Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki za Equity zaanza kutoa ushahidi mkopo tata kwa Kahama Oil Mills

Muktasari:

  • Katika kesi hiyo wadai, kampuni ya Kahama Oil Mills na wenzake wanapinga kudaiwa na Benki za Equity Dola milioni 46 (zaidi ya Sh122 bilioni) za mkopo wanaodaiwa kupewa na benki hizo, wakidai licha ya kusaini mkataba benki hizo hazikutekeleza. Benki hizo zinadai ziliwapatia mkopo huo na hawajalipa.

Dar es Salaam. Benki za Equity Tanzania Limited (EBT) na Equity Kenya Limited (EBK), zimeanza kutoa ushahidi katika kesi nyingine ya mgogoro wa malipo ya mkopo wa Dola za Marekani milioni 32.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara na kampuni za Kahama Oil Mills Limited na Kahama Import & Export Commercial Agency Limited, zinazodaiwa kukopeshwa fedha hizo na benki hizo.

Wadai wengine katika kesi hiyo namba 78/ 2023 ni wadhamini wa mkopo unaobishaniwa; Kom Group of Companies Limited, Shinyanga Royal Pharmacy (2015) Limited, Royal Supermarket (2008) Limited na Mhoja Nkwabi Kabalo, mkurugenzi wa kampuni hizo.

Kesi hiyo ni mwendelezo wa kesi mbalimbali zilizofunguliwa dhidi ya benki hizo na kampuni zinazodaiwa kukopeshwa na benki hizo mabilioni ya fedha, kisha zikazifungulia kesi benki hizo zikipinga kudaiwa kwa madai kwamba hazikukopeshwa na benki hizo au zimeshalipa mkopo.

Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo baada ya kuandikiwa barua na benki hizo zikiwataka kulipa zaidi ya Dola 46.6 milioni za Marekani (sawa na zaidi ya Sh122.54 bilioni).

Kiasi hicho cha fedha kinajumuisha deni la msingi la mkopo wa Dola milioni 32 (zaidi ya Sh84 bilioni) ambao benki hizo zinadai zilizikopesha kampuni hizo pamoja na riba.

Kesi hivyo inayosikilizwa na Jaji Profesa Agatho Ubena, iko hatua ya utetezi ambao umeanza kutoa ushahidi wake baada ya upande wa wadai kufunga ushahidi wake kupinga kukopeshwa na kudaiwa na benki hizo.

Katika hatua hiyo, benki hizo zinazowakilishwa na Wakili Zharani Sinare, kupitia mashahidi wake zinatoa ushahidi unaolenga kupangua hoja na madai ya wadai kuwa hazikuwakopesha pesa hizo na kuthibitisha madai yake kinzani kuwa zilizikopesha kampuni hizo kiasi hicho cha fedha na zimekataa kurejesha.

Hata hivyo, shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi (benki hizo) ofisa wa Equity Bank Kenya, Michael Kessy kutoka idara ya mikopo, ameieleza Mahakam hiyo kuwa hakushiriki katika mchakato wa utolewaji wala usimamizi wa mikopo hiyo kwa kuwa wakati huo alikuwa hajaajiriwa na benki hizo.

Kessy ametoa maelezo hao leo Jumatatu Julai 22, 2024, wakati akihojiwa maswali ya dodoso na wakili wa kampuni hizo (wadai), Frank Mwalongo, kuhusiana na ushahidi wake aliouwasilisha mahakamani hapo kwa njia ya maandishi pamoja na nyaraka mbalimbali alizoziwasilisha kama vielelezo vya ushahidi wake.

Sehemu ya mahojiano baina ya wakili Mwalongo na shahidi huyo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Kielelezo P3F (kielelezo cha 3F cha upande wa wadai, taarifa ya benk ya akaunti), ieleze Mahakama Dola 26,592,232 zimeingia kwenye akaunti ya mdaiwa wa kwanza (Kahama Oil Mills) kutoka kwa nani?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, maelezo hapa ni Kom Group of Companies Limited- Escrow account.

Wakili: Dola milioni 4.2 kwenye hiyo bank statement inasema imetoka wapi?

Shahidi: Imeandikwa Kom Group Companies Limited

Wakili: Una statement nyingine yoyote inaonyesha Dola milioni 26 na milioni 4 inaonyesha hizo hela zimetoka mdaiwa wa pili Equity Bank Kenya Limited (EBK)?

Shahidi: Hapana, hii ndio statement ambayo inaonyesha hela zilizoingia.

Wakili: Kwa nafasi yako ya kuwa mwajiriwa wa EBK haufahamu yaliyokuwa yanatokea?

Shahidi: Siyo kweli.

Wakili: Wakati pesa inatumwa kutoka Kom Group of Companies ndani ya EBK wewe haukushiriki kutuma hiyo pesa kweli au si kweli?

Shahidi: Kweli.

Wakili: Akaunti zilizotumika kutuma pesa katika hii transaction (miamala) kule Kenya wewe hukushiriki kuzifungua, kweli au si kweli?

Shahidi: Ni kweli mimi sikushiriki.

Wakili: Kwa mujibu wa madai kinzani, wewe haukushiriki kwenye utoaji na usimamizi hiyo mikopo kutoka, kweli?

Shahidi: Siyo kweli

Wakili: Wewe Kessy haukushiriki utoaji pesa kutoka EBK kwenda Kom Group of Companies, ni kweli au si kweli?

Shahidi: Ni kweli, mheshimiwa Jaji.

Wakili: Pia haukushiriki utoaji pesa toka Kom Group of Companies kuja kwa mdai wa kwanza, kweli?

Shahidi: Ni kweli mimi mwenyewe personal sikushiriki sababu nilikuwa bado sijawa mwajiriwa.

Wakili: Hata leo hii kwa nafasi yako huwezi kuingia kwenye mfumo kuangalia zile transactions (miamala) ya pesa kutoka EBK kuja Kom Group of Companies na kutoka Kom Group of Companies kwenda kwa mdai wa kwanza (Kahama Oil Mills?

Shahidi:Ndio

Wakili: Habari ya kwamba pesa imetoka EBK (kwenda kwa wadai wa kwanza na wa pili) una nini ambacho kinaonyesha hiyo au ni mawazo yako tu?

Shahidi: Kuna nyaraka nyingine zinaonyesha.

Baada ya mahojiano hayo, kesi hiyo imeahirishwa mpaka Alhamisi Julai 25, 2024, ambapo shahidi huyo ataendelea kuhojiwa maswali ya dodoso, kabla ya mashahidi wengine wa utetezi kuitwa.

Katika kesi hiyo, kampuni hizo licha ya kukiri kuingia mikataba na benki hizo wa mkopo wa jumla ya Dola milioni 32 za Marekani iliyosainiwa na pande zote Mei 28, 2018 na Juni 19, 2020, zinapinga kupokea mkopo huo kutoka kwa benki hizo.

Badala yake zinadai kuwa benki hizo zilitoa kiasi hicho cha pesa Dola milioni 32 kwa kampuni ya Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya na kwamba wenyewe  walipokea mkopo wa jumla ya Dola milioni 30 kutoka kwa Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya na si kwa benki hizo.

Pia zinadai kwamba zimeshalipa sehemu ya mkopo huo kwa kampuni hiyo, huku wakitaja nyaraka za uthibitisho wa malipo hayo ambazo watazitumia kama vielelezo vya ushahidi wao.

Hivyo wanaiomba Mahakama itamke kuwa mkataba wa makubaliano ya mkopo wa Kibenki baina yao na benki hizo uliosainiwa Mei 28, 2018 na Juni 19, 2020 haukutekelezwa na kwamba benki hizo zilikiuka mkataba wa makubaliano ya mkopo huo kwa kushindwa kuwapatia mkopo huo.

Pia wanaiomba Mahakama itamke kuwa benki hizo hazina madai yoyote dhidi yao na kwamba dhamana za mkopo walizozikabidhi kwa benki hizo zinashikiliwa isivyo halali na iamuru benki hizo ziziachilie dhamana hizo pamoja na kuwarejeshea hati mmiliki za amana hizo.

Vilevile wanaiomba Mahakama hiyo itaziamuru benki hizo kumlipa mdai wa kwanza Dola milioni 1.3 ambazo EBK ilizilipa kwa kampuni ya Nisk Capital Limited, kinyume cha mkataba baina ya mdai wa kwanza na mdaiwa wa pili, malipo ambayo invoice iliwasilishwa kwake mdaiwa wa kwanza.

Wadai hao pia wanaiomba Mahakama hiyo iziamuru benki hizo, ziwalipe riba, fidia ya hasara ya jumla na gharama za kesi.

Hata hivyo, benki hizo nazo zimefungua madai kinzani dhidi ya wadai, zikipinga madai ya kukiuka masharti ya mkataba wa mkopo wa kibenki kwa kushindwa kuutekeleza na kwamba zilitoa mkopo huo kwa kampuni ya Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya na si kwako.

Benki hizo zinawataka kuthibitisha madai hayo na uwepo wa kampuni inayojulikana kama Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya ambayo wanadai kuwa ndivyo EBK iliipatia mkopo wa Dola milioni 32.

Badala yake benki hizo zinadai kuwa zilitoa mkopo huo wa Dola milioni 32 kwa mdaiwa wa kwanza na wa pili.

Benki hizo zimetoa mchanganuo wa utoaji wa mkopo huo kwa awamu tofautitofauti, zikionyesha tarehe na kiasi cha pesa zilizoingizwa katika akaunti za benki zinazodaiwa kuwa za wadai hao.

Zinadai kuwa zilitimiza wajibu wake wa kimkataba kama kama walivyokubaliana, lakini wadai hao (wakopaji) waliokiuka masharti ya mkataba wa mkopo.

Zinadai kuwa mpaka kufikia Julai 26, 2023 deni la msingi lilikuwa limeshafikia zaidi ya Dola milioni 47.2 (sawa na zaidi ya Sh124 bilioni), ambalo riba inazidi kuongezeka kwa kiwango kilichokubaliwa kimkataba mpaka malipo yote yatakapokamilika.

Kwa hali hiyo benki hizo zinadai kuwa zinastahili kushikilia amana zote zilizowekwa kama dhamana ya mkopo huo.

Hivyo, nazo zinaomba Mahakama hiyo iitupilie mbali shauri la madai ya wadai na  itoe amri kwamba mdai wa kwanza na wa pili (wakopaji) wamekiuka vigezo na masharti ya mkataba wa mkopo uliosainiwa na pande zote Mei 28, 2028.

Pia zinaomba Mahakama itamke kwamba wadaiwa wa tatu, wa nne, wa tano na wa sita (wadhamini) wanawajibika kwao wadaiwa.

Vilevile zinaomba amri ya Mahakama kwa wakopaji na wadhamini kwa pamoja na mmoja mmoja kulipa zaidi ya Dola milioni 47.2 (sawa na zaidi ya Sh124 bilioni).