Ahukumiwa miaka 20 jela kwa kumiliki fisi kinyume cha sheria

Muktasari:
- Emmanuel John (31), maarufu Chifu mkazi wa Kijiji cha Kilulu Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu amehukumiwa kwenda jela miaka 20 na kuchapwa viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki fisi kinyume cha sheria.
Simiyu. Emmanuel John (31), Chifu mkazi wa Kijiji cha Kilulu wilaya ya Bariadi kwenda jela miaka 20 na kuchapwa viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki fisi kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano, Machi 12,2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Caroline Kiliwa baada ya mshtakiwa kukutwa na hatia.
Mshtakiwa huyo ambaye pia ni mganga wa kienyeji, alipewa adhabu hiyo katika kesi iliyokuwa inamkabili kwenye mahakama hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Awali akisoma kosa la mshtakiwa, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa, Lupiana Mahenge alielezea mahakama kuwa Chifu alikutwa na nyara ya Serikali ambayo ni fisi akiwa hai akimfuga nyumbani kwake kinyume cha sheria.
Alisema kuwa Januari Mosi, 2025 katika eneo la Kijiji cha Kilulu Chifu alikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai nyumbani kwake akiwa amemfungia ndani.
Alieleza kuwa aliishi na fisi huyo kama mnyama wake wa kufuga kinyume na kifungu cha 86 (1) kifungu kidogo na cha (2) (C) (III) cha sheria ya kuhifadhi wanyamapori sura ya 283 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Alisema kuwa kifungu hicho kinasomeka pamoja na aya ya 14, jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na kifungu cha 60 (2) cha sheria ya kupambana na uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Upande wa mashitaka katika kuthibitisha kosa hilo ulipeleka mahakamani mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka.
Chifu alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne wakiwemo pacha ndipo hakimu akatoa adhabu hiyo, ili iwe fundisho kwake na watu wengine.