Balozi Kusiluka: Niliwasiliana na Mususa siku moja kabla ya kifo chake
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka akizungumza katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa.
Muktasari:
- Mususa alifariki dunia Jumamosi Mei 30, 2026 na atazikwa leo, Juni 2, 2026 katika makaburi ya Kondo jijini Dar wa Salaam.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka amesema siku moja kabla ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa (72), waliwasiliana na alimwahidi jambo.
Mususa alifariki dunia Jumamosi ya Mei 30, 2026 na atazikwa leo Jumanne, Juni 2, 2026 katika makaburi ya Kondo jijini Dar wa Salaam.
Baada ya misa kumalizika katika Kanisa la St Peters Oysterbay jijini Dar es Salaam, waombolezaji mbalimbali wamepata wasaa wa kutoa salamu za rambirambi na kumwelezea Mususa walivyomfahamu na mchango wake kwenye jamii na Taifa.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali, Balozi Kusiluka, amesema siku chache kabla ya kifo cha Mususa waliwasiliana kuhusu jambo fulani.
Amesema Mususa alimtumia taarifa ya jinsi Ugiriki ilivyofanikiwa kiuchumi huku akimsihi waharakishe utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya kutathimini mifumo ya kodi ambayo Mususa alikuwa mjumbe wake.
"Nikamjibu kwamba nitakuteua kuwa mwenyekiti wa kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya tume, lakini kwa bahati mbaya kabla hilo halijatokea, ametuaga," amesema.
Mbali na hilo, Balozi Kusiluka amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kutokana na msiba huo.
Balozi Kusiluka, amesema alimfahamu Mususa miaka 15 iliyopita akijiunga kutoka chuoni wakati huo tayari Mususa alikuwa kiongozi ndani ya Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa mahesabu na Ushauri (PwC).
Amesema alikuwa mtu wa kwanza wa viwango vya juu na alimsaidia katika kujiandaa kwa maisha ya kitaaluma na amemfunza mengi kwenye maisha.
Amesema Mususa aliombwa na Serikali kufanya kazi nyingi ikiwemo tume ya kutathimini mifumo ya kodi, kamati ya kuangalia uhaba wa dola na mjumbe wa kamati ya kuangalia jinsi ya kusimamia ndege za Serikali.
"Nilipata bahati ya kumsimamia mtu ambaye alikuwa kiongozi wangu. Ilikuwa si kumsimamia kwa sababu kila alichofanya kilikuwa sahihi. Alikuwa anasoma sana na wiki iliyopita alisoma taarifa fulani ya Botswana tulibishana sana na tunakubaliana," amesema.
Kesho yake, amesema alimtumia taarifa jinsi Ugiriki ilivyonufaika kutoka kwenye hali ngumu ya kiuchumi.
Amesema alimjibu kuwa atamteua kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya kutathimini masuala ya kodi lakini amefariki dunia.
Akitoa salamu za familia, Patrick ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mususa, amesema baba yake asingeweza kushiriki kuandika historia yake mwenyewe kwa kuwa alishirikiana na wengi katika mengi.
Amesema familia inajivunia kuwa na watu wengi waliosimama nyumba yao baada ya msiba wa Mususa, hilo linawathibitishia kuwa aliishi vema na wengine.
Mwakilishi wa sekta binafsi, Paul Makanza amesema walikuwa karibu na Mususa katika kazi mbalimbali na kuna wakati walimwomba awe mwenyekiti wao.
"Tulipomuomba awe mwenyekiti wetu Mususa alikataa, akatwambia haiwezekani vijana wote hawa msiwape nafasi mkanipe mimi. Hiyo inathibitisha alivyopenda kulea vipaji," amesema.
Huyu ndiye Mususa
Mususa alifahamika zaidi ya taaluma yake ya uhasibu na anatajwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Akizaliwa Septemba 25, mwaka 1953 katika visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza, eneo ambalo alipata elimu yake ya msingi na baadaye kujiunga na katika Shule ya Sekondari Kibaha.
Mususa ambaye ni mtoto wa pili kati ya saba wa wazazi wake, alisoma Chuo Kikuu nchini Uingereza na alipomaliza alipata nafasi ya kuwa Mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa takriban mwaka mmoja.
Baadaye, akahamia katika Kampuni ya Ukaguzi ya Price House Water Coopers Ltd, ilivyokuwa inawakilisha Afrika Kusini, Uingereza na Tanzania na alistaafu mwaka 2014 baada ya kuhudumu kwa takriban miaka 36.
Pia, Mususa ni mmoja wa waasisi wa CEO Roundtable alihudumu kwa nafasi ya Mwenyekiti wa bodi kwa miaka 10 na aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mifumo ya Kodi akiteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.