Aliyemuua dada yake mjamzito, kumchoma moto na kumzika sasa kunyongwa

Muktasari:
- Mahakama ya Rufani Tanzania imeidhinisha adhabu ya kifo kwa Mayunga Mwenelwa, aliyemuua dada yake na kumzika.
Mwanza. Mahakama ya Rufani Tanzania, imebariki adhabu ya kifo aliyopewa mkazi wa Kijiji cha Mangulua Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Mayunga Mwenelwa, aliyemuua kikatili dada yake, Nyazala Mwenelwa kisha kumzika.
Viongozi wa kijiji pamoja na ndugu wa marehemu walipombana Mayunga, kwanza alisema katika shimo hilo alikuwa ameua mbwa na kumzika, lakini baada ya kubanwa zaidi ndipo alipokiri kumuua mdogo wake na kumzika katika shimo hilo.
Jopo la majaji watatu wa mahakama ya Rufani walioketi jijini Mwanza kusikiliza rufaa ya Mayunga ambaye awali alihukumiwa kunyongwa hadi kufa Julai 26,2020 na Jaji Fredrick Manyanda, waliitupa rufaa hiyo na kubariki adhabu hiyo ya kifo.
Katika hukumu yao waliyoitoa Julai 19, 2024, majaji Lugano Mwandambo, Lilian Mashaka na Gerson Mdemu, wamesema kesi ya upande wa Jamhuri ilithibitishwa kwa viwango vinavyokubalika na hawana shaka shitaka hilo lilithibitishwa.
Namna mwili ulivyogundulika
Kulingana na ushahidi wa Jamhuri, Nyanzala Mwenelwa alitoweka ghafla Julai 18,2015 na mwili wake kupatikana Julai 30,2015 ukiwa umezikwa katika shimo lililopo jirani na muuaji huyo, ambapo alikamatwa na kushitakiwa kwa mauaji.
Ilielezwa Julai 18,2015, kaka mwingine wa marehemu aitwaye Jombele Mwenelwa aliyekuwa akimwagilia bustani yake, alimuona marehemu akiwa amebeba mfuko wa sandarusi akienda shambani kwake kuvuna viazi.
Baada ya kumaliza kumwagilia bustani, Jombele ambaye alikuwa shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, aliondoka kuelekea Kijiji cha Jojilo, huku nyuma akimwacha mdogo wake huyo wa kike akiendelea na shughuli ya kuvuna viazi.
Aliporudi, mtoto wa kiume wa marehemu aitwaye Kinda Emmanuel, alimjulisha shahidi huyo alikuwa hamuoni mama yake na alikuwa akimtafuta, wawili hao wakaamua kwenda shambani na kukuta mfuko na ndoo iliyojaa viazi na jembe.
Walianza kumtafuta na kuulizia pia kwa ndugu wengine bila mafanikio ambapo waliamua kumpa taarifa mumewe aitwaye Malimi Koroboi aliyekuwa shahidi wa nne. Mumewe alirejea nyumbani na kuitisha kikao cha familia kujadili suala hilo.
Pia walimjulisha mwenyekiti wa kitongoji, Shilala Lyagamana aliyekuwa shahidi wa 2 na siku iliyofuata ambayo ni Julai 21, 2015, kiongozi wa usalama kijijini hapo alitoa taarifa kijijini na wanakijiji waliitikia na kuanza kumtafuta marehemu.
Hata hivyo, kazi ya kumtafuta marehemu haikuzaa matunda, kwani viongozi wa Kijiji waliwaelekeza ndugu wa marehemu ndio waendelee na shughuli ya kumtafuta marehemu wakati wao wakiendelea kufanya uchunguzi wa siri.
Julai 30, viongozi wa vijiji wakiwamo baadhi ya ndugu walimshuku Mayunga baada ya kubaini ameacha kumtafuta mdogo wake, ambapo katika uchunguzi wao wa siri waligundua uwepo wa shimo jipya lililokuwa jirani na nyumba ya mshitakiwa.
Mara baada ya shimo kugunduliwa, mshitakiwa alitoweka kijijini na alipotafutwa na kuulizwa, alijibu kuwa alikuwa ameua mbwa na kumtupa katika shimo hilo lakini alipobanwa zaidi alikiri kumuua marehemu na kumzika katika shimo hilo.
Mshitakiwa huyo akawaongoza viongozi wa kijiji na ndugu katika shimo hilo nje ya nyumba yake na walipoanza kufukua walikutana na mifupa ya binadamu ambapo waliacha kuendelea na kazi hiyo na kutoa taarifa polisi ambao walifika.
Polisi walifika wakiwa na daktari na kukuta tayari mshitakiwa yuko chini ya ulinzi wa viongozi wa vijiji na wananchi na kazi ya kuchimba iliendelea, ambapo walipata fuvu na mifupa ya mwanadamu ambapo mwili wake ulikuwa umeanza kuharibika.
Pia ndani ya shimo hilo walikuta kisu na baadhi ya nyama za mwanadamu zilizochomwa ambapo ndugu waliweza kumtambua marehemu kutokana na mabaki ya nguo alizokuwa amevaa siku ya mwisho kabla ya kutoweka kwake.
Mbali na nguo, lakini walithibitisha ni yeye kutokana na nywele alizokuwa amesuka siku hiyo ambazo hazikuwa zimeungua na kuthibitisha ni marehemu na alipohojiwa polisi mbele ya ndugu zake, alikiri kufanya mauaji hayo.
Polisi walimchukua maelezo ya onyo ambayo katika maelezo hayo alikiri kufanya mauaji na baadaye alipelekwa kwa mlinzi wa amani, ambako napo ilielezwa aliungama kumuua mdogo wake na yalipokelewa kama kielelezo.
