Afariki dunia kwa kufukiwa na kifusi cha choo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo
Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea wakati vijana wakifanya kazi ya kuchimba shimo kwa ajili ya choo baada ya lililokuwepo awali kujaa.
Arumeru. Emmanuel Kilusu maarufu kama ‘Chinga’ (28), mkazi wa Olturoto wilayani Arumeru, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi cha udongo wakati akichimba shimo la choo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema leo Januari 25, 2024 kuwa tukio hili limetokea jana, Januari 24, 2024, muda wa mchana na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa Mount Meru.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kivululu kilichopo kata ya Olturoto, Eliakimu Saimon amesema kijana huyo aliyekuwa na mwenzake, alikuwa akichimba shimo kwa ajili ya kufanywa chemba ya choo.
“Hawa vijana walikuwa wanachimba shimo kwa ajili ya choo baada ya lililokuwepo awali kujaa, sasa ule udongo waliozalisha kwenye hilo shimo walilokuwa wanachimba wakawa wanatupia pembeni ya ile chemba ya awali iliyokuwa imejaa, bahati mbaya udongo ukazidi uzito ikamomonyoka na kumrudia akiwa chini,” amesema.
Amesema tukio hilo ni la tatu kutokea katika kijiji chake ndani ya mwaka mmoja, wamekuwa wakitoa tahadhari juu ya uchimbaji wa shimo karibu na shimo lingine linalotumika, lakini utekelezaji umekuwa mdogo.
“Niwaombe vijana wetu wanaofanya kazi za vibarua wawe wanaangalia pia usalama wao, maana haya matukio yanatokea na ni kutokana na asili ya udongo wetu, hauhimili uzito mkubwa,” amesema.
Kijana aliyenusurika katika tukio hilo, Daniel Shayo “Winga” amesema walikuwa wakifanya kazi na marehemu kabla ya umauti kumkuta na ameshangaa rafiki yake akifunikwa na udongo.
“Tulikuwa tunachimba wawili kwa awamu, mimi nachimba yeye anavuta udongo kule juu, nilivyochoka na yeye akaingia kwa kutumia ngazi akawa anachimba mimi navuta udongo kusogeza pembeni usirudi shimoni, sasa wakati navuta ghafla nikashangaa natitia kumbe Ile chemba ya mwanzo ililemewa na udongo" amesema na kuongeza:
“Shimo tulilokuwa tumechimba lilifika parefu na tukio la kuzama udongo lilikuwa la ghafla ndio maana mwenzangu alishindwa kujiokoa. Nilipiga kelele kuomba msaada wa uokozi, tukashirikiana lakini hadi tunamfikia alikuwa amefariki dunia,” anasema.
Mmiliki wa eneo hilo la kazi, Julius Korei amesema maji ya mvua za mfululizo yalijaza chemba yake ya awali, hivyo akaamua kutafuta vibarua wa kuchimba shimo lingine.
“Hili shimo lilijaa maji ya mvua, hivyo nikaona kuliko kuvuta maji taka bora nichimbe lingine lihamishe miundombinu, baadaye mvua zikikata litakauka tu, ndio nikaita vijana wafanye kazi, lakini kwa bahati mbaya ajali hii ikatokea,” amesema.