AT. Profesa Nombo ataka kozi za biashara CBE kuyagusa makundi yote
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Profesa Carolyne Nombo akitoa Cheti kwa mmoja wa Taasisi zilizofanikisha mkutano wa kitaaluma wa Chuo Cha Biashara (CBE)
Muktasari:
- Imeshauriwa kozi fupi zinaweza kuwa msaada kwani zitawagusa makundi ya watu wenye nia ya kujifunza ili waweze kufanya biashara na kujipatia kipato.
Dodoma. Serikali ya Tanzania imekiagiza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kuanzisha kozi maalumu za biashara za muda mfupi ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Novemba 12,2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo wakati akifungua mkutano wa sita wa kitaaluma wa kusikiliza matokeo ya tafiti zilizofanywa na wanataaluma kutoka vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.
Profesa Nombo amesema tumaini lao ni kwa CBE kwani kozi zinazofundishwa, nyingi zinawalenga Watanzania kwenye masuala ya ujasiriamali, hivyo ingependeza kama zianze kuwalenga watu wa makundi ya chini.
“Anzisheni kozi maalumu za biashara kwenye mitaala yenu, lakini nawataka mzalishe walimu wa kutosha watakaofundisha masuala ya biashara na ujasiriamali, tayari wenzenu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wameshaanza kutengeneza mpango huo,” amesema Profesa Nombo.
Pia ameagiza Watanzania kuzitumia na kuziamini tafiti zinazofanywa na wasomi kwani zinaweza kuwasaidia katika kuyafikia malengo yao kwa kuwa hakuna utafiti unaopelekwa kwa wananchi kama haujawa na matokeo mazuri, huku akiwasisitiza wasomi waendelee kufanya tafiti zao bila kuchoka.
Ameagiza matokeo ya tafiti kuwekwa katika uelewa mzuri ili yaweze kuwafikia makundi yote ikiwemo watu binafsi, sekta binafsi na kwa watunga sera ili wasaidie wananchi kuendana na mazingira ya sasa hasa kwenye masuala ya kiuchumi.
Awali, Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga amesema chuo hicho kimedahili wanafunzi 23,111 idadi ambayo bado haitoshelezi malengo na akataja sababu ya kuwa na idadi ndogo ni uchache wa matawi ya chuo.
Profesa Lwoga amesema kuanzia Januari 2026 wanakwenda kuanzisha kampasi nyingine mkoani Kilimanjaro ambapo watakuwa wamezifikia kanda zote tano baada ya kuwa na vyuo katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya.
“Chuo chetu tumeendelea kufanya vizuri na tunaamini tutafanya zaidi hasa wakati huu ambao tumeingia kwenye miradi mikubwa, tulikuwa nafasi ya nane kwa utoaji wa huduma bora kati ya vyuo vyote nchini, sasa tunalenga kuwa katika nafasi tatu za juu,” amesema Profesa Lwoga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha CBE, Profesa Zacharia Mganilwa ameomba Wizara ya Elimu kuanzisha mpango maalumu wa kuwa na mikutano ya kitaaluma kwa vyuo vyote nchini.