Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Sefue, Nape watakavyomkumbukwa Msusa, ubingwa wa Arsenal…

Muktasari:

  • Uongozi, heshima kwa wote na moyo wa kusaidia, ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuwa kumbukumbu za milele za maisha ya Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue amemtaja Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), marehemu Leonard Mususa kuwa mtu aliyeheshimu, kupenda na kuwajali wengine.

Wakati Balozi Sefue akimkumbuka kwa hayo, Patrick ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mususa ametaja kumbukumbu za mwisho kabla ya kifo cha baba yake, jinsi alivyofurahia ushindi wa Arsenal iliyochukua Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza.

Mususa, alifariki dunia Mei 30, mwaka huu na maziko yake yanatarajiwa kufanyika kesho Jumanne Juni 2, 2026 katika makaburi ya Kondo jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), marehemu Leonard Mususa. Picha na Michael Matemanga.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Masaki jijini Dar es Salaam, Balozi Sefue amesema kabla ya kufanya kazi naye katika Tume ya Rais ya Maboresho ya Mifumo ya Kikodi, alifahamiana na Mususa kifamilia.

Wakiwa katika tume hiyo, amesema Mususa hatasahaulika kwa uzito wa hoja na mawazo yake kuhusu mageuzi ya mifumo ya kikodi nchini na uwezo wa kusikiliza wengine kwa umakini na usawa bila kujali hadhi zao na yake.

“Alikuwa mtu mkubwa kwenye hii nchi, lakini usingedhani ni mtu mwenye hadhi hiyo kwa sababu alimpa nafasi yeyote kumsikiliza na kuzungumza naye na alitoa fursa hiyo kwa usawa,” amesema.

Nje ya kazi, Balozi Sefue amemtaja Mususa kuwa mtu aliyejali wengine na mwepesi wa kusaidia kama ingetokea kuna aliyepata shida na akamwambia.

Waombolezaji wakiwa katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), marehemu Leonard Mususa, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga.

“Ungekuwa na shida na ukamwambia Mususa, asingeacha kukusaidia, ni mtu ambaye kwa kweli hakupenda kuona mwingine akiteseka wakati ana uwezo wa kumsaidia,” amesema.

Ameeleza Mususa aliheshimu watu wengine bila kujali sifa zake na aliwapenda.


Kuhusu Arsenal

Kwa upande wa mtoto wa kwanza wa Mususa, Patrick amesema miongoni mwa matendo ya mwisho ya baba yake anayoyakumbuka ni namna alivyofurahia ushindi wa Arsenal.

Amesimulia baba yake alipostaafu uenyekiti wa bodi ya MCL moja ya zawadi alizopewa ni picha aliyochorwa akiwa amevalia jezi ya klabu ya Arsenal.

Baada ya klabu hiyo kushinda ligi kuu ya Uingereza, Patrick amesema baba yake aliwaambia hatimaye picha hiyo imekuwa na maana na imesema ukweli.

“Siku Arsenal wameshinda Ligi Kuu ya Uingereza, akatwambia sasa hii picha ina maana, sasa nitasherehekea. Ni vitu vizuri tulivyoviona siku chache kabla hajaenda kwa Mungu,” amesema.

Mengine anayoyakumbuka, amesema ni namna walivyokuwa pamoja kwa takriban siku chache kwenye matukio mbalimbali ikiwemo msiba wa mmoja wa ndugu yao Mlandizi mkoani Pwani.

“Tulikwenda kuzika na kula pamoja na mzee alikuwa mtu wa namna hiyo. Anapenda kuhudhuria katika shughuli zote za kijamii na kuwatia watu moyo na kucheka nao,” amesema.

Paredi la ubingwa wa Arsenal likikatiza katikati mwa Jiji la London jana Mei 31, 2026.

Amemtaja Mususa nje ya maisha ya kazi alikuwa mzazi wa wengi kwa kuwa aliwapokea.

“Katika ukuaji wetu tumefikiwa na kina kaka na dada wengi sana ambao waliishi na sisi mzee mlango wake ulikuwa wazi saa zote kupokea ndugu na jamaa ambao wanahitaji msaada na hata sehemu ya kujihifadhi,” amesema.

Ameeleza baba yake alijenga maisha ya watu wengi na mitazamo yake iliwafunza mengi nje ya darasa. Ameeleza kuna wakati alifanya mambo magumu lakini yakafanikiwa.

“Alikuwa na uwezo wa kupunguza makali na uzito wa mambo kwa kutafakari tu. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili changamoto za maisha kwa namna rahisi,” amesema.

Ameeleza Mususa ndiye aliyewasomesha wanawe wote wawili katika shule nzuri na alifanya hivyo hata kwa wasio wanawe na alilea vipaji.

Ndugu na jamaa wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Leonard Mususa, baada ya mwili kuwasili nyumbani kwake jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga.

Patrick, amesema walijifunza vipaji vya uongozi kutoka kwa baba yao, akisema kila mafanikio waliyoyaona kutoka kwake, yaliwashawishi kufuata nyayo zake.

“Tulianza kumuangalia na kumfuatilia anavyokwenda, haikuwa rahisi kwa sababu mara nyingi tulijiuliza anawezaje na yeye ukimuuliza anacheka anakwambia utaweza,” amesema.

Ameeleza amefariki akiacha watoto wawili, wajukuu wanne na mke.


Nape, Mchechu watakavyomkumbuka

Akizungumza msibani hapo, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema alikuwa mithili ya mzazi kwake, akikumbusha walivyofanya naye kazi Mususa akiwa MCL na yeye akiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Amesema walifanya kazi katika utungaji wa sheria na kanuni mbalimbali na alichangia pakubwa hasa kushauri utungwaji wa Sheria ya Huduma za Habari iliyopo sasa.

“Kama mnakumbuka wakati ule sera ya habari ilitaka vyombo vya habari nchi hii vimilikiwe kwa asilimia 51 na wazawa, jambo hili kwa MCL lilikuwa tatizo. Mimi na mzee Mususa tulitengeneza utaratibu ambao MCL iliendelea kufanya kazi,” amesema.

Ameeleza anamkumbuka kwa uelewa, ustaarabu na alikuwa miongoni mwa watu wenye akili kwenye Taifa na alijua namna ya kupata majawabu ya changamoto zilipojitokeza.

Nape, amesema mara ya mwisho waliwasiliana na Mususa wakati anaondoka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya MCL na pia, walijadili kuhusu uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema alimjua Mususa akiwa PwC, yeye akiwa Stanchat na walifanya kazi katika jengo moja.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), marehemu Leonard Mususa. Picha na Michael Matemanga.

Baadaye, amesema walifanya kazi katika maeneo mbalimbali ndani ya Serikali na sekta binafsi ikiwemo kuanzisha CEO Roundtable.

Amesema ameshiriki naye katika uwekezaji wa Legacy Capital Partners, Mususa akiwa mwenyekiti na alichukua nafasi hiyo baada ya Ali Mufuruki kufariki dunia.

“Ni mtu aliyekuwa na maono, misimamo na maadili. Katika uwekezaji tulifikiri alipofariki Mufuruki tungeyumba, lakini Mususa alikuja mambo yakaenda sawa,” amesema.

Ameeleza wamefanya kazi ngumu ikiwemo katika kikosi cha kufikiria utatuzi wa changamoto ya uhaba wa dola, Mususa alikuwa mjumbe.