Ahukumiwa kunyongwa kwa kumuua mpenzi wake

Muktasari:
- Grace alitenda kosa hilo Julai 16, 2021 eneo la Mbezi Makabe wilayani Ubungo Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Grace Mushi (25) maarufu kama Neema, baada ya kumtia hatia ya kumuua mpenzi wake, Abdallah Sekamba.
Grace, alimuua mpezi wake kwa kumchoma moto hadi kufa kwa kutumia mafuta ya petrol, baada kumfungia ndani ya nyumba, tukio alilolitenda Julai 16, 2021 eneo la Mbezi Makabe, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Hukumu hiyo ilitolewa leo, Februari 28, 2024 na Jaji Awamu Mbagwa baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka kuwa alitenda kosa hilo.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mbagwa amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa kwa kosa la mauaji na upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wao kwa kuwaita mashahidi 10 pamoja na vielelezo vitano.
Jaji Mbagwa amesema pia upande wa utetezi uliwasilisha shahidi mmoja ambaye ni mshtakiwa mwenyewe.
"Grace, ninakutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka ambao wamethibitisha shtaka pasina kuacha shaka.
"Pia, baada ya kusmikiliza na kupitia ushahidi wako (mshtakiwa) mahakama hii imejiridhisha na hatimaye imekukuta na hatia, hivyo inakuhukumu kifungo cha kunyongwa hadi kufa," amesema Jaji Mbagwa.
Akiendelea kupitia ushahidi, Jaji Mbagwa amesema katika hukumu hiyo, mahakama imezingatia mambo mawili muhimu. Jambo la kwanza, kama mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo kwa marehemu huyo.
"Hakuna ubishi, upande wa mashtaka umeeleza wazi nyumba ya mshtakiwa ndiyo iliyoungua katika kutilia uzito ushahidi huo, shahidi Aziza Juma ambaye ni mpangaji katika nyumba hiyo alieleza jinsi alivyomsikia marehemu akiomba msaada.
"Pia katika ushahidi wa ndugu wa karibu na marehemu walieleza jinsi walivyomtambua ndugu yao pamoja na daktari aliyejaza fomu ya "postmortem" na maungamo kutoka kwa mlinzi wa Amani," amebainisha.
Jaji Mbagwa ameelezea kuwa hata ushahidi wa polisi aitwaye Augustino alieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea akiwa doria na kumkuta mshtakiwa kituo cha Polisi baada ya kuutoa mwili katika nyumba anayokuwa anaishi mshtakiwa.
Kuhusu nia ya kusababisha kifo, Jaji Mbagwa amesema ushahidi unaonyesha wazi marehemu amefariki kwa sababu ya mlipuko wa moto akiwa ndani na mlango uliofungwa kwa nje.
"Hii haina ubishi, japo upande wa mashtaka haujaweka wazi kama mlipuko huo umesababishwa na mafuta ya petroli kweli au kuna vyanzo vingine vya moto," amesema.
Akihitimisha hoja hizo, Jaji Mbagwa amesema kwa kuzingatia hayo mahakama inamtia hatiani bila kuacha shaka yoyote, mshtakiwa Grace na kumhukumu kifungo cha kunyongwa hadi kufa.
"Kama hujaridhika na adhabu hii, una haki ya kukata rufaa," amesema.
Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Frola Massawe, akishirikiana na mawakili wawili wa Serikali, Happy Mwakanyamale na Groly Kilawe uliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo, ili iwe funzo kwake na jamii pia.
Pia, waliomba Mahakama itoe adhabu kali kwa sababu mshtakiwa amekiuka haki za kibinadau, haki za kikatiba na pia amepoteza nguvu kazi ya Taifa.
Hata hivyo, kwa upande wa mshtakiwa kupitia wakili wake, Hilda Mushi aliiomba Mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa, kwani ni mama mwenye watoto wawili wadogo ambao wanamtegemea.
"Pia, mshtakiwa bado ni kijana mwenye kuhitaji kutimiza ndoto zake na pia mtuhumiwa ni mwathiriwa wa moto aliopoteza mali," amesema Mushi.
Hata hivyo, utetezi huo w ulitupiliwa mbali na Jaji Mbagwa na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.