Askofu Novatus Rugambwa afariki dunia Roma
Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa, Mtanzania aliyewahi kuhudumu kama Balozi wa Baba Mtakatifu katika nchi mbalimbali duniani amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu huko Roma, Italia.
Taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Jovitus Mwijage kwenda kwa maaskofu, mapadri, watawa na waamini imesema, Askofu Mkuu Rugambwa amefariki dunia usiku wa Septemba 16, 2025 akiwa Roma.
Askofu huyo alizaliwa Oktoba 8, 1957 mkoani Kagera na kuwekwa wakfu katika daraja takatifu ya upadri Julai 6, 1986 na Askofu Nestorius Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba (wakati huo).
Baada ya miaka kadhaa ya huduma, Machi 18, 2010 aliwekwa wakfu katika daraja takatifu ya Uaskofu na Kardinali Tarcisio Pietro Evasio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican.
Katika safari yake ya utumishi, Askofu Rugambwa aliwahi kuteuliwa Balozi wa Baba Mtakatifu katika nchi mbalimbali ikiwamo Angola, Honduras na visiwa vya Fiji, ambapo alitambulika kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa Vatican na mataifa hayo.
Wasifu wa Askofu Rugambwa
Askofu Mkuu Novatus Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, 1957, katika Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa mtandao wa Vatican, baada ya masomo na majiundo ya kikasisi, akapewa daraja takatifu ya upadre mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.
Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican Julai mosi, 1991.
Baada ya kufanya kazi mbalimbali katika balozi za Vatican, Juni 28, 2007 Papa Benedikto wa XVI alimteua kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalumu.
Februari 6, 2010, Papa Benedikto XVI, alimteua kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican kwa wakati huo, Machi 18, 2010.
Machi 5, 2015 aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras. Machi 29, 2019, Papa Francisko alimteua kuwa Balozi wa Vatican nchini New Zealand na mwakilishi wa kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific.
Machi 30, 2021, Papa Francisko alimwongezea majukumu kwa kumteua kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific.
Wakati huohuo aliendelea kuwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga. Pia Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, Palau na Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific.
Endelea kufuatilia Mwananchi