Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Adaiwa kukatwa kiganja na mtalaka wake

Mkami Maseke (43) akiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kulia na mtu anyedaiwa kuwa ni mume wake wa zamani. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, mjini Musoma kwa matibabu

Musoma. Mkami Maseke (43) amejeruhiwa kwa kukatwa kiganja cha mkono wa kushoto na mtu anayedaiwa alikuwa mumewe.

Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Kurusanga, wilayani Bunda mkoani Mara.

Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, mjini Musoma kwa matibabu.

Mbali na kupoteza kiganja, mama huyo mwenye watoto watatu pia amejeruhiwa katika mkono wake wa kulia na kusababisha mfupa wa kiganja kuvunjika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema jeshi hilo linaendelea kumtafuta mtuhumiwa anayedaiwa kutoroka baada ya kutekeleza kitendo hicho.

Dk Elias Nguti wa Kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara amesema leo Jumatano, Juni 10, 2026 kuwa majeruhi huyo atalazimika kupata matibabu kwa awamu mbili, ikiwamo kusafisha majeraha na kuunganisha mfupa uliovunjika.

Amesema awamu ya pili inatarajiwa kufanyika baada ya wiki mbili na atafanyiwa upasuaji wa kuwekea vyuma vya kuunganisha mfupa huo uliovunjika.

Akizungumza akiwa amelazwa hospitalini, Maseke amesema tukio hilo lilitokea Juni 8, 2026  saa sita mchana katika Kijiji cha Kurusanga, wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Maseke amedai kuwa siku ya tukio alikwenda shambani asubuhi kwa ajili ya kupalilia mihogo,  baada ya kumaliza kazi hiyo alipokuwa akijiandaa kurejea nyumbani, ghafla alivamiwa na aliyekuwa mume wake na kuanza kumshambulia kwa panga.

"Alifika na kunyanyua panga akitaka kunikata kichwani nikakinga mkono wa kushoto, alinikata mara nne kiganja kikadondoka akaendelea kunikata tena nikanyanyua mkono wa kulia kijikinga akaendeela kunikata tena mara mbili," amesema.

Mkami amesema baada ya mtuhumiwa kuona wananchi wameanza kufika eneo la tukio kufuatia kelele zake za kuomba msaada, alikimbia na kuacha viatu vyake eneo la tukio.

Amesema aliishi katika ndoa na mtuhumiwa huyo kwa miaka 16 na walibahatika kupata watoto watatu, wote wa kike.

"Ndoa yetu ilianza kupata changamoto baada ya miaka mitano na kuanzia hapo ikawa ni vipigo kila mara huku nikishindwa kuhudumia familia," ameeleza.

Amesema baada ya jitihada za kusuluhisha ndoa hiyo kushindikana, Aprili mwaka huu aliamua kuondoka na kurejea nyumbani kwao kuishi na wazazi wake.

Mkami amesema baada ya kuvunjika kwa ndoa akiwa nyumbani kwao, mwanamume huyo alimpigia simu na kumtaka amrejeshee mahari ili aweze kuoa mwanamke mwingine atakayewatunza watoto wao.

"Nilipoondoka niliwaacha watoto kwake na alipoona sina mpango wa kurudi kwake alinipigia simu akitaka nimrudishie mahari na tulikubaliana nimpe Sh600,000 kama thamani ya ng'ombe wawili ingawa yeye wakati ananioa alitoa ng'ombe wanne kama mahari," amesema.

Amesema baada ya makubaliano hayo aliuza mazao yake ya shambani ikiwamo mihogo na mtama na kupata kiasi cha fedha alichomkabidhi mwanamume huyo mbele ya uongozi wa kijiji Mei mwaka huu.

Mkami amesema aliamini kuwa baada ya kurejesha fedha hizo angekuwa huru, hivyo ameshangazwa na uamuzi wa aliyekuwa mume wake wa kumshambulia kwa mapanga.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwimange, George Saranga amesema wanandoa hao walikuwa wakifika ofisini kwake mara kadhaa kwa ajili ya kusuluhisha migogoro yao ya ndoa.

Ameeleza kuwa mwanamume alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa na uhusiano ya kimapenzi na mwanamume mwingine, jambo lililosababisha kumfanyia vipigo vya mara kwa mara.

"Chanzo kikubwa ilikuwa ni simu, mara nyingi alikuwa akimuona mke wake akiongea na simu yeye alikuwa anahisi anaongea na mwanamume mwingine,  nakumbuka kesi yao ya mwisho alipasua simu kabla ya kumpiga mke wake," amesema.

Ndugu wa majeruhi, Bunuri Julius amesema kiganja cha ndugu yao kilipatikana baadaye baada ya kutafutwa kwa muda mrefu na kilipelekwa kituo cha polisi kisha hospitalini kabla ya baadaye kukirudisha nyumbani na kukizika.

Amesema ndugu yao alikuwa akilalamika mara kwa mara kuhusu vipigo kutoka kwa mume wake, malalamiko ambayo yalijaribiwa kupatiwa suluhu lakini hatimaye ndoa ikaendelea kuwa na migogoro hadi kuvunjika.