Asilimia 30 ya wafanyakazi wanapitia manyanyaso kazini

Muktasari:
- Ripoti ya haki za binadamu na biashara iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imeonyesha kuwepo kwa unyanyasaji kazini kwa asilimia 30.
Dar es Salaam. Uonevu na vitisho kwa wafanyakazi wa ofisini vimetajwa kuongoza katika manyanyaso sehemu ya kazi, ripoti ya haki za binadamu na Biashara ya nane iliyozinduliwa leo Julai 29, 2021 na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) imeeleza.
Utafiti huo unaonyesha kuwa kati ya asilimia 29 ya wafanyakazi waliokiri kuwepo kwa manyanyaso kazini, asilimia 73 wametaja vitisho, kubezwa na manyanyaso mengineyo, huku asilimia 15 wakikiri kunyanyaswa kingono.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo kupitia mtanmdao wa Zoom, Ofisa Mwandamizi a Kitengo cha Utafiti, Fundikila Wazambi amesema katika utafiti huo wafanyakazi 3 kati ya 10 walikiri kuwepo kwa ukatili katika maeneo yao ya kazi licha ya uelewa kuhusiana na ukatili kuwa mdogo.
“Asilimia kubwa ya ukatili mahali pa kazi inaonekana kuwa ni vitisho na uonevu kwa asilimia 73 ikifuatiwa na vitendo vya kingono kwa asilimia 15,” amesema Wazambi.
Amesema malalamiko mengi ya unyanyasaji wa kingono yalitolewa zaidi na wafanyakazi walio katika sekta ya ukarimu (hoteli na baa), hususan kushikwa shikwa na wateja bila ridhaa, huku mabosi wao wakiwahimiza kuvumilia suala hilo ili wasipoteze wateja.
“Kuna baadhi ya vitendo watu huwa wanafikiria kuwa si vya unyanyasaji ikiwemo mtu kukushika bila ridhaa jambo hili kuwa ni moja ya vitendo vya unyanyasaji,” amesema Wazambia
Amesema mwaka 2019 Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilitunga mkataba wa ukatili na mahali pa kazi hivyo wanatoa rai kwa Serikali kuuridhia na kuutungia Sheria ili uwe moja ya Sheria za nchi.
Katika hatua nyingine, MKurugenzi wa LHRC, Anna Henga anasema ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 41 ya wafanyakazi hawana mikataba ya ajira katika sehemu wanazofanyia kazi.
“Asilimia 59 walisema kwamba wana mikataba ya ajira,” amesema Henga.
Hata hivyo, kuhusiana na mikataba ya maandishi, ni asilimia 56 pekee ya wafanyakazi walidai kuwa na aina hiyo ya mkataba, sawa na punguzo la asilimia 19 ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 2019.