Barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi kujengwa kiwango cha lami

Muktasari:

  1.  Kilio cha Wananchi wanaotumia barabara ya Kimara,Bonyokwa hadi Kinyerezi cha sikika sasa washusha pumzi, baada ya Serikali kumpata mkandarasi atakayejenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ndani ya miezi 16

Dar es Salaam. Kilio cha changamoto ya usafiri kwa wananchi wanaotumia barabara ya Kimara, Bonyokwa hadi Kinyerezi kimesika baada ya Serikali kumpata mkandarasi wa kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita sita, iliyokuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu, itaanza kujengwa mwezi huu na mkandarasi, kampuni ya Nyanza Road Works Ltd kwa thamani ya Sh24 bilioni na ujenzi utakamilika Juni, 2025.

Kampuni hiyo inaijenga barabara hiyo baada ya kuingia mkataba na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuijenga kwa kiwango cha lami, njia ya watembea kwa miguu, kuweka mitaro ya kupitisha maji sambamba na kufunga taa.

Kukamilika kwa ujenzi wake kutaleta ahueni kwa wananchi, kwani kipindi cha mvua magari hayapiti, hivyo kulazimika kutumia usafiri wa bodaboda kwa Sh7,000 au zaidi kutegemeana na umbali wa eneo unaloishi.

Mkazi wa Mavurunza, Salome Ayoub amesema mvua zikinyesha hali inakuwa tete kwa watumiaji wa barabara hiyo, huku akieleza foleni ya magari inakuwa kubwa kutokana na ubovu wa barabara.

Amesema shughuli zake za kujipatia kipato anafanyia katikati ya mji, hivyo kila siku analazimika kutumia gharama kubwa kwenye usafiri.

“Kupanda bodaboda kutoka Kimara hadi hapa Mavurunza ni Sh6,000 mvua zikinyesha tunapitia magumu mengi, tunaishukuru Serikali kwa kusikia kilio chetu,” amesema.

Kwa upande wake, Jacob Steven amesema anatarajia uwekezaji mkubwa baada ya kukamilika kwa barabara hiyo huku akieleza sehemu nyingi zilikuwa chini kimaendeleo kutokana na changamoto ya barabara.

Diwani wa Kimara, Ismail Mvungi amesema kuanza kujengwa kwa mradi huo sasa kunampaisha katika nafasi yake hiyo, huku akieleza hali ilikuwa tete kwake kwani baadhi ya wananchi walimtahadhirisha kuwa hawawezi kumpigia kura kama barabara hiyo haitajengwa.

“Ofisini kwangu malalamiko yalikuwa mengi na ilifikia hatua wananchi wanaongea hadharani hawawezi kunichagua katika uchaguzi ujao, sasa kujengwa kwake si furaha kwa raia pekee bali hata mimi nimejitengenezea nafasi nzuri,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Meneja na msimamizi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya Nyanza, Mhandisi Gilberti Bahesha amesema wamejipanga kukamilisha ujenzi huo kwa kuzingatia muda wa mkataba.

“Tunajenga na hadi Juni mwakani tutaikabidhi, ili wananchi waanze kuitumia na kuondokana na changamoto ya usafiri,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa miradi Tanroads, Japherson Nnko amesema ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha daraja lenye mita 25 na madaraja madogo saba ya karavati na mkandarasi atatakiwa kufunga taa.