Baba adaiwa kumbaka mtoto wake, kumpa ujauzito kisha atoweka

Mtoto (14) anayedaiwa kubakwa na kupewa ujauzito na baba yake akiwa na mama yake mdogo. Picha na Juma Mtanda
Muktasari:
- Tukio hilo linadaiwa kutokea Januari 2024 katika Kijiji cha Vuleni mkoani Morogoro na Jeshi la Polisi limeanza kuchunguza tuhuma hizo.
Morogoro. Miezi sita sasa imepita tangu lilipofanyika tukio la baba kudaiwa kumbaka na kumpa ujauzito mtoto wake (jina limehifadhiwa), jambo ambalo sasa linashughulikiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi.
Januari 2024, baba wa mtoto huyo, Azizi Hussein, mkazi wa Kitongoji cha Mwidu mkoani hapa, anadaiwa alimbaka mtoto wake, nyumbani kwake na kumsababishia ujauzito.
Msichana huyo alikaa na ujauzito huo hadi Machi 2024 ambapo mimba yake iliharibika na wakati huo alifukuzwa nyumbani kwao, akaenda kuishi kwa baba yake mkubwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limekiri kutokea kwa tukio hilo huku likiendelea kumtafuta mtuhumiwa ambaye alitoweka, ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
Tukio lilivyobainika
Kisa cha msichana huyo kiliibuliwa na Kituo cha Taarifa na Maarifa chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Machi 2024, baada ya kusikia taarifa zake, hivyo waliitafuta familia yake na kuwasukuma kwenda kwenye vyombo vya sheria.
Katibu wa kituo hicho katika kata ya Tomondo, Doris Richard amesema uongozi wa kituo hicho baada ya kupata taarifa za tukio hilo walimfuatilia msichana huyo na kupata ukweli.
Doris amesema kituo hicho kilibaini ukatili dhidi ya mtoto huyo siku chache kabla ya mimba yake kuharibika na walichangishana fedha za matibabu, ili kunusuru maisha ya msichana huyo mdogo.
Amesema waliisukuma familia kuripoti tukio hilo kwenye vyombo vya sheria, ndipo alipokwenda kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ili kutoa taarifa kuhusu kitendo alichofanyiwa mtoto huyo.
Akizungumzia hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tomondo, Kornelly Mkombo amesema familia ya Hussein ilifika ofisi za kata hiyo ili ipewe ushauri, lakini yeye aliwaelekeza kwenye Kituo cha Polisi kwa kuwa matukio ya jinai yanatakiwa kuripotiwa huko.
“Kesi za kubakwa huwa zinaripotiwa polisi, sio ofisi ya mtendaji kata, hiyo kesi imeripotiwa huko na inaendelea. Kwangu walifika kupata ushauri na niliwaongoza kituoni,” amesema Mkombo.
Mwathirika asimulia
Akisimulia mkasa huo, mwathirika wa tukio hilo, amesema Januari mosi, 2024, saa 3 usiku, baba yake aliingia chumba cha watoto ambacho alikuwa amelala yeye na kumuamsha akiwa usingizini na kumbaka kwa nguvu na vitisho.
“Niliandaa chakula siku ya tukio na tunakaenda kulala na ilipofika saa 3 usiku, baba aliingia chumbani kwetu moja kwa moja na kuniamsha, akanieleza nikae naye na nisipokaa naye, mama na mimi tutakufa,” amesema msichana huyo.
Ameongeza kuwa baba yake alimweleza akiendelea kukataa, atawaua wote. Amesema aliendelea kukataa, ndipo baba yake akatumia nguvu kumwingilia hadi kumpa ujauzito.
“Baba aliniingilia kwa kunibaka na nilipata maumivu makali, nikapata ujauzito ambao ulitoka ukiwa na umri wa miezi mitatu. Lilikuwa ni tukio la kulazimishwa lililoambatana na vitisho kuwa nisipolala naye, ataniua mimi na mama. Niliogopa sana, akaniambia nisimwambie mama tendo lililofanyika,” amesema msichana huyo, amesema binti huyo ambaye amehitimu elimu ya msingi mwaka 2023.
Ameiomba jamii, taasisi na mashirika kumsaidia kutoka kijijini hapo ili ajifunze ufundi wa kushona nguo.
Familia yaeleza kusikitishwa
Mama mdogo wa msichana huyo, Aziza Ramadhani amesema msichana huyo alikutwa na ukatili huo mama yake akiwa amesafiri kwa siku kadhaa.
“Ni aibu tumeipata familia na ukoo, namna jamii inavyotutazama kwa ukatili uliofanywa na shemeji yangu, kwa kweli ametuvua nguo kwa kumwingilia mtoto wake wa kumzaa na kumpa ujauzito, ni tukio la aibu kwetu,” amesema Aziza.
Aziza amesema baada ya dada yake, Khadija Ahmad kurudi safari aliona tofauti kwa binti yake, hali iliyomshtua na kuanza kumuuliza maswali ndipo alisema haoni hedhi.
“Baada ya kujua siri imefichuka, Azizi aliandika talaka kumuacha mke wake na kutoroka kusikojulika baada ya kuuza shamba.
Aziza amesema hilo sio tukio la kwanza kwa shemeji yake kuhusishwa na ukatili wa kingono kwani amewahi kudaiwa kumbaka shemeji yake na kumpa ujauzito na mtoto amezaliwa.
Kauli ya Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza tukio la Hussein anayedaiwa kumbaka mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 14 na kumpata ujauzito.
Tukio hilo linadaiwa kutokea mapema Januari 2024 na Jeshi la Polisi limeanza kuchunguza kitendo hicho cha mtuhumiwa kuzini na maharimu wake, jambo ambalo ni kinyume na sheria na maadili ya Kitanzania.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 4, 2024 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema baba huyo amezini na mtoto wake wa kike, kisha kutoroka na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.
“Tayari shauri limefunguliwa Kituo cha Polisi Mikese kwa namba 229/2024 la kuzini na maharimu na upelelezi umeanza,” amesema Kamanda Mkama.