Barabara 17 Kariakoo, Upanga kusukwa kwa lami

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Adolf Ndunguru akibadilishana mkataba wa utekelezaji wa mradi wa DMDP II Mkoa wa Dar es Salaam na Mwakilishi wa Kampuni ya China Wu Yi Co .Limited leo Aprili 11,2025 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Mkataba wa ujenzi wa barabara za Upanga na Kariakoo kupitia awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP II) utagharimu Sh26.06 bilioni na utatekelezwa na Kampuni ya China Wu Yi Co. Limited.
Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa mkataba wa awali wa ujenzi wa barabara kupitia awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP II) ukiwa hatua ya ununuzi ya vifaa, Ofisi ya Rais Tamisemi imeingia makubaliano mapya yatakayohusisha ujenzi wa barabara 17 za Upanga na Kariakoo, zenye urefu wa kilometa 7.38.
Mkataba huo wenye thamani ya Sh26.06 bilioni, umesainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kampuni ya China Wu Yi Co. Limited.
Akizungumza kwenye hafla ya kuingia mikataba hiyo leo Aprili 11, 2025, Mratibu wa Miradi ya DMDP, Humphrey Kanyenye amesema mkataba huo unakuwa wa 18 kati ya mikataba ambayo tayari wamekwishasaini.
“Tuna miradi ambayo ilishaanza tangu Mei 2024 kupitia DMDP na kazi kubwa iliyofanyika tuliona tuanze na manunuzi, kwa sababu miundombinu hiyo ndio imechukua sehemu kubwa ya mradi,” amesema.
Mkataba anaouzungumzia Kanyenye ni wa Km84.24 wenye thamani ya Sh221.85 bilioni ambao ulisainiwa Machi 21, 2024 ukihusisha barabara za Kinondoni, Temeke, Kigamboni, Ubungo na Dar es Salaam CC.
Kuhusu kilometa 7.38 zitakazojengwa na kampuni ya Wu Yi, kwa Kata ya Upanga Kanyenye amesema utahusisha barabara za Undali, Senegal, Nyangoro, Mtitu, Maweni, Mathudaras, Kiwanuka 2, Kitonga, Kalenga, Isevya na Bwera zenye urefu wa kilometa 4.63.
Kwa upande wa Kariakoo, barabara zitakazohusika ni Viwandani, Somali Kipande, Lindi 1, City Garden, Songea 3 na Kilwa 2, zote zikiwa na urefu wa km 2.75.
Kanyenye amesema mwaka jana walisaini mikataba minane ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 63.66 kwa gharama ya Sh190 bilioni, na ukasailia mkataba mmoja ambao waliacha kuangalia uwezo wa mkandarasi.
“Mkataba huu haukusainiwa mapema ili kujiridhisha na uwezo wa mkandarasi na sasa tumejiridhisha na uwezo wake hivyo tayari ataanza utekelezaji wa mradi huu,” amesema.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila amesema mkoa huo, una changamoto ya barabara, hivyo mradi huo unakwenda kuondoa kero iliyopo.
Amesema kwa mvua za mwaka jana barabara nyingi ziliibua kero, hivyo sasa utekelezaji wa mkataba utakwenda kuwa faraja kwa wananchi.
“Wakazi wa Dar es Salaam wameanza kufanya biashara kwa saa 24, ujenzi wa miundombinu ni muhimu sana kuchochea uchumi wa mkoa kwa sababu taa zitakwenda kujengwa kila mahali pamoja na miundombinu mingine,” amesema.
Mwakilishi wa Meya wa Manispaa ya Ilala, Saady Kimji amesema ujenzi wa miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam utakwenda kuongeza ufanisi hasa kupunguza foleni na kero za maji wakati wa mvua.
Mradi wa DMDP kwa ujumla unagharimu Sh1 trilioni fedha ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, ambapo wakandarasi 18 wameingia mikataba kujenga barabara zenye urefu wa km155.28.
Samson Juma, mfanyabiashara Kariakoo amesema uchafuzi wa mazingira na kusambaa majitaka ni kero inayowasumbua wafanyabiashara wengi Mtaa wa Lindi, hivyo uboreshaji wa miundombinu kwao utaleta ahueni.
“Maji ya chemba kufunguliwa na kutiririka hovyo n tatizo sugu hali hii inahatarisha afya zatu na kusababisha maradhi ya mlipuko, ni vyema kama Serikali inakuja na mradi huo wa DMDP tunaamini utatuondolea kero,” amesema.
Hali kama hiyo ipo upande wa Upanga ambapo Aisha Amir, mkazi wa eneo Muhimbili amesema kutokana na shughuli za biashara na ongezeko la watu usimamizi wa taka ni changamoto.
Awamu ya pili ya DMDP itaboresha barabara za kiwango cha lami jijini Dar es Salaam, ujenzi wa madampo ya kisasa yatakayohifadhi taka kwa ufanisi, ujenzi wa masoko, mifereji na vituo vya mabasi.