ACT- Wazalendo wamtwisha Rais Samia zigo la miswada ya sheria za uchaguzi

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji
Muktasari:
Ni miswada iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023. Chama kimedai kuwa haijatimiza haja na mategemeo ya wadau..
Geita. Chama cha ACT-Wazalendo kimemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kutoridhia miswada ya Sheria za Uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023 kwa kuwa haijatimiza haja na mategemeo ya wadau, na kwamba endapo sheria hizo zitapitishwa basi uchaguzi mkuu ujao unaweza kuwa wa vurugu.
Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji ameyasema hayo jana Jumapili, Januari 14, 2024 mara baada ya kumalizika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa uliofanyika mjini Geita.
Amesema chama hicho ni miongoni mwa wadau waliotoa maoni yao kwenye kikosi kazi na kutegemea kuona mabadiliko na sheria kuwa nzuri inayotoa nafasi kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, lakini kilichotokea ni baadhi ya maoni ya wadau kuwekwa kando na mambo kuendelea kama yalivyokuwa.
“Sisi tumekuwa na malalamiko mengi kuhusu zile sheria…Tulitegemea baada ya mjadala wa kikosi kazi na mjadala wa wadau, sheria iwe nzuri zaidi na kutoa nafasi ya kufanya uchaguzi huru wa 2025,” amesema na kuongeza:
“Sisi tuliona bora tukaseme maoni yetu kwenye kikosi kazi na kwenye kikao cha wadau tulipeleka kitabu kizima cha jinsi sheria zile zibadilikeje na tulikabidhi kwenye kikosi kazi, lakini ni maoni machache sana yamekubaliwa kwa ujumla sheria zile zilivyo hazikidhi.’’
Amesema kama chama wameshatoa maoni yao bungeni ya kuwa sheria hizo hazikidhi ile falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R iliyotaka maridhiano, kustahimiliana, kubadilisha mambo na kujenga upya.
“Kwenye falsafa hizi za 4R, ile sheria haijafikiria hata moja, falsafa ya Samia inasema mengine na watunga sheria wamebaki na yaleyale,” amesema Duni.
Kuhusu uamuzi wa Chadema kufanya maandamano ya amani, mwenyekiti huyo amesema kila chama kina utaratibu wake, na kuwa wao walitoa maoni na kwenda bungeni kwenye kamati.
Amesema hali ilipofika sasa, Rais Samia anapaswa kutoziacha sheria hizo kupitishwa kama zilivyo kama kweli alidhamiria falsafa yake ya 4R.
Uchaguzi ulivyokuwa
Katika uchaguzi huo, Lucas Tibengana alipita bila kupingwa na kuwa mwenyekiti wa chama hicho baada ya kuteuliwa kuwa mgombea pekee kutokana na mshindani wake Emmanuel Otto kuenguliwa na kamati ya uchaguzi, muda mfupi kabla ya yeye kusimama kujinadi kwa wapiga kura.
Akizungumza baada ya kupita bila kupingwa mwenyekiti huyo mpya, aliwashukuru wapiga kura na kusema kazi kubwa kwake ni kukijenga chama na kuhakikisha wanapata ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kwa upande wa Otto amesema alifuata taratibu zote zinazotakiwa na kuwa anashangazwa kupewa barua dakika za mwisho akiwa ukumbini na kuwa pamoja na kuondolewa, lakini hajapewa tuhuma zinazomhusu na hajui sababu za yeye kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho.