20 Bilioni kwa ajili ya kukarabati vyanzo vya umeme vya Kidatu, Mtera na Kihansi.
Iringa. Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali imetoa fedha Sh20 Bilioni kwa ajili ya kukarabati vyanzo vya umeme vya Kidatu, Mtera na Kihansi.
Kapinga amesema hayo Septemba 9, 2023 wakati Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea Bwawa la Kuzalisha umeme la Kihansi, Mkoani Iringa.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha unazalishwa umeme unaotosheleza mahitaji ya nchi na ziada.
"Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu tayari fedha za ukarabati wa vyanzo vya kuzalisha umeme zimeshatolewa, Sh8 bilioni (Mtera), Sh8 bilioni (Kihansi) na Sh4 Bilioni (Kidatu)," amesema Kapinga.
Amewatoa hofu Watanzania kuhusu suala la umeme na kwamba mpaka februari mwakani, Bwawa la Mwalimu Nyerere litakuwa limeanza kufanya kazi.
Kapinga amewataka wanachi kuendelea kutunza mazingira ili kutoathiri upatikanaji wa maji ambayo ni chanzo cha umeme.
Awali Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ussi Salum amesema ziara yao imelenga kuona vyanzo vya kuzalisha umeme ili kujiridhisha na maendeleo yake.
Hata hivyo amesema licha maji kupungua, uzalishaji wa umeme utaendelea na hakutakuwa na upungufu.