Adai kubomolewa nyumba na ndugu, kisa mgogoro wa ardhi

Makorwa Omollo akiangalia nyumba yake iliyobomolewa na ndugu zake kwa madai ya kuwepo kwa mgogoro wa ardhi baina yao katika kijiji cha Kisumwa wilayani Rorya. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Ndugu watatu wamedaiwa kubomoa nyumba ya Omollo alipokuwa kaenda Tarime mjini
Rorya. Mkazi wa Kijiji cha Kisumwa wilayani Rorya Mkoa wa Mara, Makorwa Omollo (48) amedai kubomolewa nyumba na ndugu zake chanzo kikiwa mgogoro wa ardhi.
Akizungumza katika eneo la tukio, leo Jumanne Julai 23, 2024, Omollo amesema kutokana na tukio lililotokea mwishoni mwa wiki, maisha yake yako shakani, huku akiomba Serikali imsaidie.
Omollo amedai kuwa siku ya tukio ndugu zake hao walifika nyumbani kwake mchana wakiwa na pikipiki mbili, lakini hawakumkuta alikuwa ameenda Tarime mjini kununua vifaa vya ujenzi.
Amesema kumekuwa na mgogoro baada ya yeye kutaka kujenga nyumba eneo wanalogombea.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Mark Njera amesema ndugu hao ambao majina yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Omollo chanzo kikiwa mgogoro wa kifamilia unaohusisha ardhi.
"Hakuna anayeshikiliwa ila tayari tumeweka mazingira salama kwa mlalamikaji na uchunguzi tayari umeanza. Taarifa za awali ni kwamba, hawa watu watatu walivamia nyumbani kwa ndugu yao wakiwa na mapanga wakidaiwa kutaka kumshambulia, lakini ndugu yao hakuwepo nyumbani muda huo, badala yake wakabomoa nyumba yake iliyojengwa kwa nyasi na miti," amesema Kamanda Njera.
Amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa ndugu hao hawakubaliani na uamuzi wa Omollo wa kutaka kujenga nyumba katika ardhi hiyo.
Baadhi ya mashuhuda wamesema siku hiyo watu watatu wakiwa na pikipiki mbili walifika kwenye mji huo wakimtaka Omollo atoke nje.
"Walifika na kupaki pikipiki zao na watu wawili wakashikilia mapanga wakawa wanamuita Omollo atoke nje, lakini bahati nzuri Omollo hakuwepo nyumbani muda huo," amesema Melvin Sharon.
Shuhuda mwingine, Zainabu Ogola amesema baada ya kumkosa Omollo, watu hao walianza kubomoa nyumba iliyokuwa ikiendelea kujengwa.
"Wawili walianza kukatakata nyumba na mmoja akawa anawaelekeza namna ya kubomoa na walifanya hivyo wakidai hawataki Omollo ajenge katika eneo hili," amedai Zainabu.
Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kisumwa, Magori Wambura amesema kitendo kilichofanywa na watu hao hakikubaliki, huku akifafanua kuwa eneo linalosababisha mgogoro lina ukubwa wa zaidi ya ekari 50.
Amesema Serikali ya kijiji hicho inalaani kitendo hicho kwa sababu kungeweza kutokea uvunjifu wa amani endapo wanakijiji wangeamua kujitokeza kukabiliana nao.
"Hawa walikuja kama wavamizi, sasa hebu fikiria kama watu wangepiga yowe ina maana wanakijiji wangejitokeza kukabiliana nao, au wangemkuta huyo waliyekuwa wakimtafuta si wangemuua kwa kumkatakata na mapanga," amesema Wambura.