Anayedaiwa kuwachapa fimbo wanafunzi wa madrasa kortini

Muktasari:
- Musa anadaiwa kutenda makosa hayo Februari 9, 2025, katika msikiti wa Sunna Kiburugwa, wilayani Temeke, ambapo aliwapiga fimbo kwa ukatili watoto wawili.
Dar es Salaam. Mwalimu wa Madrasa, Musa Bashiru Musa (24), ambaye kipande cha picha jongefu (video) kilisambaa katika mitandao ya kijamii kikimuonyesha akishambulia wanafunzi wake kwa kuwacharaza viboko mikononi na matakoni, amepandishwa kizimbani kujibu tuhuma zake.
Musa, mkazi wa Mbagala Kiburugwa, jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kusomewa mashtaka mawili ya kuwafanyia ukatili watoto wawili wa madrasa.
Mwalimu huyo, aliyekuwa amevalia kanzu rangi ya bluu, amefikishwa Mahakamani hapo leo, Jumatano, Februari 19, 2025, na kusomewa kesi ya Jinai namba 4344 ya mwaka 2025.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Rabia Ramadhani, akisaidiana na Nicas Kihemba, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Vick Mwaikambo.
Wakili Rabia amedai mshtakiwa alitenda makosa hayo kinyume na kifungu 169A (1) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Mshtakiwa Musa Bashiri Musa (mwenye kanzu) akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu, akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, baada ya kusomewa mashtaka mawili ya kuwafanyia ukatili watoto wadogo. Aliyevaa suti ni wakili wake, Arafat Kanzweba. Picha na Hadija Jumanne
Akimsomea mashtaka, alidai katika shtaka la kwanza, Februari 9, 2025, katika msikiti wa Sunna uliopo Kiburugwa, wilaya ya Temeke, akiwa mwalimu wa Madrasa na akiwa anamsimamia mwanafunzi mwenye umri wa miaka sita, alimpiga kwa kutumia fimbo.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumpiga kwa ukatili mwanafunzi huyo wa kike sehemu ya mikononi (viganjani) kwa kutumia fimbo na hivyo kumsababishia madhara makubwa.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, anadaiwa alimpiga fimbo binti mwenye umri wa miaka 9, ambaye ni mwanafunzi.
Inadaiwa kuwa Musa alimpiga kwa ukatili mwanafunzi huyo sehemu ya mikononi kwa kutumia fimbo, hivyo kumsababishia madhara makubwa.
Baada ya kusomewa mashtaka yake, alikana kutenda makosa hayo, na upande wa mashtaka ulidai upelelezi hujakamilika.
Hata hivyo, wakili wa mshtakiwa huyo, Arafat Kanzweba, aliomba mteja wake apewe dhamana kutokana na mashtaka yanayomkabili yana dhamana.

Mshtakiwa Musa Bashiri Musa (mwenye kanzu) akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu, akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, baada ya kusomewa mashtaka mawili ya kuwafanyia ukatili watoto wadogo. Aliyevaa suti ni wakili wake, Arafat Kanzweba. Picha na Hadija Jumanne
Hakimu Mwaikambo aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika kwa wakati na kisha kutoa masharti matatu ya dhamana kwa mshtakiwa huyo.
"Upande wa mashtaka, naomba mkalimilishe kwa haraka upelelezi wa kesi hii, ili iendelee na hatua nyingine," amesema Hakimu Mwaikambo.
Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mwaikambo amesema mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za mitaa.
Pia, wadhamini hao wanatakiwa wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida), pia wasaini bondi ya Sh 3 milioni kila mmoja.
Mshtakiwa amefanikiwa kutimiza masharti na yupo nje kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Machi 25, 2025 itakapotajwa.