Kilometa 250 za barabara kujengwa Dar Aprili

Muktasari:

  • Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Mkoa wa Dar es Salaam, umesema kuanzia Aprili mwaka huu, wataanza utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili itakayogharimu zaidi ya Sh1 trilioni.

Dar es Salaam. Zaidi ya kilometa 250 zinatarajiwa kujengwa katika awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), utakaoanza Aprili mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo,  Alhamisi Januari 18, 2024  na Meneja wa  Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga wakati akitoa taarifa kuhusu mwenendo wa miradi ya DMDP kwa Kamati ya siasa ya Mkoa na Wilaya zote tano za Dar es Salaam waliotembelea ofisini kwake.

Mkinga amesema awamu ya pili ya DMDP utagharimu zaidi ya Sh1 trilioni fedha zitakazotolewa na Benki ya Dunia (WB) na Serikali ya Uholanzi kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya barabara, usimamizi wa taka ngumu (madampo), masoko na vituo vya mabasi, mifereji na bustani.

“Awamu ya pili ya DMDP itakuwa na utekelezaji katika sehemu kuu mbili ya kwanza itaanza Aprili ambapo jumla ya kilomita136 za barabara zitajengwa ikiwemo barabara ya Banana hadi Kivule yenye urefu wa kilometa 16.

“Mwezi ujao baada ya kukamilika kwa mapitio ya usanifu tutatangaza zabuni ya kuwapata wakandarasi watakaoanza ujenzi Aprili, kilometa zilizobaki zitaanza ujenzi kuanzia Juni katika awamu ya pili ya mradi huu,” amesema Mkinga.

Mkinga amesema asilimia 78 ya fedha za mradi wa DMDP awamu ya pili zimeelekezwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara na masoko na asilimia zilizobaki zitatumika katika maeneo mengine.

Kwa mujibu wa Mkinga, Ilala imepewa kilomita 53.5 za barabara, Temeke (42), Kigamboni (57), Ubungo (52) na Kinondoni (48), zitakazotekelezwa kwa awamu tofauti hadi kukamilika kwake.

Miongoni mwa maeneo yatakayojengwa barabara ni Manzese, Tabata, Sinza, Majumbasita hadi Stakishari.

Maeneo mengine ni Tabata Mawenzi, Migombani, Tabata Baracuda hadi Chang’ombe, Mbezi Msumi, Kigamboni na Pemba mnazi mchakato utakaokwenda sambamba na ujenzi wa vivuko nane vya waenda kwa miguu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu aliyewahi kuwa mbunge wa Temeke kwa miaka 10 amewapongeza Tarura huku akiwataka kuandaa vema barabara ili kuwapa wajumbe wa chama hicho.

“Kwa wanaoijua Dar es Salaam, hali ilikuwa mbaya, tulipiga kelele tulivyokuwa wabunge lakini kwa hatua hii ya Tarura tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, hizi barabara zitaibadilisha Dar es Salaam,” amesema Mtemvu.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Nasra Mohamed amesema Tarura imefanya kazi nzuri kwa kuwa kila walipopita kusikiliza kero za wananchi suala la miundombinu ya barabara lilijitokeza.

“Hatua hii inakwenda kujibu kero za wananchi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika chaguzi za serikali za mitaa, tunaipongeza Tarura imesikia kilio cha WanaDar es Salaam,” amesema Mohamed.

Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge amesema Tarura imesikia kilio cha wakazi wa Dar es Salaam kuhusu miundombinu ya barabara na mchakato wa kuanisha njia hizo ulikuwa shirikishi.

 “Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakiangaliwa ni zile barabara mtambuka ambazo zitawaunganisha wananchi, lakini pamoja na mambo mazuri tungependa kuona uharaka katika utekelezaji wa suala hili,” amesema Mnyonge.