Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyeua kwa bisibisi ahukumiwa kunyongwa

Mfanano wa bisibisi inayotajwa kuhusika katika mauaji ya Frazer Chiwiya. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Mauaji hayo yalitokea Aprili 2, 2024 katika eneo la Mwananyamala kwa Sindano, wilayani Kinondoni.

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar Es Salaam, imemhukumu adhabu ya kifo Omary Ng’azi, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua Frazer Chiwiya kwa kumchoma na bisibisi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mauaji hayo yalitokea Aprili 2, 2024 katika eneo la Mwananyamala kwa Sindano, wilayani Kinondoni.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Awamu Mbagwa baada ya kuridhika kwamba mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu kwa kumchoma kwa kutumia kifaa chenye ncha kali.


Ushahidi ulivyokuwa

Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita na vielelezo vitatu, vikifafanya kuwa mauaji hayo yalitokana na mgogoro ulioanza baada ya mshtakiwa kumvamia na kumpora simu shahidi wa kwanza, Paulo Isaac ambaye baadaye aliripoti tukio hilo kwa shemeji yake (Frazer).

Paulo alidai alikuwa amekwenda kumtembelea dada yake na alikwenda dukani kununua voda na akiwa njiani kurudi nyumbani aliwasha tochi ya simu yake.

Alidai alipokuwa akivuka daraja alikutana na mshtakiwa akiwa na watu wengine wakivuta bangi ndipo walimwamuru azime tochi, na alipokataa mshtakiwa alimfuata na kuanza kumshambulia akishirikiana na wenzake na walimwibia simu na kumng’oa jino.

Alidai baada ya kushambuliwa, alikimbilia nyumbani kumjulisha shemeji yake (marehemu kwa sasa) ambaye alikuwa akimfahamu mshtakiwa kwani walikuwa wakiishi mtaa mmoja.

Ilidaiwa Frazer alipoenda kwa mshtakiwa, walimkuta nje ya nyumba yake na kumtaka arejeshe simu waliyomuibia shemeji yake, kisha alimpigia simu mama wa mshatakiwa kumjulisha kuhusu tukio alilokuwa amefanya mwanaye.

Kilichofuata ni mshtakiwa kuingia ndani na kutoka bisibisi, kisha akamchoma nayo Frazer na kukimbia.

 Shahidi huyo wa kwanza alikimbia kwa shahidi wa pili kuomba msaada, wakampeleka aliyeshambuliwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu na kutokana kuvuja damu nyingi mdomoni, puani na kifuani na alipofikishwa alikuwa ameshafariki.

Kufuatia kifo cha Frazer, juhudi za kumtafuta mshtakiwa zilianza ambapo alikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Oysterbay.

Daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alieleza kuwa kifo kilitokana na kupoteza damu nyingi kufuatia jeraha la kuchomwa kifuani.

Aidha, mahakama ilizingatia ushahidi wa shahidi wa kwanza aliyeshuhudia tukio hilo moja kwa moja, akieleza kwa kina namna mshtakiwa alivyotekeleza shambulio hilo, ambao uliungwa mkono na maelezo ya onyo ya mshtakiwa aliyokiri kumchoma marehemu.

Kwa upande wake, mshtakiwa alijitetea kwa kuwa kulikuwa na ugomvi kati yake na marehemu, lakini alikanusha kuhusika na kifo hicho.

Alidai kuwa aligombana na marehemu siku ya tukio akidaiwa kuiba simu na siku iliyofuata akiwa amekwenda kazini, alikamatwa.


Uamuzi wa Mahakama

Jaji Mbagwa amesema baada ya mahakama kupitia ushahidi wa pande zote mbili aliangalia mambo matatu, kama Frazer alikufa kifo kisicho cha kawaida, kama mshtakiwa ndiye alisababisha mauaji hayo na kama alisababisha mauaji kwa nia mbaya.

Katika uchambuzi wake, jaji alieleza kuwa kulikuwa na dalili zote za kuwepo kwa nia ya kufanya mauaji, akizingatia aina ya silaha iliyotumika, sehemu ya mwili iliyolengwa, pamoja na mwenendo wa mshtakiwa kabla na baada ya tukio.

Mahakama ilibaini kuwa mshtakiwa alikusudia kusababisha madhara makubwa au kifo kwa marehemu na kukubaliana na ushahidi wa kitabibu, uliotolewa na ripoti ya daktari na kusisitiza ushahidi huo haukuacha shaka yoyote kuwa Frazer alifariki kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Amesema kuwa ushahidi wa mashahidi pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa ilithibitisha kosa hilo na kuwa mshtakiwa alichukua hatua ya makusudi kwa kuingia ndani na kutoka na bisibisi, kisha kumchoma Frazer sehemu mbalimbali za mwili wake, kitendo kilichoonyesha alidhamiria kusababisha madhara au kifo.

“Kwa kuangalia aina ya silaha iliyotumika, sehemu ya mwili iliyolengwa na mwenendo wa mshtakiwa, ni wazi kwamba alikusudia kusababisha madhara makubwa ya mwili au kifo,” amesema Jaji.

Kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha shtaka la mauaji bila kuacha shaka yoyote.

Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.