Askari wanyamapori waonywa kunyanyasa wananchi

Kamishna wa Huduma za ulinzi wa wanyamapori, Kamishna msaidizi wa uhifadhi Saidi Kabanda akimvisha cheo kipya mmoja wa askari wa uhifadhi wa wanyamapori, Ofisa wanyamapori daraja la kwanza Omar Mpita mjini Bunda leo. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Askari wa uhifadhiwanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) Kanda ya Ziwa wametakiwa kutokutumia vyeo vyao kunyanyasa wananchi, badala yake vyeo hivyo vitumike kuongeza ufanisi katika majukumu yao.
S:
Beldina Nyakeke, Mwananchi
Bunda. Askari wa uhifadhi wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) Kanda ya Ziwa wametakiwa kutokutumia vyeo vyao kunyanyasa wananchi badala yake vyeo hivyo vitumike kuongeza ufanisi katika majukumu yao.
Wito huo umetolewa leo Desemba 1, 2022 mjini hapa na Kamanda wa Uhifadhi Tawa kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Gisela Kimario katika hafla ya kuwavisha vyeo vipya askari 26 wa kanda hiyo.
Amesema kuwa kanda hiyo yenye mapori ya akiba manne inakabiliwa na chagamoto kadhaa ikiwemo ujangili wa nyama, uchungaji wa mifugo ndani ya mapori hayo pamoja na ukataji wa miti na kwamba changamoto hizo zitakomeshwa endapo askari hao watazingatia maadili na taratibu za kazi.
"Ujangili wa nyama ni tatizo kubwa katika mapori yetu lakini askari wetu msitumie vyeo hivi vipya kwa kigezo hicho cha kuwepo kwa tatizo kuwanyanyasa wananchi, tunategema kuona ufanisi zaidi katika utendaji wenu wa kazi," amesema
Amefafanua kuwa zipo njia sahihi zinazotakiwa kutumika katika kukabiliana na changamoto hizo ndani ya hifadhi njia ambazo amesema kuwa zinaheshimu na kutambua utu wa mtu hivyo uongozi wa mamlaka hiyo hautasita kuwachukulia hatua za kinidhamu askari wote watakaobainika kwenda kinyme na maadili na taratibu.
Wakizungumza baada ya kuvishwa vyeo hivyo baadhi ya askari hao wamesema kuwa wanatambua umuhimu wa maadili na uadilifu katika utendaji wao wa kazi hivyo kuahidi kuwa utendaji wao wa kazi utazingatia misingi hiyo.
"Kwenye hii kazi tunakumbana na changamoto nyingi, kwa mfano suala la rushwa unapokamata mifugo iliyoingia kwenye hifadhi, sasa kama askari hautakuwa makini unaweza kujikuta umeingia kwenye mtego," amesema Ofisa wanyamapori daraja la kwanza Omar Mpita.
Mpita amesema kuwa vyeo walivyopata vitasadia kuboresha utendaji wao wa kazi badala ya kuleta taharuki katika jamii na kwamba endapo watalazimika kukamata watu basi ukamataji huo hautatumia nguvu zaidi.
Naye Ofisa mhifadhi daraja la kwanza, Holo Kilongo amesema kuwa utendaji kazi kwa kuzingatia maadili mbali na kuleta sifa kwa askari binafsi lakini pia ni sifa kwa wizara ya maliaasili na taifa kwa ujumla.
"Tunalo jukumu kubwa la kulinda rasilimali za wanyamapori lakini jukumu hili halitakuwa na maana kama taswira ya taasisi yetu, wizara na nchi kwa ujumla itachafuka kwa vitendo vyetu viovu kwahiyo sisi tunaahidi utendaji kazi mzuri wa kuzingatia maadili," amesema.