Alivyojitetea kortini
Katika utetezi wake, mshitakiwa huyo alipinga ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri na kueleza kuwa aliamua kukiri kufanya mauaji baada ya mwili kugunduliwa, kwa sababu kundi kubwa la wananchi na baadhi ya ndugu walianza kumpiga.
Alijitetea kuwa wakati akihojiwa polisi, alikanusha kumuua marehemu lakini polisi waliamua kumpiga na ili kuokoa maisha yake, aliamua kukiri kutenda kosa hilo.
Kutokana na ushahidi huo wa mashahidi 8 wa Jamhuri na vielelezo 4, Mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kunyongwa hadi kufa, lakini akatata rufaa mahakama ya rufani Tanzania akiegemea katika hoja sita akitaka aachiliwe huru.
Hoja za rufaa zilivyokuwa
Miongoni mwa hoja alizowasilisha mahakamani kupinga adhabu hiyo ya kifo ni pamoja na kwamba Jaji alikosea kisheria kwa kumtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo, kwa kuegemea ushahidi wa mazingira na hakuna aliyeshuhudia.
Pia akaeleza kuwa Jaji alikosea kumtia hatiani na kumhukumu kwa kuegemea maelezo ya kukiri kosa, wakati maelezo hayo hayakuwa na maelezo ya kutosha kuweza kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya kukusudia ambalo adhabu ni kifo.
Halikadhalika akajenga hoja kuwa Jaji alikosea kisheria kumtia hatiani na kumpa adhabu ya kifo kwa kuegemea maelezo ya ungamo kwa mlinzi wa amani, wakati sheria inataka maelezo hayo yawe yameungwa mkono na ushahidi huru.
Mbali na hoja hizo, alisema Jaji alikosea kumtia hatiani kwa vile hapakuwepo ushahidi wa kisayansi kuthibitisha kuwa mabaki yale yaliyokutwa kwenye shimo yalikuwa ni ya Nyanzala Mwenelwa kwa kuwa hakuna aliyeshuhudia mauaji hayo.
Pia alijenga hoja kuwa maelezo yake ya onyo aliyoyaandika polisi, aliyaandika akiwa hayuko huru hivyo yalistahili kuondolewa katika mwenendo wa kesi na pia Jaji alikosea kufanyia kazi ushahidi dhaifu wa Jamhuri na wenye mashaka.
Hukumu ya majaji
Hata hivyo, baada ya majaji kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, walikubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu Mwanza iliyompa adhabu ya kifo wakisema hata maelezo ya ungamo kwa mlinzi wa amani hayakupingwa kortini.
“Tunakubaliana na uchambuzi wa kielelezo namba p4 uliofanywa na Jaji aliyesikiliza kesi kuwa mrufani hakuwa amepigwa au kutishiwa maisha yake akiwa mbele ya mlinzi wa amani. Alikuwa huru na alihiyari mwenyewe kueleza,” wamesema.
“Hoja kuwa maelezo hayo hayakuungwa mkono na mashahidi huru hayana msingi na yamekuja kama njia tu ya kujinasua. Maelezo hayo yalimhusisha na kosa na yalitoka kwenye kinywa chake chake mwenyewe,” wamesisitiza majaji hao.
Kuhusu maelezo ya onyo yaliyoandikwa Polisi, majaji walisema hakuna ubishi Jaji aliegemea katika maelezo hayo pia kumtia hatiani mrufani na kusema kulingana na kumbukumbu za mahakama, alikiri kwa mdomo na kwa maandishi.
“Alikiri katika eneo la tukio, akakiri akiwa kituo cha Polisi Ngudu na akakiri mbele ya mlinzi wa amani katika mahakama ya mwanzo Ngudu. Hoja ya kutopokelewa maelezo hayo ilishughulikiwa na mahakama na kutupwa,” wameeleza.
Katika hoja nyingine, majaji wamesema ni jambo lisilobishaniwa kuwa hakuna shahidi hata mmoja aliyeshuhudia mauaji na kwamba kutiwa kwake hatiani kuliegemea ushahidi wa mazingira na maelezo yake ya kukiri kutenda kosa.
Majaji wamesema ilikuwa sahihi kwa mahakama kuamini ushahidi wa mashahidi namba 1,2,3,4 na 6 na mrufani mwenyewe na haukuacha shaka kuwa Nyanzala Mwenelewa alikuwa ameuawa na kifo chake hakikuwa cha kawaida.
Wamesema kunaweza kuwa na mabishano kuwa hapakuwepo ushahidi wa kisayansi kuthibitisha utambuzi wa mabaki ya mwili kama ni ya marehemu lakini shahidi wa kwanza na wa nne walimtambua marehemu kutokana na mtindo wa nywele aliosuka.
Pia mwili wake ulitambuliwa kupitia aina ya nguo alizoonekana amezivaa mara ya mwisho, alikuwa na ujauzito wa miezi nane na ushahidi wa shahidi wa tano, ulionyesha kitovu na kondo kilipatikana kuthibitisha kweli alikuwa mjamzito.
Majaji hao wamesema kwa kuchambua ushahidi wote kwa ujumla wake na maelezo ya kukiri kosa, unaonyesha kisu kilitumika kuondoa uhai wa marehemu na katika ushahidi, kulipatikana kisu eneo la tukio ambako mwili ulipatikana.
Kutokana na ushahidi huo, mahakama ya rufani imeona hakuna sababu ya kubatilisha hukumu ya mahakama kuu iliyomtia hatiani na kumhukumu mshitakiwa adhabu ya kifo na kubariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa.