Aliyekuwa kocha wa makipa Simba na wenzake waendelea kusota gerezani

Muktasari:
- Kesi inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa klabu ya soka ya Simba, Mwalami Sultan na wenzake watano wanaendelea kusota gerezani huku upelelezi ukiwa bado haujakamilika.
Dar wa Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa kocha wa makipa wa klabu ya soka ya Simba, Mwalami Sultan na wenzake watano umedai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina heroin zenye uzito wa kilo 34.89.
Wakili wa Serikali, Caroline Matemu alidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini upelelezi bado haujakamilika.
"Upelelezi haujakamilika naiomba mahakama hii ihairishe shauri hili kwa ajili ya kutajwa,"alidai Matemu
Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi aliahirisha shauri hilo hadi Machi 16, 2023 kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Sultan washitakiwa wengine ni Mmiliki wa Kituo cha Soka cha Kambiasso Sports Academy, Kambi Seif, Maulid Mzungu, Said Matwiko, John John na Saraha Eliud.
Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 huko katika eneo la Kivule lililopo ndani ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakisafirisha kilo 27.10 za dawa za kulevya aina ya herione.
Pia inadaiwa kuwa Novemba 4, 2022 huko Kamegele katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani washitakiwa walikutwa wakisafirisha kilo 7.79 za dawa za kulevya aina ya heroine.