Adaiwa kumchoma moto mtumishi wa ndani
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake. Picha na Anania Kajuni
Muktasari:
- Mtumishi huyo anadaiwa kufanyiwa ukatili huo na mwajiri wake ambaye alimtuhumu kuiba Sh161, 000, fedha ambayo ilirejeshwa baadaye.
Mwanza. Mfanyakazi wa nyumbani, Grace Joseph (17) anauguza majeraha katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza baada ya kumwagiwa mafuta ya taa mwilini kisha kuchomwa moto na mwajiri wake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema jeshi hilo linamshikilia mkazi wa Usagara wilayani Misungwi mkoani humo, Christina Shiriri (43) akidaiwa kutenda ukatili huo.
Kamanda Mutafungwa amesema Christina anadaiwa kutenda ukatili huo kwa mtumishi wake baada ya kumtuhumu kuiba Sh161, 000, fedha aliyokuwa ameihifadhi chumbani kwake.
“Mtuhumiwa alidai kuibiwa fedha zake alizokuwa amehifadhi chumbani kwake na alipomuuliza binti yake wa kazi (Grace) alikiri kuchukua fedha hizo na kuamua kumrejeshea. Baada ya kurejeshewa fedha hizo Christina Shiriri aliamua kumfanyia ukatili binti huyo kwa kumchoma moto mikono yote miwili, tumboni pamoja na mapaja yake yote mawili,” amesema Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, upelelezi wa tukio hilo unaendelea huku mfanyakazi huyo akiendelea kupatiwa matibabu .
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi wakati wanapowatuhumu watu wanaofanya makosa, badala yake wawafikishe kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua za kisheria,” amesema kamanda huyo.
Wakati hayo yakijiri, viongozi wa dini mkoani Mwanza wakizungumza na Mwananchi Digital leo katika semina ya kuwajengea uelewa kuhusiana na wafanyakazi wa ndani kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi wa Ndani inayofanyika kila mwaka Juni 16, wamelaani tukio hilo huku wakiwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
"Inasikitisha hasa unaposikia matukio ya unyanyasaji, mateso na vipigo kwa mabinti wa kazi, hii haikubaliki kabisa kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mtu akikosea sio vyema kujichukulia sheria mkononi bali ni vyema sheria zichukuliwe ili haki itendeke na kila mmoja apokee adhabu kulingana na makosa yake," amesema Askofu Beatus Mlozi kutoka Kanisa la Waadventisti Wasabato Jimbo la Nyanza Kusini.
Akiunga mkono hoja hiyo Mratibu Kamati ya Amani Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza na Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Mkoa wa Mwanza, Sheikh Twaha Bakari, amewataka waajiri na wananchi kufuata taratibu na sheria za nchi pindi yanapotokea matukio kama hayo.
"Nitoe ushauri kwa wananchi kama yakitokea mambo kama hayo wafuate haki na sheria za nchi au wafuate utaratibu ambao unatuagiza namna ya kuishi na kufuata taratibu za kisheria za nchi lakini pia za dini," amesema Sheikh Bakari
Kwa upande wake Meneja Màkao Shirika la WoteSawa katika Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma, Jacquline Ngalo amesema matukio hayo yanatokea kwa sababu wafanyakazi wa ndani na waajiri hawajui haki na wajibu wao na hivyo kusababisha kufanyiana ukatili.